2015-01-07 08:32:21

Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana!


Mpendwa mwana wa Mungu, tuko tena pamoja katika ile habari ya furaha ndiyo kushirikishana mapendo ya Mungu kwa njia ya Neno lake. Leo ndipo tunahitimisha kipindi cha Noeli kwa Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana na tunaanza kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa. Kumbe leo pia ni Dominika ya kwanza ya kipindi cha Mwaka wa Kanisa. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatupeni habari juu ya mtumishi wa Mungu ambaye anapokea Roho wa Mungu na kazi yake itakuwa kuwahukumu mataifa kwa haki. Ni nuru na mwanga kwa mataifa. Sifa yake nyingine ni mtulivu na mnyenyekevu na hakati tamaa kwa maana mkono wa Mungu uko juu yake. Mtumishi huyu anakabidhiwa Roho wa Mungu kwa sababu ya kazi ya kimungu ambayo ni kujenga amani na kuunganisha vilivyovunjika.

Kadiri ya Injili ya Luka 4: 18-19 mtumishi huyu ni Yesu Kristu. Anakuja kwa ajili ya kutangaza mwaka wa Bwana ambapo wafungwa na vipofu wataondolewa katika shida zao. Kristu amekwisha fika kwetu kazi yetu sasa ni kupokea ujumbe wake. Namna ya kupokea ujumbe ni kuitika kwanza ule mpango wa Yohane Mbatizaji na Isaya wa kutengeneza njia ya Bwana, kuondoa visiki na mabonde. Tunapaswa kufanya hivyo kwa sababu tunasikia kuwa huyu ajaye hatumii nguvu bali upendo na hivi anahitaji ushirikiano. Kwa jinsi hiyo ni kuweka ubatizo wetu katika matendo.

Mtume Petro akielewa vema nia na mpango wa Mungu anasimama kama tusomavyo katika kitabu cha Matendo ya Mitume na kusema hakika Mungu hana upendeleo cha msingi ni kufanya bidii ya kumcha Bwana. Oneni jinsi ambavyo neno la Mungu linavyopiga kasi, anasema Mtume Petro, si tu kwa Wayahudi bali kwa ajili ya wote. Lakini kwa nini fundisho hili?, Ni kwa sababu kulikuwa na upinzani dhidi ya ubatizo wa wapagani. Kumbe Mtume Petro anasema, Kristu mpakwa mafuta wa Bwana amepiga kazi ya kichungaji baada ya kutiwa mafuta na Roho wa Bwana bila kubagua. Ni fundisho kwetu kujiimarisha katika utume na kuimarisha umoja kamili na watu wote milki ya Mungu. Toeni bure kwa maana mmepewa bure.

Katik Injili ya Marko tunapata fundisho la unyenyekevu wa Yohane Mbatizaji na unyenyekevu wa Kristu. Yohane Mbatizaji anakiri udogo wake ambao ni wa chini kabisa. Maana hata kushindwa kushika gidamu ya viatu vya Yesu Kristo. Anatufundisha moja kwa moja kuwa safari ya kumpenda Mungu yatudai kushuka mpaka sakafuni. Mkombozi mwenyewe pia ni kielelezo kingine cha hali ya juu kuhusu unyenyekevu. Anajishusha kwanza na anakuwa mtu, kana kwamba hiyo haitoshi anaamua kubatizwa wakati hana doa la dhambi. Anatufundisha kujishusha kukaa pamoja na wadhambi, maana tunabatizwa ili kuokolewa katika uvuli wa dhambi ya asili kwanza na kuweza kupokea neema za Mungu.

Bwana anapobatizwa yafaa tuangalie mambo yaliyo tokea. Jambo la kwanza ni kupasuka kwa mbingu, ambalo linatupa habari ileile ya Nabii Isaya katika Dominika za majilio. Nabii anauliza mbona umetufanya tukose kukutii? Mbona umetuacha hata tukasahau kukucha wewe Bwana? Is. 63:15-19. Isaya anauliza haya maswali kwa maana ni kama hakuna upatano kati ya mbingu na nchi. Sasa tendo la kupasuka kwa mbingu ni ishara ya mapatano kati ya mbingu na nchi na mpatanishi ni Kristu katika uwezo wa Utatu Mtakatifu.

Jambo la pili ni alama ya njiwa, alama hii yatukumbusha kile kilichotokea wakati wa mafuriko ya Nuhu. Wakati huo mbingu na dunia vilifungwa na njiwa alipotokea akiwa na tawi la mzeituni ilimaanisha kuwa amani imerejeshwa. Ndiyo kusema kwa ishara ya njiwa kuna amani, ni Roho Mtakatifu afanyaye kazi katika Yesu Kristu chanzo cha amani. Mpendwa jambo la pili kuhusu njiwa katika agano la kale alimaanisha nguvu waliyopewa Manabii na hivi Kristu waziwazi ana nguvu hiyo kwa ajili ya kutenda kazi ya Mungu.

Sauti kutoka juu yamaanisha kuwa Kristu ni wa juu na pia Mungu anaongea na watu wake kwa njia yake aliye mwanae mpenzi. Mpendwa msikilizaji yafaa kukumbuka pia jambo jingine nalo ni lile la Joshua anapowavusha wana wa Israeli pale Jordani, anapovuka mto anapokea Roho wa Mungu ili apate nguvu ya kuwafikisha salama katika nchi ya ahadi. Ni katika mantiki hiyohiyo Masiha anapotoka majini Roho wa Mungu anashuka juu yake ili awaongoze wana wa Mungu katika uhuru na kweli ili wafike mbinguni. Watu wanaoongozwa na Bwana kuelekea kwenye uhuru na kweli ndo sisi, wajibu wetu ni kusikia sauti ya mchungaji mwema. (Yn. 10)

Mpendwa ninakutakieni heri na baraka tele katika sikukuu ya ubatizo wa Bwana na nakuomba usisahau wajibu wako ulioupokea kwa njia ya ubatizo, na kwa namna hiyo utakuwa unasherehekea pia ubatizo wako kila siku ya maisha yako.
Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.