2015-01-09 14:13:25

Sakramenti ya Ubatizo ni Mlango wa imani!


Ubatizo Mtakatifu ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika maisha ya kiroho na mlango unaomwezesha mwamini kupata Sakramenti nyingine za Kanisa. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini anaondolewa dhambi ya asili na kuzaliwa tena upya kama mtoto mpendwa wa Mungu; mtu huru na viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kimsingi, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanazaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu.

Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana, kielelezo cha mshikamano wa dhati na binadamu mdhambi, ili apate kumkomboa, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa, Jumapili ijayo tarehe 11 Januari 2015 kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Sistina kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya. Katika Ibada hii anatarajiwa kutoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto wachanga thelathini na watatu. Hawa ni watoto wa wafanyakazi wa Vatican. Kati yao kuna Mtoto wa Familia ya John Baptist Tumusiime na Mariangela Jaguraba de Jesus kutoka Radio Vatican.

Mama Kanisa anatukumbusha kwamba, watoto wanazaliwa na hali ya kibinadamu iliyoanguka na kuchafuliwa na dhambi ya asili, hata watoto wachanga wanalazima kuzaliwa upya katika Ubatizo, ili wawekwe huru na nguvu za giza na hatimaye, kuingizwa katika utawala wa uhuru wa watoto wa Mungu, ambao watu wote wameitwa. Kwamba, neema ya wokovu ni kipaji kinachotolewa bure hudhihirika kwa namna ya pekee katika ubatizo wa watoto wachanga. Ndiyo maana Mama Kanisa anahimiza ubatizo wa watoto wachanga.

Kwa wazazi ambao wanapata fursa ya kuwabatiza watoto wao wachanga wanapaswa pia kutambua kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kulea uzima ambao Mwenyezi Mungu amewaaminisha. Ubatizo ni Sakramenti ya Imani, inayopaswa kukuza na kuendelezwa, kwa msaada wa wazazi pamoja na wasimamizi wa Ubatizo. Huu ni wajibu wa Kikanisa, lakini ikumbukwe pia kwamba, Jumuiya ya waamini inawajibika barabara katika maendeleo ya maisha ya kiroho ya mbatizwa pamoja na kuendelea kutunza ile neema ya ubatizo!

Na Padre Richard A. Mjigwa,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.