Katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2015, Kardinali
Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliwasilisha salam na matashi mema kutoka
kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya ufunguzi wa jengo linalotumika kwa ajili
ya majiundo ya majandokasisi kutoka Marekani wanaosoma katika taasisi na vyuo mbali
mbali vya kipapa mjini Roma.
Kuna uhusiano mkubwa kati ya majiundo na Khalifa
wa Mtakatifu Petro, kwani wote wanaofunda na kufundwa chuoni hapo wanahamasishwa kuwa
ni mashahidi wa Fumbo la Pasaka, sanjari na kujitahidi kuwa ni wachungaji wema na
watakatifu. Ni mwaliko wa kuendelea kusali kwa ajili ya Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi
wake wa karibu, ili aweze kuliongoza Kanisa la Kristo, daima akiongozwa na mwanga
angavu ambao ni Kristo mwenyewe!
Kama ilivyokuwa kwa Mamajusi, walipofika wakagundua
kwamba, kwa hakika Yesu ni mwanga wa wema, ukweli na uzuri, jambo ambalo waliwashirikisha
wengine mara baada ya kufanya hija yao mjini Bethlehemu na hivyo kuvuruga njama za
Mfalme Herode za kutaka kumwangamiza Mtoto Yesu wakati ule. Waamini waendelee kumtolea
Yesu zawadi ya: dhahabu, uvumba na manemane, bila kusahau shida na magumu wanayokumbana
nayo katika maisha, kwani Yesu kwa hakika ni mwanga angavu.
Kardinali Pietro
Parolin anawataka majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanajitoa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye Mkombozi wa ulimwengu.
Leo hii kuna watu wengi ambao wanaendelea kulia na kuomboleza kutokana na vita, dhuluma,
nyanyaso na kinzani zinazowaelemea walimwengu. Bado kuna mamillioni ya watu wanakabiliwa
na umaskini wa hali na kipato; njaa na maradhi.
Haya ni mambo ambayo yanahitaji
kushughulikiwa kwa njia ya sala na mshikamano wa udugu na upendo kati ya watu; kwa
kuendelea kutoa nafasi kwa Yesu Kristo Mkombozi wa dunia, ili aweze kuwaletea mageuzi
katika maisha yao, mintarafu mwanga wa haki, amani na mshikamano.
Kardinali
Parolin anawapongeza vijana ambao kwa hiyari yao wenyewe wametambua kwamba, wanaitwa
na Mwenyezi Mungu ili kushiriki katika Ukuhani wa Kristo kwa njia ya Daraja Takatifu
la Upadre. Seminari ni mahali ambapo Mama Kanisa anapatumia kwa ajili ya majiundo
makini ya mihimili ya Uinjilishaji: kiroho, kimwili, kiutu na kimaadili.
Majandokasisi
wanapohitimisha majiundo yao makini, wanapaswa kuwa kweli ni vyombo vya ujenzi wa
Ufalme wa Mungu, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha. Huu ndio utume
unaopaswa kufanyiwa kazi na wale wote ambao wamepewa dhamana ya Kuinjilisha. Mwishoni,
Kardinali ameyaweka majengo mapya chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria Mama
wa Mungu, ili aweze kuwasimamia na kuwaongoza kwa kufuata mfano wa Mwanaye Mpendwa
Yesu Kristo.
Waamini wote wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi,
kwa kuonesha uaminifu, mapendo, imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Miamba ya
Injili, iliyomwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, ili kweli Kristo nyota
angavu aendelee kung'ara katika maisha ya watu na vipaumbele vyao! Tukio hili limehudhuriwa
na viongozi kadhaa kutoka ndani na nje ya Vatican, wafadhili na waamini.
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.