2015-01-13 09:06:07

Askofu ni mwalimu wa imani na maadili!


Kardinali Gerhard L. Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa katika hotuba yake kwa Marais wa Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, wanaokutana mjini Esztergom, Hungaria kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 15 Januari anakumbusha kwamba, Maaskofu kimsingi ni walimu wa imani na kwamba, wanafanya mkutano wao nchini Hungaria, nchi ambayo ina utajiri mkubwa wa imani, maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Muller anasema msingi na maana ya huduma ya mafundisho tanzu ndani ya Kanisa inajikita katika Yesu Kristo, Mkombozi wa Ulimwenguni, ambaye anawaalika wafuasi wake kuwa ni mashuhuda wa ukweli katika imani iliyofunuliwa kwao kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Kutokana na ukweli huu, taalimungu inaishi na kumwilishwa na imani, changamoto kwa wanataalimungu kushirikiana kwa karibu zaidi na viongozi wa Kanisa, kwa ajili ya ustawi wa Kanisa na maendeleo ya Familia ya Mungu: kiroho na kimwili.

Utume wa mamlaka ya ufundishaji katika Kanisa umefungamana kwa hali halisi ya agano ambalo Mwenyezi Mungu amelianzisha pamoja na Taifa lake. Kazi ya kichungaji ya mamlaka ya ufundishaji katika Kanisa ipo pia kwa ajili ya kukesha ili Taifa la Mungu lidumu katika ukweli unaowafanya huru. Ili kutekeleza utume huu, Kristo amewapa wachungaji karama ya kutokosea katika mambo ya imani na maadili. Utekelezaji wa karama hii waweza kuwa wa namna nyingi.

Khalifa wa Mtakatifu Petro, kichwa cha urika wa Maaskofu anayodhamana nyeti ya kuwaimarisha ndugu zake katika imani na maadili mintarafu Neno la Mungu na utii kwa kutambua kwamba, Khalifa wa Mtakatifu Petro ni Mtumishi wa Watumishi wa Mungu. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa lipo kwa ajili ya kumsaidia Baba Mtakatifu kutekeleza dhamana na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu; kwa kulinda na kudumisha umoja wa Kanisa sanjari ya kusaidia mchakato wa kukuza na kuimarisha imani katika ukweli.

Maaskofu wanapaswa kulinda na kutunza imani na maadili ya Wakristo; kwa njia ya mafundisho yao huku wakiendelea kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kutambua matatizo na changamoto mbali mbali zinazowakabili Maaskofu mahalia, walikazia umuhimu wa kuanzishwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kitaifa na Kikanda, kama sehemu muhimu sana ya kuweza kubadilishana mang'amuzi na maoni katika ushirikiano mtakatifu, unaopania neema ya Kanisa zima.

Kardinali Muller anasema ushirikiano kati ya Maaskofu katika urika wao unapaswa kujionesha kwa Makanisa mahalia na kwa Kanisa la Kiulimwengu. Khalifa wa Mtakatifu Petro ni chanzo, msingi dumifu na mwonekano wa umoja wa Maaskofu na Waamini katika ujumla wao. Baba Mtakatifu huwakilisha Kanisa zima katika kifungo cha amani, upendo na umoja.

Wataalam wa masuala ya kitaalimungu wanaweza kuwa ni wanachama wa Tume ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa, lakini ikumbukwe kwamba, hii ni dhamana kwanza kabisa kwa Maaskofu. Tume hizi zinapaswa kuwasaidia Maaskofu katika kutekeleza dhamana yao ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza Watu wa Mungu.

Kumbe, Tume hizi pia zinapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, ili kurahisisha mchakato wa kuwatangazia Watu Injili ya Furaha. Tume hizi zinafanya kazi kwa idhini ya Maaskofu baada ya kupata ridhaa kutoka kwa Maaskofu.

Lengo ni kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa kwa kutambua kwamba, wote ni sehemu ya Familia ya Mungu inayowajibika katika utofauti wake. Viongozi wa Kanisa wajifunze kujiachilia mikononi mwa Yesu Kristo, Mwalimu mwaminifu anayepyaisha imani na kuipatia utimilifu wake, kwa ajili ya mafao ya Watu wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.