2015-01-13 14:59:25

Majadiliano ya kidini na kiekumene yajenge na kudumisha ushirikiano


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne jioni tarehe 13 Januari 2015 amekutana na kuzungumza na viongozi wa dini mbali mbali walioko nchini Sri Lanka. Itakumbukwa kwamba, nchi hii inaundwa na waamini wa dini ya Kibudha, Kihindu, Kiislam na Kikristo. Ni hija ambayo inajikita katika hija inayofanywa na Mama Kanisa katika mchakato wa kuheshimu na kuwapenda watu na imani na tamaduni zao, kama alivyofanya Mwenyeheri Paulo VI na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Baba Mtakatifu anasema, katika hija hii anapenda kuwaimarisha Wakatoliki katika imani, kwa kushiriki nao katika furaha na mahangaiko yao. Anapenda kushirikishana na viongozi wakuu wa dini mbali mbali, hekima, ukweli na utakatifu wa maisha. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wameonesha heshima kwa dini mbali mbali na kwamba, Kanisa linapenda kushirikiana na wote kwa ajili ya mafao ya wengi nchini Sri Lanka.

Baba Mtakatifu anasema, anapenda kwa namna ya pekee kabisa kuimarisha na kudumisha mchakato wa majadiliano na ushirikiano wa kidini na kiekumene, kwani, ufanisi wa majadiliano na utamaduni wa watu kukutana unahitaji watu kushirikishana imani yao, katika ukweli, uwazi na uaminifu, ili hatimaye, kutambua mambo msingi ambayo yanawaunganisha na kuwaimarisha katika umoja. Hapa kutakuwepo na njia mpya zitakazosaidia watu kuheshimiana, kushirikiana na kudumisha urafiki.

Baba Mtakatifu anasema, kuna haja kwa watu wenye mapenzi mema kutoa kipaumbele cha kwanza katika majadiliano na ushirikiano katika medani mbali mbali za maisha ya wananchi wa Sri Lanka. Kwa miaka mingi watu wengi wameteseka kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na kinzani. Sasa kuna haja ya kuanza mchakato wa upatanisho na umoja wa kitaifa kwa kuondokana na kinzani pamoja na migawanyiko kati ya watu. Mafao ya wengi na mahitaji ya familia ya binadamu, yapewe nafasi ya kwanza.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, majadiliano na ushirikiano wa kidini na kiekumene, yatamiwlishwa katika uhalisia watu kwa kujenga na kudumisha utulivu unaojikita katika udugu, kwani kwa kufanya hivi hakuna mtu au kikundi kinachoweza kupoteza utambulisho wake wa kikabila na kidini.

Baba Mtakatifu anasema, kuna changamoto na mahitaji makubwa yanayoweza kutekelezwa katika mazingira ya mshikamano na ushirikiano. Haya ni mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili na hasa katika kipindi hiki ambacho familia nyingi zinakumbana na athari za mtikisiko wa uchumi kimataifa, kuna ongezeko kubwa la umaskini, watu kuendelea kutengwa na wengine kuomboleza kutokana na kuondokewa na ndugu na jamaa zao.

Baba Mtakatifu anasema, wakati huu katika historia ya Sri Lanka, wananchi wengi wanasubiri kuona mchakato wa ujenzi wa msingi wa maadili kijamii. Ushirikiano kati ya viongozi mbali mbali wa dini unaweza kuwa ni alama na kielelezo makini cha upatanisho kwa wananchi wote wa Sri Lanka, katika jitihada za kupyaisha jamii na taasisi zake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, si vyema kukufuru kwa kutumia dini kuhalalisha vita na kinzani. Hapa viongozi wa kidini wanapaswa kuwa wakweli na makini, ili kuongoza jumuiya katika njia ya amani kwa kulaani kwa macho makavu matendo ya vurugu na vita yanapojitokeza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican







All the contents on this site are copyrighted ©.