2015-01-10 10:07:00

Boko haram sasa tatizo la kimkoa -Afrika Magharibi


Rais wa Cameroon Paul Biya, ameonya kwamba, ghasia zinazofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, sasa ni kitisho kwa nchi jirani. Hilo limeonyeshwa pia katika mkanda wa video wa kikundi hicho, uliosambazwa katika nchi jirani, ukiitaka Cameroon ifute katiba yake na izingatie sharia za Kiislamu, vinginevyo , kutakuwa na matukio mengi ya vurugu na ghasia mitaani. Katika miezi ya hivi karibuni , jeshi la Cameroon limenyamazisha fujo za kichokozi zilizokuwa zikifanywa katika eneo la mpakani kati ya Nigeria na Cameroon.

Kutokana na ghasia hizo, zaidi ya wakimbizi 3,000 waliokimbia wana jihadi hao wa Boko Haram Nigeria, wamekaribishwa nchini Chad, kama alivyoeleza Waziri Mkuu wa Chad, Kalzeubé Pahimi Deubet. Na pia kuna kundi la Wachad wapatao 500, wamerejea nchini mwao Chad, kutokana na fujo za Wanigeria Waislamu wababe.

Taarifa inaendelea kurejea matukio ya miezi ya karibuni, ambamo jeshi la Cameroon, limenyamazisha uchokozi kadhaa uliofanyika katika mpaka kati ya Nigeria na Cameroon. Ushindi ulipatikana kwa msaada wa Tume ya kimataifa ambayo inajumuisha askari wa Nigeria, Chad, Niger na Cameroon wenye kuwa na ngome yao Baga, katika kingo za Ziwa Chad upande wa Nigeria, ambako sasa Boko Haram wamepafanya kuwa eneo mkakati katika mipango yao ya mashambulizi.

Padre Patrick Tor Alumuku Mkurugenzi wa Mawasiliano Jamii katika Jimbo Kuu la Abuja, ameliambia shirika la Fides kwamba, ghasia za siku ya Jumatano ya wiki hii inayomalizika , hata makanisa kadhaa yalichomwa moto, kwa mashambulizi mfululizo, yaliyofanywa na Boko Haram katika mji wa Baga na katika vijiji vinavyozunguka, mkoani Borno, taarifa zikidai zaidi ya watu 2,000 wameathirika.

Aidha inaelezwa Boko haram walifanya shambulio hili kama kulipiza kisasi baada ya kushindwa nguvu na jeshi la kimataifa, linalolinda usalama, katika eneo Kaskazini. Mashambulizi yaliyofanywa kwa siku mbili, na kwa mujibu wa vyombo vya habari, watu zaidi ya miaka wamepoteza maisha.

Padre Alumuku anasema, Boko Haram, hasa wanapenda kufanya mashambulizi yao katika maeneo ya vijijini na siyo katika miji mikubwa, ambamo Wakristo na Waislamu wanaishi kwa amani bila kubaguana. Lakini katika maeneo ya vitongojini , Boko Haram huwa na sera ya kutenganisha Waislamu na Wakristo. Na kwamba wanaonekana kuimarishwa zaidi na wanachama wake kutoka Libya na Mali. Lengo lao ni kujenga himaya ya Kiislamu Kaskazini mwa Nigeria.








All the contents on this site are copyrighted ©.