2015-01-09 14:41:20

Iweni mashuhuda wenye mashiko!


Askofu msaidizi Titus Mdoe wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jumamosi, tarehe 10 Januari 2015 anatarajiwa kutoa Daraja la Ushemasi kwa Watawa wanne wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., Ibada itakayoadhimishwa kwenye Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, Mtongani, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Hawa ni Majandokasisi waliohitimu masomo yao ya falsafa na taalimungu na tarehe 9 Januari 2015 wamepokelewa rasmi kuwa ni Wamissionari wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu, katika Ibada iliyoongozwa na Mheshimiwa Padre Reginald Mrosso, C.PP.S. Mkuu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania.

Yafuatayo ni mahubiri aliyoyatoa katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwapokea Frt. Lauriano Januari Mushi, Innocent Emmanuel Miku, John Eleuteri Mlay pamoja na Emmanuel Joseph Makusaro kuwa Wamissionari. Ibada hii imefanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Nicholaus, Kunduchi, Mtongani, Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Katika barua yake kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa uliozinduliwa Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio Nov. 2014 na unaotarajiwa kufungwa rasmi tarehe 2 Feb. 2016, Siku kuu ya kutolewa Bwana Hekaluni sanjari na Siku ya Watawa Duniani, Baba Mtakatifu Francisko anaanza na maneno haya; napenda kusema neno moja kwenu na neno hilo ni furaha. Popote walipo watawa, ipo pia furaha. Wale wote waliosikia sauti ya Bwana wanaalikwa kufurahi: wimbo wetu wa katikati leo unatualika tufurahi kwa sababu sisi ni watu wa ufufuko na watu wake Mungu – Zab. 95: kwa sababu dunia imeuona wokovu wa Mungu. Ninyi vijana wapendwa mko hapa kwa sababu mnaamini katika huo ufufuko, katika huo uzima wa milele wa kimungu.

Leo tunamshukuru Mungu kwa sababu ndugu zetu hawa wamefikia hatua hii kubwa katika maisha yao ya wito na ya Kanisa kwa ujumla katika kumtumikia Mungu na watu wake. Tunasoma maneno haya katika - Zab. 100:3 – jueni kwamba Bwana ndiye Mungu, ndiye aliyetuumba, nasi tu watu wake, taifa lake na kondooo wa malisho yake. Ufahamu huu ni muhimu sana katika maisha ya mwanadamu ye yote. Ni chanzo cha wito mbalimbali katika maisha ya kawaida na katika kanisa. Ye yote yule anayetambua Mungu ni nani, atapata mwelekeo wa kimungu katika maisha yake. Asiyetambua hilo, hupoteza mwelekeo wa kimungu katika maisha yake.

Mtume Paulo katika - 1 Tim. 6:15-16 – anaandika hivi – wakati wake mwenye heri atalidokeza tokeo la yeye aliye peke yake mtawala, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana, Yeye peke yake hawezi kufa. Amekaa katika mwanga usiosogeleka. Hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na enzi ya milele ni yake. Amina. Tunaona kuwa ufalme na utawala wa kweli ni wake.

Ufahamu huu unatupelekea kutambua kuwa tumeitwa kumtumikia yeye tu na si kitu kingine cho chote kile – Mt. 4:10 – Yesu akamwambia, nenda zako shetani, kwa maana imeandikwa– umwabudu Bwana Mungu wako, ukamtumikie yeye peke yake. Na katika Kumb. 6:13 – ndiye Bwana Mungu wako utakayemwogopa, ndiye utakayemtumikia na kuapa kwa jina lake.

Somo la kwanza toka Nabii Isaya – “Injili ya Ufalme wa Mungu” - mwandishi anaandika neno hili wakati Waisraeli wamekuwa huru toka Babeli - linaelezea habari ya ukombozi. Waisraeli wanatoka katika utumwa. Wanafurahi. Nanyi pia tafakarini sana hali yenu – mjiweke huru kwa ajili ya Mungu. Yule aliyeufahamu ukombozi wa Mungu, anajiweka huru kwa ajili yake. Nanyi kuweni huru siku zote kwa ajili ya kumtumikia Mungu na mumtumikie kwa furaha siku zote za maisha yenu. Nabii Isaya– anatambua kuwa thamani ya maisha iko katika uhuru wa kimungu. Huo ndio uhuru wa kweli na wenye kuleta wokovu.

WHO IS A CONSECRATED PERSON?

He is a person who has an experience of God and especially as an Absolute. One who deeply aware of his encouter with God and having received a special gift which is divine and trinitarian. This is more than reading or hearing about God (Cf. Mk 8:27-29 – ungamo la Petro – baada ya Yesu kuwauliza – watu wasema mimi ni nani? ). And because in encoutering God he knows himself, then the experience of his weakness, fragility and suffering leads him to see God as an Absolute — God is all, man is nothing. Hence, the first task of consecrated person is to reveal the primacy of God to the world. All vocations reveal the mystery of Christ: the lay vocation reveals the face of Christ facing towards the world, the priestly vocation reveals the face of Christ facing towards the community and the consecrated vocation reveals the heart of Christ turned towards the Father. The consecrated person lives for God and only for God. The first value of our vows is to sing the primacy of God in our lives.

Waraka wa Kitume Injili ya Furaha,“Evangelii Gaudium” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Fransisko unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema – furaha ya Injili inajaza mioyo na maisha ya wale wanaokutana na Kristo. Pamoja na Yesu Kristo, furaha inazaliwa upya tena. Sura ya 4 – mwanzoni - ya waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Wakorintho – inazungumzia juu ya watumishi kwa ajili ya Kristo. Mstari wa sita – kwani Mungu aliyesema, Mwanga ung’ae kutoka gizani, ndiye yeye anayeng’aa mioyoni mwetu tupate kwa mwanga wake kuutambua utukufu wa Mungu uliopo usoni mwa Yesu Kristo. 2 Kor. 4: 6…. Mnaalikwa muwe mwanga wake Kristo. Kwa maisha yenu na ushuhuda wenu wa maisha, Kristo aendelee kuonekana duniani. Maisha haya mnayotaka kufuata yawe changamoto kwa wale wote ili wanapowaona ninyi wazidi kumpenda na kumtumikia Mungu Baba.

Katika barua kwa mwaka wa watawa – Baba Mtakatifu Francis anamtaja wazi Mtakatifu Francisko wa Assisi kama mfano wa kuigwa, yeye aliyefanya Injili iwe njia yake ya maisha, akafanya imani ikakua na akahuisha kanisa na jamii, akaifanya iwe ya kindugu zaidi, lakini daima akiongozwa na Injili na ushuhuda wa maisha yake. Nanyi yapokeeni na yatimizeni mapenzi ya Bwana kama mtakatifiu Francis. Na imani yenu ionekane katika matendo yenu. Lengo lenu liwe tu ni kutangaza habari njema kwa kila kiumbe.

Neno la Mungu katika somo la Injili leo liwaongoze na kuwatafakarisha sana - Yesu ndiye masiha aliyepakwa mafuta, ambaye kadiri ya maandiko ya manabii ‘ndiye aliyepelekwa kuwatangazia maskini habari njema na kuutangaza mwaka wa Neema – Lk. 4, 18-19, pia katika Isa. 61: 1-2 - ‘Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi, watu wote wakamkodolea macho. Naye akaanza kuwaambia, andiko hili mlilolisikia limetimia leo’.

Nanyi ingieni katika programu hii ya kimasiha ya Yesu Kristo. Yaani muwe watangazaji mahiri wa ufalme wake na kuutangaza daima mwaka wa Bwana. Ujumbe huu bado u hai hata leo. Msijihangaishe na lo lote lile lililo nje ya programu hii. Katika kumfuata Kristo – Baba Mtakatifu katika barua yake kwa Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa anaendelea kusema – kuweni na mwanga na furaha, ng’aeni furaha. Isa. 66: 10-14 – shangilia pamoja na Yerusalemu, pigeni vigelegele kwa ajili yake, enyi nyote mnaomlilia, furahini, furahini pamoja naye ninyi nyote mlioomboleza kwa ajili yake Ili mpate kunyonya na kushibishwa maziwa ya faraja yake, na kufurahishwa kwa maziwa yake matukufu.

Maana, Bwana asema hivi; nitatiririsha amani na utulivu pande zote kama mto; nao utukufu wa mataifa kama kijito kifurikacho. Nanyi mtapata kunyonya, mtabebwa kifuani, na kubembelezwa juu ya magoti yake, mfano wa mwana anayefarijiwa na mama yake, ndivyo nami nitawafariji, nanyi mtafarijiwa moyo katika Yerusalemu. Kwa kuona hayo, moyo wenu utafurahi, na mifupa yenu itasitawi mfano wa majani mabichi na mkono wa Bwana utajulikana kwa watumishi wake, nayo ghadhabu yake kwa maadui zake.

Wote watakaoshiriki karamu hii ya Bwana na mwaliko huu mtakatifu watapata uzima wa milele. Ninyi mnataka kuingia katika karamu hii. Furahini pamoja na Bwana na furaha hiyo izae matunda katika maisha yenu.

Naye Mtakatifu Gaspari anatupa changamoto nyingine katika maisha ya ufuasi. Alipoanzisha Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu alialika wafuasi wake wawe na upendo mkuu akisema ‘upendo ni kifungo kwa wamisionari wake’. Wakifungwa na upendo, Gaspari aliamini Wamisionari wake wataweza kueneza kwa maisha yao Tasaufi ya damu azizi. Tena watakuwa tayari kutoa huduma ya Neno la Mungu. Akinukuu maneno toka waraka wa Paulo kwa waefeso 1;6-8 – Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo …katika yeye ametuchagua kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu kusudi tuwe watakatifu na bila doa mbele yake katika upend.

Mtakatifu Gaspari aliamini kuwa upendo ukiwepo kazi ya Mungu itaendelezwa. Nasi tumwaminio tutapata uzima wa milele. Katika maisha yake alieneza sifa na utukufu wa neema hizi za Mungu, neema ambayo inatoka kwa mwanae mpendwa Kristo Yesu. Kutoka kwake Kristo tunaona ukombozi wetu na tuna msamaha wa dhambi. Nanyi muwe na upendo mkuu kwa Mungu Baba na Mwanae anayewajalia roho ya kutaka kumtumikia yeye kwa ulimwengu wa leo wenye changamoto nyingi za maisha.

Ninyi leo mnakuwa Wamisionari wanashirika. Mtakatifu Gaspari hakuona ibada kwa Damu azizi ya Yesu kama ibada nyingine ya kawaida, bali aliona ni kama kiini kabisa cha dini. Mtakatifu Gaspari mwenyewe anasema, ‘ni njia salama ya kufikia utakatifu binafsi na chachu ya maisha mapya ya jumuia na nguvu imara ya kazi ya kitume.

Pengine twaweza kujiuliza kama Kristo alishamwaga damu yake kwa ajili yetu sote, nafasi yangu ni ipi leo katika kuutangaza upendo huu wa Kristo? Kwa nini nihangaike kufanya mengi kama Kristo tayari ameshatukomboa? Waraka wa mtume Paulo kwa Wakolosai 1:24 unatupatia jibu “ nayatimiliza katika mwili wangu yale yaliyopungua katika mateso kwa ajili ya mwili wake yaani kanisa lake”

Nihitimishe homilia hii nikinukuu tena maneno ya Baba Mtakatifu Francis katika barua yake kwa Mwaka wa Watawa, akisema – nataka niseme neno moja kwenu, nalo ni furahini. Po pote walipo watawa na watu wa maisha ya wakfu, waseminari, wanaume na wanawake, vijana, ipo furaha, ipo daima furaha. Ni furaha ya upya, furaha ya kumfuata Kristo, furaha ambayo Roho Mtakatifu atupatia. Siyo furaha ya ulimwengu. Somo la pili la leo linatoa mwelekeo – Ebr. 13:12-15, 20-21- habari juu ya maisha mapya katika ufufuko.

Sisi tumepatanishwa na Mungu kwa njia ya kifo cha mwanawe, tumeokolewa kwa ufufuko wake. Sisi ni viumbe vipya. Ni watu wa ufufuko. Mnapoaanza maisha mapya katika shirika letu na ndani ya kanisa – jitahidini nanyi kuwa wapya katika yote – ishini maisha ya ufufuko. Maneno ya Petro Mtume yawaongoze“tuishi kama watakatifu kwa mfano wa Mungu aliyetuita katika imani”.

Tumsifu Yesu Kristo.
Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.