Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani kuanzia tarehe 25 hadi tarehe 31 Januari 2015
litaadhimisha Juma la shule Katoliki Marekani, linaloongozwa na kauli mbiu "Shule
Katoliki: Jumuiya ya imani, maarifa na huduma".
Askofu George Joseph Lucas,
Mwenyekiti wa Tume ya Elimu Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani anasema, elimu ni
sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji, unaolihamasisha
Kanisa kujikita katika kuwafunda watu tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili,
ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake!
Baraza la Maaskofu
Katoliki Marekani linabainisha kwamba, shule za Kikatoliki ni mahali muafaka pa majiundo
endelevu ya kiimani katika maisha ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Hapa
ni chimbuko la miito mitakatifu ya maisha ya ndoa, upadre na utawa, kwa hakika ni
sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa, unaowashirikisha watu mbali mbali
katika utekelezaji wake.
Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 99% ya wanafunzi
wanaopata masomo yao kutoka katika shule za Kikatoliki wanahitimu masomo yao kwa ubora
na viwango vya hali ya juu kabisa. Asilimia 87% ya wanafunzi wanaohitimu masomo yao
katika sekondari zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki wanaendelea na masomo
yao katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ndani na nje ya Marekani.
Kanisa
Katoliki nchini Marekani lina jumla ya shule 6, 600 zinazowahudumia wanafunzi millioni
2.1 kwenye majiji, miji na vijiji nchini Marekani. Wanafunzi wanapewa elimu makini
itakayowasaidia kupambana na changamoto za maisha pamoja na kuwajengea ujuzi na maarifa
na ufanisi kazini. Wachunguzi wa masuala ya elimu nchini Marekani wanasema, kwa hakika
shule za Kanisa Katoliki zinatoa elimu makini kwa wanafunzi na wazazi wengi wanapenda
kuwapeleka watoto wao huko, ili waweze kufundwa si tu kiakili, bali kiutu na kimaadili
pia!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.