Mshikamano wa kimataifa dhidi ya vitendo vya kigaidi!
Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, zaidi ya viongozi wakuu wa Serikali arobaini
wameshiriki katika maandamano ya amani mjini Paris, Ufaransa, siku ya Jumapili jioni,
tarehe 11 Januari 2015 ili kupinga vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kuhatarisha
amani, usalama na ustawi wa watu wengi pamoja na kuendelea kukazia uhuru wa kujieleza.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa amewashukuru viongozi wakuu wa Serikali
kwa kuonesha umoja na mshikamano katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi, vilivyosababisha
watu 17 kupoteza maisha yao nchini Ufaransa, hivi karibuni.
Waandamanaji zaidi
ya millioni mbili walionekana kwenye mitaa kadhaa nchini Ufaransa kupiga vitendo vya
kigaidi. Maandamano kama haya yamefanyika pia katika sehemu mbali mbali za dunia.
Viongozi wakuu wa nchi wameshiriki katika maandamano haya ili kuonesha umoja na mshikamano
wa kimataifa dhidi ya vitendo vya kigaidi, kwa kulinda na kuendeleza uhuru wa mtu
kujieleza kadiri ya Katiba ya nchi!
Wakati huo huo, vikosi vya ulinzi na usalama
kutoka Ufaransa vinaendelea kumsaka kwa udi na uvumba msichana Hayat Boumedienne anayesadikiwa
kuhusika kwa karibu zaidi na vitendo vya kigaidi mjini Paris, Ufaransa.