Waandishi 76 wako kwenye Msafara wa Papa Sri Lanka!
Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa njiani kuelekea nchini Sri Lanka, amewatakia
matashi mema, heri na baraka waandishi wote ambao wako kwenye msafara wake huko Sri
Lanka na baadaye Ufilippini, kwani wanayo kazi kubwa mbele yao ili kuhakikisha kwamba,
watu wanaweza kusikia kwa ufasaha yale yanayojiri katika hija yake ya kitume Barani
Asia.
Kabla ya kusalimiana na mwandishi mmoja mmoja na kubalishana naye mawili
matatu; Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican amemwambia Baba Mtakatifu
kwamba, msafara wake una ambatana na waandishi wa habari 76 na kati yao 14 wanatoka
nchini Ufilippini, kwani kuna umati mkubwa wa watu wanaotarajia kusikia mengi wakati
Baba Mtakatifu atakapowatembelea nchini mwao kuanzia tarehe 16 Januari 2015 hadi tarehe
19 Januari 2015 atakaporejea tena mjini Vatican.
Kuna waandishi wawili wa magazeti
kutoka Ufaransa ambao hawakuweza kushiriki katika msafara wa Baba Mtakatifu kutokana
na sababu za kiufundi, zilizowalazimu kubaki nchini Ufaransa baada ya matukio ya kigaidi
yaliyoutikiza ulimwengu hivi karibuni.
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko
hakuweza kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka kama ratiba ilivyopangwa
kutokana na muda kuwatupa mkono na hivyo kulazimika kwenda kupata chakula cha mchana
kwenye Ubalozi wa Vatican na Kardinali Pietro Parolin pamoja na msafara mzima wa Baba
Mtakatifu kushiriki chakula cha mchana pamoja na Maaskofu Katoliki Sri Lanka.
Baba
Mtakatifu Francisko akiwa njiani kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Colombo kuelekea
kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Sri Lanka, umbali wa kilometa 28, amekutana na umati
mkubwa wa watu uliokuwa umejipanga pembeni mwa barabara, kumshangilia wakati alipokuwa
anapita.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.