2015-01-07 09:28:46

"Walimwengu ni watata"!


Askofu mkuu mstaafu Alessandro Plotti wa Jimbo kuu la Pisa, Italia katika maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana, tarehe 6 Januari 2015, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane, lililoko mjini Roma, ametoa Darala la Ushemasi kwa Wamissionari wawili wa Mapendo, maarufu kama Warosimini. RealAudioMP3

Mashemasi hawa ni Aristid Shayo kutoka Tanzania na Shemasi Justus Okibo kutoka Kenya. Katika Ibada hii ya Misa Takatifu, Askofu mkuu mstaafu Plotti amefanya pia kumbu kumbu ya miaka 34 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu.

Katika mahubiri yake Askofu mkuu mstaafu Plotti amekazia umuhimu wa Umissionari unaomwilishwa katika huduma ya mapendo; huduma kwa Neno la Mungu, linalotamadunishwa katika uhalisia wa maisha ya watu sanjari na kujikita kwa njia ya sala na tafakari kuitafuta ile nyota angavu, yaani Yesu Kristo katika kuishirikisha Familia ya Mungu mwanga wa upendo na huruma ya Mungu.

Baadhi ya waamini ndani ya Kanisa Katoliki kwa kuwekewa mikono na Askofu wanapewa Daraja la Ushemasi, wakiwa na dhamana na utume wa kuhudumia Altareni, Kuhubiri Neno la Mungu, kuwagawia waamini Ekaristi Takatifu, kuhudumia wakati wa mazishi na kusaidia kuendesha Ibada mbali mbali kadiri ya Daraja la Ushemasi pamoja na kutambua kwamba, Mashemasi ni wahudumu wakuu wa matendo ya huruma yanayofanywa na Mama Kanisa kwa waja wake. Mashemasi wanapaswa kutambua kwamba, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni hazina na utajiri mkubwa wa Mama Kanisa katika maisha na utume wake.

Askofu mkuu Plotti katika utangulizi wa Ibada ya Misa anasema, Siku kuu ya Epifania ni tukio linalomwonesha Yesu, Mwanga wa Mungu akijifunua kwa Mataifa na utukufu wake ukaonekana mjini Bethlehemu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumfungulia malango ya mioyo yao, ili Kristo Mwanga wa mataifa apate kuingia na kuwaangazia katika mapito, maisha na historia yao. Mashemasi wapya waongozwe na mwanga huu kwa kuendelea kuchota utajiri kutoka kwa Mwenyeheri Rosmini, Mwanzilishi wa Shirika la Mapendo ili kuwahudumia Watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu!

Askofu Plotti katika mahubiri yake, amewataka Mashemasi wapya, kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, maskini ni hazina kubwa kwa Mama Kanisa na kwamba, Yesu hakuzaliwa kwenye majumba ya Kifalme, bali alizaliwa katika pango ya kulishia wanyama, yaani alizaliwa katika hali ya umaskini, kule mjini Bethlehemu, lakini hata hivyo bado aliendelea kuwa na mvuto pamoja na mashiko kwa wachungaji waliokuwa wanalisha wanyama wao kondeni, kama ilivyokuwa pia kwa Mamajusi kutoka Mashariki ya Mbali.

Ujumbe wa Habari Njema, unajikita katika maneno yanayoleta changamoto na bashasha katika maisha ya waamini! Simama, tazama, angaza, amezaliwa Mkombozi wa dunia, nyota angavu. Hapa swali la msingi ambalo mwamini anapaswa kujiuliza ni kama ikiwa yuko tayari kuupokea mwanga unaokuja! Je, ametoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Kristo katika maisha. Wakristo wanapaswa kuwa macho na makini, ili kushinda kishawishi cha kukata tamaa au kukatishana tamaa, vikwazo katika mchakato wa kutaka kumwona Mtoto Yesu.

Askofu mkuu mstaafu amewakumbusha Waamini kwamba, hija iliyofanywa na Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali ni sawa na hija ya maisha ya kiroho inayofanywa na kila mwamini; hija inayojikita katika uaminifu, udumifu, daima wakiwa na taa zinazowaka na akiba ya mafuta, ili kufanikisha mchakato wa kumtafuta Mtoto Yesu, Fumbo lililokuwa limefichika tangu milele, lakini watu wa nyakati hizi wamepata bahati ya kufunuliwa Fumbo hili. Changamoto kwa waamini kuwa macho, kuendelea kusali na kumpatia Mungu kipaumbele cha kwanza, ili aweze kuwaongoza katika hija ya maisha ya hapa duniani sanjari na kuandika historia katika maisha yao.

Askofu mkuu mstaafu Plotti amewataka Mashemasi na waamini katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, daima Mwenyezi Mungu anapowatembelea akute malango ya maisha yao yakiwa wazi, kwa kuwamegea wengine furaha inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; sanjari na kujenga umoja na mshikamano katika kuwahudumia watu wa Mungu.

Epifania ni Siku kuu ya Kristo anayejionesha miongoni mwa mataifa, ni siku kuu ya Kanisa la Kiulimwengu, lakini kwa bahati mbaya hata leo hii bado kuna akina Herode wanaotaka kujihudumia wenyewe badala ya kuhudumia Kanisa; huu ni uwili ambao unajitokeza hata ndani ya Kanisa kutokana na uwepo wa dhambi miongoni mwa watoto wa Kanisa wanaochuchumilia utakatifu wa maisha. Mashemasi wanachangamotishwa kuendeleza huduma katika mapendo na kwamba, ushemasi ni huduma ya kudumu hata baada ya kupokea Daraja Takatifu la Upadre. Wakleri wanapaswa kuendelea kutoa huduma ya huruma, mapendo na msamaha kwa ajili ya Watoto wa Mungu.

Askofu mkuu Plotti amewataka Mashemasi wapya kuwa ni Wamissionari na wahudumu wa Neno kwa kulimwilisha na kulitamadunisha katika maisha na mazingira ya watu, ili watu waweze kuona mwanga na kutoka gizani, ili kuonja upya wa maisha unaobubujika kutoka katika Neno la Mungu. Watu wana kiu kubwa ya kutaka kusikia Neno la Mungu.

Yesu Kristo ndiye Mkombozi wa kweli aliyekuja kumwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumstahilishia binadamu kuitwa mwana mpendwa wa Mungu. Vita na kinzani haviwezi kumkomboa mwanadamu katika shida na mahangaiko yake, bali vitaendelea kusababisha majanga kwa watu na mali zao. Yesu Kristo ndiye mwanga unaokoa na kuwawezesha watu kuwa ni Wamissionari, ili kuwatangazia jirani zao Habari Njema ya Wokovu, kwa njia ya karama ya Shirika la Mapendo, ili kweli watu waweze kuona na kuonja mabadiliko yaliyoletwa na Yesu Kristo.

Askofu mkuu mstaafu Alessandro Plotti anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea: amani, upendo, mshikamano; furaha ya kweli inayopata chimbuko lake kwa Kristo; ili hatimaye, wao pia waweze kuwashirikisha wengine furaha hii.

Askofu mkuu mstaafu anakiri kwamba, Upadre ni daraja linalobaliana na changamoto, matatizo na magumu mbali mbali, lakini Wakleri wanapaswa kujifunza kutoka kwa Kristo ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo na kwamba, mzigo wake ni mwepesi. Ile hamu na kiu ya watu kutaka kukutana na Yesu ipate jibu makini kwa kukutana na wahudumu wa Injili, ambao ni wakweli, wanyofu na watoto wapendwa wa Mungu.

Askofu mkuu mstaafu pamoja na kuwa na umri mkubwa, umati wa Familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki, Italia na nje ya Italia, wamemkubali kwa "kushusha ndondo za uhakika", kielelezo kwamba, "amekula nchumvi nyingi" katika maisha na huduma ya Kipadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.