Hotuba ya Baba Mtakatifu kwa Mabalozi mjini Vatican!
Amani duniani, utandawazi usiojali utu na heshima ya binadamu; utumwa mamboleo, vita
na kinzani sehemu mbali mbali za dunia; vitendo vya kigaidi na athari zake; vita Barani
Afrika; vitendo vya ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia; umuhimu wa kuwahudumia wagonjwa
wa Ebola kwa kuthamini utu na heshima yao kama binadamu; wakimbizi na wahamiaji; kazi
na familia; hija ya kitume Barani Asia; matunda ya amani na mahusiano ya kidiplomasia
kati ya Marekani na Cuba pamoja na kutunza mazingira kwa kukataa kishawishi cha vita
duniani!
Haya ni kati ya mambo muhimu ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyakazia
wakati alipokutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya
Kimataifa mjini Vatican, Jumatatu asubuhi, tarehe 12 Januari 2015 kabla ya kuanza
hija yake ya kitume Barani Asia. Itakumbukwa kwamba, Vatican ina uhusiano wa kidiplomasia
na Nchi 180 duniani.
Baba Mtakatifu ameanza hotuba yake kwa kukazia amani
ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayodhihirishwa kwa Fumbo
la Umwilisho, linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo
na ufufuko wa Kristo. Simulizi la kuzaliwa kwa Mtoto Yesu linaloonesha ugumu wa mioyo
ya wanadamu, hali ambayo bado inajitokeza hata leo hii, kwani watu wanashindwa kuangaliana
na kupokeana kama ndugu, matokeo yake ni kuendeleza utandawazi usiojali unaopelekea
kinzani, vita na kifo kama ilivyojionesha huko Paris, Ufaransa.
Hapa anasema
Baba Mtakatifu, kunazaliwa ubinadamu ambao umesheheni majeraha kutokana na kuendelea
kuwepo kwa kinzani na vita kama alivyofanya Mfalme Herode, kwa kuwauwa watoto wote
mjini Bethlehemu. Baba Mtakatifu anasema, inasikitisha kuona kwamba, vitendo kama
hivi vimetendeka hivi karibuni huko Pakistan.
Baba Mtakatifu anazungumzia pia
kuhusu utumwa mamboleo unaojionesha katika mitindo, madaraka, uchu wa mali na fedha
na udini; utumwa mamboleo unaoibuka kutoka katika moyo wa mwanadamu unaoelemewa na
dhambi, kiasi cha kushindwa kuona na kutenda mema, ili kulinda na kudumisha amani.
Zote hizi ni dalili za utamaduni wa utumwa mamboleo unaoendeleza kinzani kama vita
ya dunia inayoendelea kusababisha majanga makubwa.
Baba Mtakatifu anazungumzia
vita inayoendelea nchini Ucrain, ambayo kwa sasa imegeuka kuwa ni uwanja wa fujo.
Hapa kuna haja ya kujenga utamaduni wa majadiliano ili kuondokana na uadui ambao umejengeka
kati ya watu, kwa kuwahusisha wadau wakuu, ili kuanza mchakato wa majadiliano katika
hali ya kuaminiana mintarafu sheria za kimataifa.
Baba Mtakatifu Francisko
ametumia fursa hii ya kukutana na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa
kuonesha masikitiko yake kutokana na vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati, Iraq
na Syria na kwamba, Kanisa kamwe halitachoka kuombea amani, hata kama ule mkutano
wa sala uliowashirikisha viongozi wakuu wa Serikali ya Israeli na Palestina uliofanyika
mwaka 2014 mjini Vatican haujazaa matunda yanayokusudiwa, bado anapenda kuwaalika
viongozi wakuu wa Israeli na Palestina kuishi katika misingi ya amani kwa kutambua
itifaki ya mataifa mawili.
Baba Mtakatifu anasikitishwa mno na mateso ya watu
huko Iraq na Syria kutokana na vita inayoendelea kiasi cha kuibua vitendo vya kigaidi
vyenye mwelekeo wa misimamo mikali ya kidini; vitendo vinavyomkataa Mwenyezi Mungu
na binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wake. Haya ni matokeo ya utamaduni usiojali
wala kuguswa na mahangaiko ya watu.
Vitendo vya kigaidi vimekuwa na madhara
makubwa kwa Wakristo, makundi ya kikabila na baadhi ya dini katika Ukanda huu; mambo
yanayohitaji jibu makini kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kuna haja ya kusitisha vita,
kujenga amani na utulivu; kuganga na kuponya madonda miongoni mwa watu walioathirika
vibaya, ili kweli amani iweze kutawala tena na hivyo kuondokana na vita pamoja na
madhulumu ya kidini.
Uwepo wa Wakristo huko Mashariki ya Kati ni sehemu ya
vinasaba na utajiri wake. Ni wajibu wa viongozi wa kidini, kisiasa, kijamii na wasomi
hasa kutoka katika dini ya Kiislam, kulaani vikali misimamo mikali ya kidini inayosababisha
vita na madhulumu; mambo ambayo Baba Mtakatifu anasema, yanajionesha pia sehemu mbali
mbali za dunia.
Baba Mtakatifu akizungumzia Bara la Afrika, anasema kwamba,
kuna nchi kadhaa ambazo kwa sasa zinaendelea na vita kuanzia Nigeria ambako kuna mauaji
ya kikatili ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na utekaji nyara; biashara haramu ya
binadamu kwa kuwafanya wavulana na wasichana kuwa kama biadhaa. Vita bado inaendelea
huko Libya, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati hata watu wenye mapenzi mema wanaotaka
kujenga misingi ya amani wanatishiwa maisha kutokana na uchoyo pamoja na ubinafsi.
Baba
Mtakatifu anasema, hali si shwari sana huko Sudan, Pembe ya Afrika na DRC ambako kuna
idadi kubwa ya watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na vita. Baba Mtakatifu
anawataka wahusika kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani kwa kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Kuna baadhi ya watu wanatumia
ubakaji kama silaha katika vita, jambo ambalo linadhalilisha utu na heshima ya wanawake:
kiroho na kimwili; madonda ambayo haitakuwa rahisi kufutika katika maisha yao.
Baba
Mtakatifu anaialika Jumuiya ya Kimataifa kuwahudumia kwa heshima na taadhima wagonjwa
na waathirika wa Ebola huko Liberia, Sierra Leone na Guinea, kwani hadi sasa kuna
zaidi ya watu elfu sita ambao wamepoteza maisha yao. Baba Mtakatifu anawapongeza na
kuwashukuru wafanyakazi katika sekta ya afya, watawa na watu wanaojitolea kuwaganga
na kuwatibu wagonjwa wa Ebola na kwamba, ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha
kwamba inatoa huduma makini kwa wagonjwa wa Ebola pamoja na kuanzisha mikakati ya
pamoja, ili kuutokomeza ugonjwa wa Ebola kutoka katika uso wa dunia.
Baba Mtakatifu
anasiikitika kusema kwamba, bado Bahari ya Mediterania inaendelea kuwa ni kaburi kubwa
la wahamiaji na wakimbizi; wanaodhulumiwa na kunyanyaswa na wafanyabiashara wenye
uchu wa fedha. Hata Amerika, bado kuna idadi kubwa ya watoto wakimbizi na wahamiaji,
wanaohitaji tiba, uangalizi makini, ulinzi pamoja na usalama. Wote hawa wanakumbana
na pazia la chuma kwa kukataliwa, changamoto ya kubadili mwelekeo ili kuwajali, kuwapokea
na kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, ufumbuzi wa kudumu kuhusu chanzo kikuu
cha wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Baba
Mtakatifu anasema, hakuna umaskini mkubwa kama mtu kukosa fursa ya ajira, jambo linalodhalilisha
utu na heshima ya binadamu, kiasi cha kumgeuza mtu kuwa kweli ni mtumwa. Ukosefu wa
fursa za ajira miongoni mwa vijana na kazi za suluba kwa watoto ni mambo ambayo kimsingi
ni kinyume cha utu wa binadamu, kwani yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa fedha. Utamaduni
wa ubinafsi umepelekea idadi ndogo ya watoto wanaozaliwa hali ambayo inachangia pia
uwepo wa familia tenge; mambo yanayoathiri tunu msingi za maisha ya kifamilia na jamii
katika ujumla wake.
Baba Mtakatifu akizungumzia Nchi ya Italia anasema, myumbo
wa uchumi kimataifa umepelekea wananchi wengi kukosa imani kwa Serikali yao na matokeo
yake kuna kinzani nyingi za kijamii zinazoendelea kuibuka; kiasi cha kuwafanya watu
wengi kuishi katika mazingira magumu. Baba Mtakatifu anawaalika kwa namna ya pekee,
viongozi wa Serikali ya Italia kuondokana na hali ya kukosa uhakika katika masuala
kijamii, kisiasa na kiuchumi; mambo ambayo yanayoweza kuitumbukiza nchi katika kinzani
badala ya kujielekeza katika mshikamano, amani na utulivu kwa kuendelea kuwa na matumaini
kwa kesho iliyobora zaidi, hasa miongoni mwa vijana.
Baba Mtakatifu katika
hotuba yake amegusia hija yake ya kitume Barani Asia ambako anatembelea Sri Lanka
na Ufilippini, tukio ambalo ni ushuhuda wa Kanisa linaloguswa na kujali maisha ya
wananchi wa Bara la Asia. Ni matumaini yake kwamba, Korea ya Kaskazini na Kusini,
zitaweza tena kuanza mchakato wa majadiliano, kwa kutambua kwamba, hizi ni nchi pacha!
Baba
Mtakatifu anasema, licha ya hali ngumu inayojionesha sehemu mbali mbali za dunia,
lakini matunda ya amani yameanza kuonekana huko Albania ambako madonda ya chuki na
uhasama yameanza kuponyeka na watu wa dini na madhehebu mbali mbali wanaishi kwa amani
na utulivu. Haya ni matunda ya majadiliano yanayojikita katika imani kwa Mwenyezi
Mungu na kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi na kwamba, vita ni matokeo ya uelewa
potofu wa dini. Majadiliano ya kidini na kiekumene yanamlenga binadamu na maendeleo
yake; haya ndiyo yanayoendelea huko Uturuki na Yordan na kwamba, anatumainia kuwa
Lebanon itaweza kupata ufumbuzi wa kudumu wa matatizo na changamoto za kisiasa.
Baba
Mtakatifu anapongeza mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba,
ambayo ni kwa ajili ya mafao ya wananchi wa pande hizi mbili. Anaipongeza pia Serikali
ya Marekani kwa kuamua kufunga Gereza kuu la Guantanamo. Anaipongeza pia Serikali
ya Burkina Faso inayoendelea kujielekeza katika ushirikiano na maendeleo na maridhiano
yaliyofikiwa nchini Ufilippini, ili kukata mzizi wa chuki na uhasama nchini humo.
Anaendelea kuwatia shime wote wanaojitaabisha kwa ajili ya kutafuta amani nchini Colombia,
maridhiano huko Venezuela na mapatano kati ya Iran na Nchi tano zinazotumia nguvu
za kinyuklia kwa ajili ya matumizi ya amani.
Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba
yake kwa kukumbushia kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka
sabini tangu Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa kutokana na majivu ya Vita kuu ya Pili
ya Dunia na wakati huo, Mwenyeheri Paulo VI alisikika akikemea uwepo wa vita tena
duniani. Baba Mtakatifu Francisko anaangalia kwa matumaini utekelezaji wa Malengo
ya Maendeleo baada ya mwaka 2015, kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika masuala ya
tabianchi, kwani hapa ni chimbuko la amani ya kweli, toba na wongofu wa ndani!
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.