Mshikamano wa upendo na udugu kwa Wakristo Mashariki ya Kati!
Ujumbe wa Maaskofu Katoliki kutoka Ulaya, Marekani na Afrika ya Kusini, wanaoratibu
shughuli za misaada kwa Nchi Takatifu, (HLC2015) kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 15
Januari 2015 wanatembelea Nchi Takatifu kama kielelezo cha mshikamano umoja, upendo
na udugu kwa ajili ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, hasa kipindi hiki ambako Ukanda
huu umegeuka kuwa ni uwanja wa fujo na kinzani za kisiasa na kijamii!
Askofu
Duarte da Cunha, Katibu mkuu wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Ulaya anasema,
pengine watu wamekuwa na mazoea ya kuona mashambulizi, vita na mateso ya watu yalisimuliwa
kwenye vyombo vya habari na kusahau kwamba, mambo haya yamechangia kwa kiasi kikubwa
kwa Mashariki ya Kati, kuwekwa pembezoni mwa mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa. Maaskofu
wanapenda kuwaonesha Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema ujumbe wa amani na matumaini
yanayojikita katika ushuhuda wa maisha, kwa kuwa karibu zaidi na wale wote wanaoteseka
pamoja na maskini pamoja na kuwatia shime wafanyakazi wa Mashirika mbali mbali ya
misaada yanayosimamiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki.
Wakiwa Nchi Takatifu
wajumbe hawa watatembelea na kukutana na viongozi pamoja na Wakristo wanaoishi kwenye
Ukanda wa Ghaza, ili kuangalia huduma zinazotolewa katika shule na vituo vya afya
kwa ajili ya wananchi. Watatembelea pia mji wa Hebron na Sderot, ambayo imeharibiwa
hivi karibuni kutokana na kupigwa kwa makombora. Watatembelea pia mji wa Cremisan,
ambao kuna ukuta unaotenganisha familia za Kikristo zinazoishi katika miji ya Beit
Sahour na Beit Jala. Ujumbe huu utakapokuwa mjini Bethlehemu utatembelea na kujionea
shughuli mbali mbali zinazofanywa kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenye ulemavu na
wanaoishi kwenye mazingira hatarishi; wazee wanaotunzwa na kuhudumiwa na Kanisa. Watatembelea
na kukagua huduma zinazotolewa kwenye shule za visiwi na vipofu; nyumba ya wanawake
wajane. Wajumbe wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Maaskofu mahalia.
Taarifa
zinaonesha kwamba, Baraza kuu la Shirikisho la Makanisa Katoliki Ulaya, linatarajiwa
kufanya mkutano wake wa Mwaka kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 16 Septemba 2015. Huu
ni mkutano unaowashirikisha Maaskofu Katoliki kutoka katika Nchi 43 za Bara la Ulaya.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.