Lengo ni Uinjilishaji kwa cheche za majadiliano ya kidini!
Kardinali mteule Francis Xavier Kriengsak Kovithavanij, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la
Bangkok, Thailand anasema, Baba Mtakatifu Francisko anafanya hija yake ya kitume akiwa
na Injili pamoja na cheche za majadiliano ya kidini, ili kulinda na kudumisha utu
na heshima ya binadamu, upendo na mshikamano kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.
Kanisa la kiulimwengu linaendelea kuonesha matumaini makubwa kwa Bara la Asia
ambalo lina matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazohitaji mchakato wa majadiliano
ya kidini na kitamaduni, ili kweli imani ya Kikristo iweze kuota mizizi katika maisha
na vipaumbele vya waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Mtakatifu Yohane Paulo
II aliwahi kusema kwamba, Uinjilishaji Barani Asia ni kati ya changamoto kubwa kwa
Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, licha ya ukweli kwamba,
Wakristo ni kundi dogo sana wakilinganishwa na waamini wa dini kuu zilizoko Barani
Asia.
Uinjilishaji Barani Asia unajikita katika mchakato wa majadiliano ya
kidini kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko! Haya ni majadiliano yanayopaswa
kujikita katika uhalisia wa maisha, kwa kutekeleza kwa kina na mapana changamoto zilizotolewa
na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, yaani majadiliano yaguse uhalisia wa
maisha ya watu. Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand katika mkutano wake wa mwaka,
utakaofanyika mwezi Aprili 2015 utajikita zaidi katika Uinjilishaji mpya sanjari na
majadiliano ya kidini.
Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi
na teknolojia, jambo linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza anasema Kardinali mteule
Francis Kovithavanij ni majiundo makini, ya awali na endelevu kwa waamini, ili kamwe
wasimezwe na malimwengu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu
kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji katika uhalisia wa maisha.
Hija ya kitume
ya Baba Mtakatifu Barani Asia ni chachu kubwa kwa maendeleo ya waamini na watu wote
wenye mapenzi mema Barani Asia, kwani ni kiongozi anayependwa na kuthaminiwa na wengi
kutokana na mfano na unyofu wa maisha yake; ni kiongozi anayebeba ndani mwake Injili
ya Furaha ambayo anataka kuimegea Familia ya Mungu Barani Asia. Ni matumaini ya Kanisa
nchini Thailand kwamba, iko siku, Khalifa wa Mtakatifu Petro, atawatembelea ili kuwaimarisha
katika imani, matumaini na mapendo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.