Wachunguzi wa masuala ya afya ya binadamu wanasema kwamba, madhara ya ugonjwa wa Ebola
Afrika Magharibi yataendelea kudumu kwa muda mrefu na kwamba, watu wanaendelea kupoteza
maisha yao kutokana na kuambukizwa kwa virusi vya Ebola. Hadi kufikia mwishoni mwa
Mwezi Desemba 2014, zaidi ya watu 8880 walikuwa wameambukizwa virusi vya ugonjwa wa
Ebola nchini Sierra Leone.
Taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari za Kimissionari,
FIDES inaonesha kwamba ni zaidi ya wagonjwa 2529. Licha ya watu wengi kuendelea kupoteza
maisha yao, lakini kutokana na juhudi, zaidi ya wagonjwa 1326, wametibiwa na kupona
kabisa, tayari wamekwisharudi kwenye familia zao. Madhara ya virusi vya Ebola, vimesababisha
madhara hata katika ibada.
Waamini wanapokwenda Kanisani wanapaswa kuosha
mikono yao kwa maji yenye dawa, hawaruhusiwi kushikana mikono, wala Sakramenti ya
Ubatizo, Mpako wa wagonjwa na Ndoa Takatifu hazitolewi tena. Protokali iliyowekwa
inazuia pia mikusanyiko mikubwa ya watu, kwa hofu ya kuambukizwa virusi vya Ebola.
Kuna kundi la watoto yatima na watu waliosalimika kupoteza maisha, lakini bado wanabaguliwa
na kutengwa na jamii. Ubaguzi pia wanafanyiwa wale wanaohusika na huduma ya mazishi
wa ugonjwa wa Ebola! Kwa maneno machache, ugonjwa wa Ebola umetikisha maisha na imani
ya watu!