Watoto wanavyoguswa na shida na mateso ya watoto wenzao duniani!
Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu nchini Ujerumani, limeendelea kuonesha hali ya
kujali na kuguswa na mahangaiko ya watoto wenzao sehemu mbali mbali za dunia, kiasi
kwamba, kipindi cha Noeli, wanakitumia kwa ajili ya kukusanya fedha kwa ajili ya kuwasaidia
watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi sehemu mbali mbali za dunia.
Watoto hawa wanatekeleza utume huu kwa zaidi ya miaka hamsini na saba. Kampeni
ya Mwaka 2015 inaongozwa na kauli mbiu "Kupeleka na kuwa baraka. Lishe bora kwa watoto
nchini Ufilippini na duniani kote". Watoto wametembelea nyumba mbali mbali nchini
Ujerumani, ili kuomba mchango kwa ajili ya kuwasaidia watoto wenzao sehemu mbali mbali
za dunia kama kielelezo cha upendo na mshikamano wa kidugu.
Watoto hawa wamekuwa
wakichangia kwa kiasi kikubwa katika mikakati ya mshikamano wa upendo, kwa ajili ya
watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi sehemu mbali mbali za dunia.
Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 842 wanasumbuliwa kwa baa la
njaa na utapiamlo duniani. Kuna watoto millioni 2.6 chini ya umri wa miaka mitano
wanaofariki dunia kutokana na utapiamlo wa kutisha.
Shirika la Kipapa la Utoto
Mtakatifu nchini Ujerumani linajihusisha pia katika kuwasaidia watoto yatima, waliofiwa
na wazazi wao kutokana na ugonjwa wa Ukiwmi; watoto wanaoishi mazingira hatarishi
kiasi kwamba hawana tena fursa ya kuendelea na masomo; hawana fursa ya kupata maji
safi na salama; wote hawa wanaonjeshwa upendo kutoka katika mfuko wa fedha zinazochangishwa
na watoto hawa kutoka Ujerumani. Majimbo mbali mbali Barani Afrika pia yanaendelea
kuwekeza katika malezi na majiundo ya utume wa watoto, ili kuwajengea uwezo wa kuwa
ni Wamissionari kwa ajili ya watoto wenzao, ambao hawakubahatika kama wao!
Na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.