2015-01-08 13:29:50

Zingatieni utawala wa sheria na haki, ili kukemea maovu!


Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania Bwana George Masaju amewakumbusha watumishi wa umma katika sekta ya sheria kufanya kazi kwa ushirikiano, uzalendo, maadili, utii wa sheria ili kulinda maslahi ya taifa. Bwana Masaju, ambaye ameteuliwa na kuapishwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo, amefafanua kuwa watumishi wa umma wanapozingatia uzalendo katika utendaji wao, wanapata nguvu ya kusimama na kukemea maovu.


Bw. Masaju ameyasema hayo Jumatano, Januari 7, 2015 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria alipokwenda kubadilishana nao mawazo. “Sisi kama Wizara kwa ujumla wetu, tunapaswa kuwa mfano wa uzalendo katika taifa hili ili tunaposimama mbele ya watu, tuwe na nguvu kwa kuwa tupo safi,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Asha-Rose Migiro alimpongeza Bw. Masaju kwa heshima aliyopewa na Rais Jakaya Kikwete na kuahidi kuwa yeye na Wizara itaendelea kumpa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake. “Tunakupongeza kwa heshima kubwa uliyopewa na Mheshimiwa Rais na sisi kama wasimamizi wa sera, tutaendelea kutoa ushirikiano kwako kama tulivyofanya kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali aliyetangulia,” alisema Waziri Migiro.

Aidha, Waziri Migiro aliahidi kuongeza ushirikiano katika kuimarisha kada ya Mawakili wa Serikali pamoja na watumishi wengine ili kuongeza ufanisi katika utoaji haki. Bw. Masaju aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali tarehe 2 Januari mwaka huu na kuapishwa tarehe 5 Januari. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Aidha, Bw. Masaju amewahi kuwa Mshauri wa Sheria wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.