Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya
Mashariki anasema, historia ya Mashariki ya Kati, itakuwa na walakini mkubwa, ikiwa
kama Ukristo utafutika huko kwa sababu ya madhulumu, chuki, uhasama na vita vinavyoendelea
huko Syria na Iraq. Ukristo ni sehemu ya utajiri na vinasaba vya historia na maisha
ya watu wa Mashariki ya Kati.
Licha ya
magumu na machungu yanayoendelea kujitokeza huko Mashariki ya Kati, waamini na watu
wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani,
kwani Yesu Kristo ndiye chemchemi ya tumaini katika maisha yao yote! Baba Mtakatifu
ameendelea kuwatia moyo wa imani na matumaini Wakristo wanaoishi huko Mashariki ya
Kati kwa kuwakumbuka daima katika sala na sadaka yake, pia kama alivyofanya hivi karibuni
alipowaandikia barua Wakristo wa Mashariki ya Kati, tarehe 21 Desemba 2014.
Kanisa
linatekeleza dhamana na wajibu wake, lakini pia, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujifunga
kibwebwe zaidi, ili kweli haki, amani na umoja viweze kupatikana tena huko Mashariki
ya Kati, kwani kuna umati mkubwa sana wa watu wanateseka kutokana na vita, dhuluma
na nyanyaso za kidini.
Hatima ya wakimbizi na wahamiaji ni kati ya changamoto
kubwa zinazofanyiwa kazi na Kanisa huko Mashariki ya Kati, kwa kuitaka Jumuiya ya
Kimataifa kuhakikisha kwamba, haki ya watu kuhama kutoka sehemu moja kwenda sehemu
nyingine ili kusalimisha maisha yao, inaheshimiwa. Pale inapowezekana, wananchi wapewe
nafasi ya kurudi tena katika nchi zao za asili ili kuendelea na maisha kama kawaida.
Baraza
la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema Kardinali Sandri, linaendelea
kutoa msaada wa hali na mali kwa Wakleri, ili kuweza kuwahudumia watu wanaohitaji
msaada wa dharura, pamoja na kuendelea kuhimiza umuhimu wa kulinda na kudumisha uhuru
wa kidini, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kuwatia moyo kwa
njia ya unyenyekevu, ubaba na moyo wa udugu; jambo ambalo linawapa faraja watu wengi
zaidi katika shida na mahangaiko yao.
Vatican kwa kutumia njia ya kidiplomasia
katika vikao mbali mbali ya kimataifa, limependa kuchangia kwa moyo mkuu upatikanaji
wa suluhu ya kudumu huko Mashariki ya Kati, kwa kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kushiriki
kikamilifu, kwa kutambua mateso na mahangaiko ya watu huko Mashariki ya Kati. Matunda
ya mchango huu yanaanza kuonekana kwa baadhi ya nchi kuonesha mshikamano wake wa dhati
na watu wanaoteseka huko Mashariki ya kati pamoja na kuendelea kutoa hifadhi kwa wahamiaji
na wakimbizi kutoka Syria. Lakini anasema Kardinali Sandri, watu wanataka kuishi kwa
amani na utulivu katika nchi zao!
Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akilaani
vita, nyanyaso na madhulumu dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati na upande wa
pili wa shilingi anakazia umuhimu wa majadiliano ya kidini katika ukweli, uwazi na
mafao ya wengi; utu na heshima ya binadamu; mambo msingi yanayopaswa kusaidia mchakato
wa ujenzi wa umoja, udugu na mshikamano wa dhati.
Vijana wanapaswa kufundwa
ili kuheshimu zawadi ya maisha na utu wa binadamu. Ni wajibu wa viongozi wa dini kukemea
na kulaani vikali mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayofanywa kwa misingi ya misimamo
mikali ya kiimani, ili kweli uhuru wa kuabudu, uweze kuheshimiwa na wengi. Ni jambo
ambalo haliwezi kukubalika kuona kwamba, kuna watu wanaotumia dini kwa ajili ya mafao
binafsi. Misimamo mikali ya kidini na vitendo vya kigaidi ni mambo yanayotishia amani,
usalama na mfungamano wa kimataifa.
Kardinali Leonardo Sandri anakiri kwamba,
diplomasia ya Vatican inafanya kazi zake kwa taratibu bila ya kukata tamaa, kama ilivyokuwa
kwa Cuba na Marekani katika kipindi cha mika 53, wakipimana nguvu, lakini hatimaye,
Serikali hizi mbili zimeanzisha mchakato wa ushirikiano wa kidiplomasia. Kanisa Katoliki
huko Mashariki ya Kati linapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene,
ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa.
Kardinali
Sandri anasema, Mwaka wa Watawa Duniani kama ulivyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko,
ni fursa makini kwa Baraza lake kuendelea kuwafunda watawa wa Mashirika ya Kitawa
na Kazi za Kitume, ili kujisadaka zaidi kwa watu wanaoteseka huko Mashariki ya Kati,
huku wakiwatangazia Injili ya Furaha, Upendo na Matumaini yanayobubujika kutoka kwa
Kristo na Kanisa lake. Watawa watakuwa na nafasi ya kufanya mafungo, semina na makongamano
kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.
Watawa watambue kwamba,
wao ni sehemu ya Injili iliyo wazi, inayosomwa na wengi kwa njia ya ushuhuda wa maisha
na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwaka 2015 ni kilele
cha Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 25 tangu kuchapishwa kwa Sheria za Makanisa ya
Mashariki, kazi kubwa iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume
wake, kama sehemu ya mchakato unaopania kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa. Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.