2015-01-07 15:09:04

Papa anawashukuru akina Mama wote kwa wajibu wao muhimu kijamii na kiroho!


Baba Mtakatifu Francisko ametoa shukrani zake za dhati kwa wanawake wote, kwa wajibu na majukumu yao muhimu kijamii, kikanisa na kidunia kwa ujumla. Papa alitoa shukurani hizo wakati wa Katekesi yake kwa Mahujaji na wageni Jumatano hii, Katekesi iliyofuatia maadhimisho ya Sikukuu za Kiliturujia za Kanisa, katika kipindi hiki, zikiangalisha zaidi kwa Mama Bikira Maria , Mama wa Yesu.

Papa ameendelea kuzungumzia familia, kwa uvuvio wa uwepo wa Mama Maria, Mama yetu anayemwasilisha mtoto wake duniani. Katika tafakari hii juu ya majukumu ya Mama kwa jamii, na Kanisa Papa anasema, Kanisa pia ni sawa na Mama , na hivyo ndani yake hakuna muumini yatima. Na wakati huohuo ametoa wito kwa jamii, kuelewa matatizo na mahangaiko ya Mama katika maisha yake ya kila siku, ambayo hupambana nayo, katika majitoleo yake ya sadaka ya maisha , kwa ajili ya watoto wake.

Papa amekumbusha, ndani ya familia kuna mama , na kila binadamu, amepata maisha yake kutoka kwa mama na daima ni mama ambaye hutoa msaada mkubwa wa malezi katika yote mawili kibinadamu na kiroho pia. Mama, hata hivyo, kwa mara nyingi, licha ya kuwa na jukumu hili kubwa , katika maisha ya kila siku, uwepo wake haupewi uzito kama inavyotazamiwa. Na badala yake, mara nyingi majitoleo yake ya sadaka kwa watoto wao, huchukuliwa kama jambo la kawaida kwa maisha ya kijamii au hata kupuuzwa.

Papa aliendelea kuonyesha masikitiko yake kwamba, hata katika jamii za Kikristo, mama si mara zote hupewa haki na heshima anayostahili au kusikilizwa. Papa ameonyesha kujali na kuiomba jamii, ibadilike, ifanye mageuzi yenye hatua za kusikiliza na kuelewa malalamiko ya mama , iwe maisha ya kijamii au ndani ya maisha ya kanisa, mama waungwe mkono.

Lakini pia Papa alionyesha kutambua uwepo wa mama wachache ambao huvuka hata mipaka yao kama mama na kutenda kama wanaume. Amesema mama hao, wanakwenda nje ya barabara, na si sahihi kwao, kwa kuwa hujiongezea mzigo wa majukumu, katika kweli za maisha yao, kama wanawake, na maisha ya kifamilia.

Papa anataja ni umama ni fimbo ya nguvu yenye kusitisha moyo wa ubinafsi na uchoyo. Papa alifafanua maana ya ubinafsi katika maana ya kutokuwa na moyo wa kugawana na wengine . Mama mwema daima huwa tayari kugawana na wengine alivyo navyo kama inavyojionyesha katika shule yake ya malezi kwa watoto wao. Umama Papa anasema ni zaidi ya kuzaa watoto.Ni uchaguzi wa maisha yenye kuwa na mwelekeo wa kujitolea sadaka kwa ajili ya wengine, kuheshimu maisha na uwajibikaji katika kurithisha yaliyo mema na tunu msingi za kidini ambayo ni mambo muhimu kwa jamii adilifu na tulivu.

Papa ameeleza na kurejea maneno ya Marehemu Askofu Mkuu Oscar Arnulfo Romero aliyesema, kukubali kuwa mama mzazi ni sawa na kukubali kifo dini.. kama pia ilivyoandikwa katika mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican kwamba, "Sisi wote ni lazima kuwa tayari kufa kwa ajili ya imani yetu. Papa amezungumzia kwa kina heshima hii ya kuyatoa maisha kwa ajili ya mwingine akisema ni wajibu na haki katika maisha ya ukimya wa imani, sala na uaminifu, katika maisha ya kila siku, kuyatoa maisha hatua kwa hatua, kama anavyoyatoa mama kwa mwanae, bila hofu, wala kuchoka lakini kwa unyenyekevu hata wakati anapojua kufanya hivyo anaweka maisha yake katika hatari za kifo, huendelea kuwa kuwa shahidi wa maisha kuzaliwa na kuyahudumia kwa upendo .

Papa anasema Jamii bila mama, ni jamii isiyokuwa na ubinadamu, kwa sababu mama ni ushuhuda wa kugawana na kushirikishana yaliyo mema , na hata wakati mgumu, hubaki kuwa chimbuko la huruma, sadaka na nguvu ya maadili. Mama mara nyingi, ni nguzo katika utendaji wa kidini, ibada na sala, ambamo mtoto hujifunza, na kuiandika thamani ya imani katika maisha yake. Mama ni Mpanzi wa wa kwanza wa mbegu ya imani.

Bila mama, Kanisa haliwezi kuwa na waumini wapya, na imani huwa na mwelekeo wa kupoteza sehemu kubwa ya joto lake kirahisi. Papa alieleza na kutoa shukurani zake nyingi za dhati kwa mama wote, kwa familia na pia kwa Kanisa na Dunia.







All the contents on this site are copyrighted ©.