2015-01-10 12:25:52

Kilio cha damu!


Askofu mkuu Mario Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la haki na amani anasema, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2015 umegusa utumwa unaogusa utu, heshima na uhuru wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utumwa mamboleo una madhara makubwa katika umoja, mshikamano na mfungamano wa kijamii, kwa kushindwa kutambua utu wa mtu na matokeo yake mtu anageuzwa kuwa kama bidhaa inayouzwa sokoni.

Hapa kuna ibuka makundi ya baadhi ya watu wanaoendelea kujitajirisha kwa kunyanyasa utu na heshima ya jirani zao. Ili kufanikisha mapambano dhidi ya utumwa mamboleo, licha ya kuimarisha utawala wa sheria, kuna haja anasema Askofu mkuu Mario Toso, kutoa msaada kwa wahanga wa vitendo vya utumwa mamboleo na biashara haramu ya binadamu; Pili ni kuwasaidia kutambua utu na heshima yao kama binadamu, kwa kuwasaidia kisaikolojia pamoja na kuendelea kuwafunda na tatu, ni kuwashirikisha tena katika mikakati na maisha ya kijamii.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2015 amegusia matatizo nyeti yanayopaswa kushughulikiwa na sheria za kitaifa na kimataifa: yaani: wakimbizi na wahamiaji; ajira, mchakato wa kuasili kwa watoto kimataifa; ugawaji wa maeneo ya vitega uchumi pamoja na manunuzi ya bidhaa zinazotengenezwa kutokana na dhuluma na unyonyaji wa wafanyakazi.

Yote haya ni madonda makubwa yanayomwandama mwanadamu na kweli yanaweza kupata ufumbuzi na tiba kamili katika mchakato wa kijamii ambao kwa bahati mbaya unaendelea kugubikwa na ubinafsi usiotambua wala kuthamini umoja, udugu na mshikamano, jambo linalopewa kipaumbele cha kwanza ni fedha na wala si utu na heshima ya binadamu.

Demokrasia ya kweli, nafasi ya elimu, fursa sawa za ajira, usalama katika masuala ya afya; uwezo wa mtu kupata makazi bora, chakula na ardhi ya kufanyia shughuli zake za kiuchumi na kijamii ni mambo msingi katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo ambayo kimsingi yanapata chimbuko lake katika umaskini wa watu na tamaa ya kupata mafanikio ya haraka haraka hata kwa njia za mkato! Utawala wa sheria, utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa.

Askofu mkuu Mario Toso anasema, amani inawezekana kutawala katika mioyo ya watu, kama ambavyo pia vita inaweza kudumishwa kwa ajili ya mafao ya watu wachache katika jamii. Si ajabu kuona kwamba, kunatokea tena Vita ya tatu ya Dunia. Ukiangalia mahusiano kati ya Jumuiya ya Ulaya na Russia yanatia shaka, kiasi hata cha kuhatarisha mikakati ya kiuchumi na kisiasa.

Kuna wafanyabiashara wanaoendelea kuuza silaha za kisasa kwenye maeneo yenye vita na migogoro ya kijamii, wanachotaka wao ni fedha, kumbe kwao kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia ni sawa na “feni inayowaondolea bughuza ya maisha”. Majiundo makini katika elimu na dhamiri nyofu ni mambo msingi katika mchakato wa ujenzi wa amani ya kudumu. Matabaka ya watu katika jamii; yaani ya wale wenye nacho na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi ni hatari sana katika mshikamano wa kijamii; mambo haya yasiposhughulikiwa kikamilifu, iko siku, machafuko yatajitokeza tu!

Mwaka 2014 umekuwa ni mwaka ambao pia umeshuhudia kuibuka kwa vita kali, machafuko, kinzani na madhulumu ya kidini; mambo ambayo yanatishia uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee; umuhimu wa kudumisha utawala wa sheria, uhuru wa kuabudu, majadiliano ya kidini na kiekumene katika misingi ya ukweli na uwazi.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuandika Waraka wake wa kichungaji kuhusu mazingira yanayogusa maisha ya watu na kanuni maadili. Ni waraka ambao utagusa mambo msingi katika maisha ya mwanadamu na changamoto ya kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji, Upendo katika ukweli, Caritas in veritate anagusia kwa kina na mapana ekolojia ya binadamu, kwa kuwataka waamini na watu wenye mapenzi mema kukumbatia Injili ya Uhai kama sehemu ya mchakato wa kutunza mazingira!

Bila mwanadamu kupewa kipaumbele cha kwanza, mambo mengine yote ni ubatili mtupu anasema Askofu mkuu Mario Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la haki na amani.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.