2015-01-07 14:05:31

Jengeni na kuimarisha umoja wa kitaifa!


Kwa mara ya kwanza katika historia ya maisha na utume wa Kanisa la Kikoptik, lililoko nchini Misri, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli yaani tarehe 6 Januari 2015, Rais Abdel Fattah Al-Sisi ameshiriki pamoja na kupata fursa ya kuzungumza na waamini waliokuwa wamefurika kwenye Kanisa kuu la Abasiya, lililoko Mjini Cairo, Misri.

Historia inaonesha kwamba, miaka ya nyuma, Marais walikuwa na utamaduni wa kutuma wawakilishi wao katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, lakini kwa Mwaka huu, Rais mwenyewe amehudhuria na kusalimiana na waamini, jambo ambalo limeleta matumaini na faraja katika mchakato wa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Misri, sanjari na kukazia uhuru wa kuabudu!

Rais Abdel Fattah Al-Sisi amemtakia kheri na matashi mema Papa Tawadros II, Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kikoptik la Misri. Rais amesema kwamba, kwa miaka mingi Misri imekuwa ni nchi ya rejea katika kuwafunda walimwengu ustaarabu, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatarajia makubwa kutoka Misri. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa kutambua kwamba, wote ni wanaunda taifa moja la Misri, licha ya tofauti zao za kiimani na kitamaduni.

Rais Abdel Fattah Al-Sisi anawataka viongozi wa kidini nchini Misri kuleta mapinduzi ya kweli katika mioyo ya watu kwa kuondokana na misimamo mikali ya kiimani, jambo ambalo linapelekea uwepo wa vitendo vya kigaidi, kikwazo kikubwa cha amani, ustawi na maendeleo ya watu. Misimamo mikali ya kiimani inayosigana na imani ya kweli ya dini ya Kiislam inaweza kuitumbukiza dini hii katika mwelekeo potofu miongoni mwa Jamii ya Kimataifa.

Kumbe, ni jukumu la viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanawafunda waamini wao kuwa kweli ni mashahidi wanaojitahidi kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa!







All the contents on this site are copyrighted ©.