Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na wafanyakazi mbali mbali wa Vatican,
kama sehemu ya mchakato wa kutakiana kheri na baraka kwa Kipindi cha Noeli na Mwaka
Mpya 2015 amewataka wafanyakazi hawa kutumia neema na baraka ya kipindi hiki kwa ajili
ya kuganga na kutibu madonda yaliyojitokeza katika hija ya maisha yao pamoja na kujitakasa,
ili kuanza mchakato wa maisha mapya.
Baba Mtakatifu
katika hotuba yake kwa wafanyakazi wa Vatican amekazia zaidi: umuhimu wa maisha ya
kiroho, kifamilia, upendo kwa Mungu na jirani, kazi pamoja na kutibu mapungufu ya
mtu binafsi.
Hii ni nafasi murua kabisa Familia ya Mungu inapoendelea kuwasindikiza
Mababa wa Sinodi kwa sala, tafakari na mchango wao kwa ajili ya Sinodi ya Maaskofu
kuhusu Familia, itakayoadhimishwa hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe
25 Oktoba, 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “wito na utume wa Familia katika Kanisa
na Ulimwengu mamboleo”, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inapenda kukukumbusha
tena ujumbe wa Baba Mtakatifu, ili uweze kuumwilisha katika maisha yako ya kila siku!
Kwanza
kabisa Baba Mtakatifu anawataka wafanyakazi kuhakikisha kwamba, wanashughulikia kwa
ud ina uvumba maisha yao ya kiroho ambayo yanapaswa kujikita katika: Sala, Sakramenti
pamoja na tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma, Baba
Mtakatifu anasema mahusiano ya karibu na Mwenyezi Mungu ni uti wa mgongo wa maisha
na utambulisho wa kila mwamini. Ikiwa kama mwamini atatindikiwa na mambo haya, maisha
yake yako hatarini, anaweza kunyauka na hatimaye, kukosa dira na mwelekeo wa maisha.
Baba
Mtakatifu anasema, kuna haja kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kujikita zaidi
na zaidi katika maboresho ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kutoa kipaumbele
cha kwanza kwa malezi na makuzi ya watoto wao. Wazazi wahakikishe kwamba, wanatenga
muda wa kukaa pamoja na watoto wao, ili kuwajengea matumaini ya kesho iliyo bora!
Baba Mtakatifu anasema, haitoshi kuwapatia watoto fedha kibao na simu za viganjani
wakadhani kwamba, hapo wamemaliza wajibu wao!
Baba Mtakatifu anawataka waamini
kuhakikisha kwamba, wanaboresha mahusiano yao na jirani zao, ili kweli familia ziweze
kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kushuhudia na kutangaza Injili ya Familia,
kwa njia ya imani tendaji. Maisha ya wanafamilia yajikite katika imani, wema, mapendo
na matumaini; kwa kuonesha ukarimu na kusaidiana kwa hali na mali.
Pale ambapo
familia zimeonesha mtafaruku, waamini wawe na ujasiri wa kutibu madonda haya kwa njia
ya mafuta ya huruma, upendo na mshamaha kwa kutambua kwamba, kukosa na kukoseheana
ni sehemu ya ubinadamu, kusamehe na kusahau ni kuanza mchakato wa maisha ya uzima
wa milele. Waamini wajitahidi kuponya madonda waliyowatendea wengine, kwa njia ya
toba na wongofu wa ndani.
Baba Mtakatifu anasema, kazi na ajira ni kielelezo
cha ut una utumilifu wa maisha ya mwanadamu na kwamba, kazi ndilo jina lako haswaaa!Baba
Mtakatifu anawahimiza wanafamilia wanaofanya kazi, kutekeleza wajibu huu nyeti kwa
unyenyekevu mkubwa, weledi, juhudi, bidii na maarifa, daima wakionesha moyo wa shukurani
kwa Mwenyezi Mungu anayewakirimia nafasi hii.
Ni changamoto kwa wafanyakazi
kujiepusha na majungu, utovu wa nidhamu, uchu wa mali na madaraka; mambo ambayo wakati
mwingine ni sababu ya kutoweka kwa amani na utulivu kati ya jamii ya watu, kiasi cha
kuwatumbukiza watu katika majanga na maafa makubwa. Watu wajiepushe kulipiza kisasi
kwani hali hii ni kwenda kinyume kabisa cha haki ya Mungu, kwani Mwenyezi Mungu ndiye
mwenye kipimo na hakimu mwenye haki. Watu waondokane na uvivu, jamvi la shetani; kiburi
na majivuno. Wafanyakazi waoneshe ukomavu kazini kwa kukuza na kudumisha maadili badala
ya kutaka kuwapaka wenzao kwa matope, mambo ambayo ni hatari kwa ustawi na maendeleo
ya jamii.
Jamii ijifunze kuwahudumia maskini, wanyonge na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii; hawa ni watoto ambao bado hawajazaliwa, wazee, wagonjwa, wageni,
wakimbizi na wahamiaji. Kipindi cha Noeli, kiwe ni kielelezo cha imani, upendo na
mshikamano wa dhati; kipindi cha kushirikishana furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo
na Kanisa lake; kwa kutambua kwamba, Mwana wa Mungu yuko pamoja na watu wake. Yesu
Kristo, Mwana wa Mungu aliyejifanya maskini kwa ajili ya maskini, anaendelea kuwashangaza
wanadamu kwa kujifunua kwa watoto wadogo na maskini na kwamba, Kristo Yesu, amekuja
ili kuhudumia na kujisadaka kwa ajili ya wokovu wa wengi.
Noeli ni kipindi
cha Amani, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; inayopaswa kulindwa, kudumishwa
na kuendelezwa. Baba Mtakatifu anathubutu kuomba msamaha kutokana na mapungufu yake
ya kibinadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuombana msamaha, ili kuanza hija
ya maisha mapya katika haki, wema na utakatifu wa maisha!
Na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican