2015-01-12 08:38:51

Mkutano wa majadiliano kuhusu mafundisho tanzu ya Kanisa!


Viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu ya Kanisa kuanzia tarehe 13 hadi tarehe 15 januari 2015 watakutana na kuzungumza na Marais wa Tume za Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, mkutano unaofanyika huko Esztergom nchini Hungaria.

Itakumbukwa kwamba, ni Mwenyeheri Papa Paulo VI kunako mwaka 1967 alipoagiza kwamba, Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia sanjari na Maaskofu mahalia kuhakikisha kwamba, wanaunda Tume ya Mafundisho Tanzu ya Kanisa katika maeneo yao. Ili kuimarisha mahusiano kati ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Tume hizi za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika ngazi ya Kibara, kunako mwaka 1982, ikaamriwa kwamba, kuwepo na mikutano hii, inayowawezesha viongozi waandamizi wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kujadiliana kwa kina na mapana masuala ya kiimani yanayojitokeza katika Mabara husika.

Mikutano kama hii kwa ajili ya Amerika ya Kusini imefanyika kunako mwaka 1984 huko Bogotà; kunako mwaka 1987 mkutano kwa ajili ya Bara la Afrika ulifanyika mjini Kinshasa na kwa Bara la Ulaya, mkutano ulifanyika kunako mwaka 1989 huko Vienna, Austria. Mkutano kwa ajili ya Bara la Asia, ulifanyika kunako mwaka 1993 huko Hong Kong. Mkutano mwingine wa viongozi wakuu ulifanyika Guadalajara, kwa ajili ya Amerika ya Kusini kunako mwaka 1996 na mwaka 1999, viongozi hawa wakakutana kuno San Francisco, Marekani.

Mikutano hii yote imekuwa ikifanyika nchini ya uongozi wa wakati huo Kardinali Joseph Ratzinger. Kardinali William Levada alifanikiwa kuandaa mkutano wa viongozi wakuu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwa ajili ya Bara la Afrika kunako mwaka 2009 na mkutano huu ulifanyika Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Lengo kuu la mikutano hii anasema Kardinali Gerhard L. Muller, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwamba, ni kusaidia kulinda, kutunza na kudumisha mafundisho tanzu ya Kanisa, na kama ambavyo anakazia Baba Mtakatifu Francisko, pamoja na kuangia matatizo na changamoto zinazowakabilia waamini katika maisha na utume wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.