2015-01-13 09:35:26

Acheni ubaguzi, hata Nigeria kuna watu wanakufa!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasikitishwa sana na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kutendeka nchini Nigeria hata kwa kuwatumia watoto wadogo katika mashambulizi ya kujitoa mhanga yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram, ambacho kwa sasa kimekuwa chanzo kikuu cha majanga, mateso na mahangaiko ya wananchi wa Nigeria na katika nchi jirani!

Mabomu ya kujitoa mhanga ambayo chanzo chake kikuu ni misimamo mikali ya kidini ni jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa cha dini yenyewe ambayo kimsingi inapaswa kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha amani. Hakuna sababu inayoweza kukubalika kwa kufanya mashambulizi ya kigaidi ambayo hivi karibuni yamepelekea watu zaidi ya elfu mbili kupoteza maisha yao nchini Nigeria.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kuunganisha sauti yake na ile ya viongozi mbali mbali wa kidini waliokemea kwa nguvu zote mauaji ya watu wasiokuwa na hatia nchini humo. Baraza la Makanisa linaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuonesha mshikamano wa dhati na wananchi wa Nigeria ambao wanakabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram. Inasikitisha kuona kwamba, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia nchini Nigeria, si habari tena yenye mvuto na mashiko kutoka kwenye vyombo vya habari vya kimataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema, Jumuiya ya Kimataifa imeonesha mshikamano mkubwa na Ufarasana pale waliposhambuliwa na magaidi na hivyo kusababisha vifo vya watu kumi na saba! Lakini jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, watu wanaendelea kupoteza maisha yao nchini Nigeria kutokana na mashambulizi haya haya ya kigaidi, lakini wakuu wengi kutoka Jumuiya ya Kimataifa wamekaa kimya, jambo ambalo si haki kabisa!







All the contents on this site are copyrighted ©.