Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji Barani Asia kuanzia
tarehe 12 hadi tarehe 19 Januari 2015 kwa kutembelea Sri Lanka na Ufilippini.
Baba Mtakatifu
ataondoka mjini Roma Jumatatu tarehe 19 Januari 2015 majira ya saa jioni 12:50 kwa
saa za Ulaya na kuwasili kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Colombo nchini Sri
Lanka, majira ya saa 3: 00 Asubuhi. Hapo Baba Mtakatifu atapokelewa na kukaribishwa
na viongozi wa Serikali na Kanisa.
Saa 7:15 mchana, Baba Mtakatifu anatarajiwa
kukutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Sri Lanka, katika Makao makuu
ya Jimbo kuu la Colombo. Jioni majira ya saa 11:00, Baba Mtakatifu atamtembelea Rais
wa Sri Lanka Ikulu na baadaye saa 12:15 atakutana na kuzungumza na viongozi wakuu
wa dini.
Baba Mtakatifu ataianza siku ya Jumatano tarehe 14 Januari 2015 kwa
kumtangaza Mwenyeheri Giuseppe Vas kuwa Mtakatifu, katika Ibada ya Misa takatifu itakayoanza
saa 2:30 kwenye Bonde la “Green Colombo”. Baadaye, Baba Mtakatifu atasafiri kwa njia
ya Elkopta hadi kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu yaliko Madhu,
ili kusali na kutafakari kidogo kuhusu matendo makuu ya Mungu.
Tarehe 15 Asubuhi
kabla ya kuondoka nchini Sri Lanka, Baba Mtakatifu Francisko atatembelea Kikanisa
kilichowekwa wakfu kwa heshima ya Bikira Maria wa Lanka, kilichoko mjini Bolawalama.
Baada ya hapo ataelekea Uwanja wa ndege wa Colombo, tayari kuanza safari kuelekea
Manila, Ufilippini, na kuwasili majira ya saa 9: 00 na jioni saa 11: 45 atakaribishwa
rasmi kitaifa.
Ijumaa tarehe 16 Januari 2015, majira ya saa 3:15 asubuhi Baba
Mtakatifu atatembelea Ikulu na kukaribishwa rasmi na Rais wa Ufilippini baadaye atazungumza
na viongozi wa Serikali na Wanadiplomasia nchini Ufilippini. Baadaye saa 5: 15 asubuhi,
Baba Mtakatifu ataelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili
na hapo ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Familia ya Mungu nchini Ufilippini
na jioni atakutana na Familia katika Uwanja wa Mall, ulioko Jijini, Manila.
Jumamosi
tarehe 17 Januari 2015, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
huko Tacloban, karibu na Kiwanja cha Ndege, Ibada itakayoanza saa 2: 15 na baadaye
mchana, Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana na baadhi ya wahanga wa tufani ya
Yolanda, tukio litakalofanyika kwenye Makao makuu ya Jimbo Katoliki Palo. Jioni, atabariki
na kuzindua Kituo cha Maskini cha Papa Francisko na baadaye atazungumza na Wakleri,
Watawa, Waseminari na Familia za wahanga wa tufani ya Yolanda, baadaye jioni atarejea
kwa ndege Manila.
Jumapili tarehe 18 Januari, 2015 asubuhi, Baba Mtakatifu
atakutana na kuzungumza na viongozi wa dini nchini Ufilippini; baadaye atakutana na
vijana kutoka Ufilippini na jioni atadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja
wa Riz.
Jumatatu tarehe 19 Januari, 2015 Baba Mtakatifu atakuwa anahitimisha
hija yake ya kichungaji Barani Asia na ataagwa na baadaye kuanza safari ndefu ya kurejea
tena mjini Vatican anakotarajiwa kuwasili majira ya saa 11: 45 jioni, kwenye Uwanja
wa ndege wa Ciampino. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega
kukujuza yale yatakayokuwa yanajiri katika hija hii ya kichungaji, ukiwa na haraka
zako chungulia kwenye mtandao wetu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.