2015-01-13 15:10:59

Huruma na upendo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linasema, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 19 Januari 2015. itaongozwa na kauli mbiu ”huruma na upendo”. Baba Mtakatifu Francisko anakuwa ni Papa wa tatu kutembelea Ufilippini. Kwa mara ya kwanza hija za kichungaji nchini humo zilizinduliwa na Mwenyeheri Paulo VI, yapata miaka arobaini na nne iliyopita, yaani kuanzia tarehe 27 hadi 29 Novemba 1970, Papa Paulo VI alikuwa mjini Manila.


Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alibahatika katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kutembelea Manila mara mbili. Mara ya kwanza ilikuwa ni tarehe 17 hadi tarehe 22 Februari 1981 na mara ya pili ilikuwa ni tarehe12 hadi tarehe 16 Januari 1995. Kumbe, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko inakuja baada ya takribani miaka ishirini baada ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, iliyofanyika Jimbo kuu la Manila na kuwakutanisha vijana zaidi millioni tano kutoka sehemu mbali mbali za dunia; vijana ambao wengi wao leo hii wamekuwa ni Mapadre na Watawa kadiri ya shuhuda mbali mbali zilizowahi kukusanywa.


Hili ni tukio ambalo liliacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki nchini Ufilippini, hadi leo hii, bado wengi wanalikumbuka tukio hili. Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini linasema, vijana ni moto wa kuotea mbali nchini mwao na wataka kwa mara nyingine tena kuonesha maajabu kwa walimwengu, kwa kumpokea na kumkarimu Baba Mtakatifu Francisko atakapowatembelea.


Ni mwaliko wa kujiandaa kikamilifu kwa njia ya tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma kwa kutambua kwamba, Ufilippini ni kati ya nchi ambazo zimeathirika sana kutokana na majanga asilia. Kardinali Louis Antonio G. Tagle wa Jimbo kuu la Manila anasema, wananchi kutoka Barani Asia wanampenda na kumthamini sana Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, wamepokea taarifa ya hija yake ya kichungaji kwa mikono miwili na kwamba, safari kadiri siku zinavyozidi kusogea imekuwa ni “gumzo” kwenye vyombo vya habari nchini Ufilippini.


Waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka Ufilippini watabahatika kuonana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ana kwa ana baada ya kukutana nao kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alipokuwa anabariki Sanamu ya Mtakatifu Pedro Calungsod. Ni kiongozi aliyeonesha mshikamano wake wa dhati wakati ule Ufilippini ilipokumbwa na tufani ya ya Yolanda.


Huruma na Upendo ni mambo msingi yanayoongoza maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wakati huu, mwaliko kwa waamini pia kuongozwa na tunu hizi msingi katika hija ya maisha yao ya kiroho, katika hali ya unyenyekevu na huruma, kwa kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii kabla ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao.


Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.