2015-01-06 15:15:23

Vatican-maelfu kwa maelfu ya waamini washiriki Sikukuu ya Epifania


(Vatican)Baba Mtakatifu Francisco, Jumanne nyakati za adhuhuri kabla ya sala ya Malaika wa Bwana, alipokea Maandamano yaliyofanyika kwa mujibu wa mapokeo ya utamaduni wa Waitaliani katika kuadhimisha Sikukuu ya Epifania, Sikukuu ya tokeo la Bwana. Tukio lililohudhuriwa na umati wa watu wasiopungua hamsini elfu, waliokusanyika katika uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Katika hotuba yake fupi, kwa ajili ya kupokea maandamano na sala ya Malaika wa Bwana , Papa alirejea kwa mara ingine, Sikukuu ya Tokeo la Bwana,akieleza kilichotokea katika pango la Bethlehemu, juu ya wachungaji wa Bethlehemu, watu wa Israeli; na maadhimisho ya Epifania, ambamo mama Kanisa anakumbuka kuwasili kwa Majusi, waliotoka Mashariki ya mbali, kwenda kumwabudu Mfalme wa Wayahudi aliyezaliwa, Mkombozi wa ulimwengu , na kumtolea zawadi zao.

Papa anasema, kitendo cha majusi kwenda kumwabudu mtoto Yesu, ni ushuhuda kwamba, Yesu alikuja duniani kuokoa, si kwa ajili ya kabila moja tu, lakini watu wote. Kwa hiyo, sikukuu ya Epifania, hupanua upeo wa macho ya dunia, kusherehekea "udhihirisho" wa Bwana kwa watu wote, kwamba ni udhihirisho wa upendo wa Mungu wa wokovu kwa binadamu wote. Na hivyo tunaona kwamba, upendo wake haukuwa na upendeleo, lakini unatolewa kwa watu wote. Na kama ilivyo kwamba ndiye Muumba na Baba, ndivyo ilivyo kwa wote kuwa ndiye yeye Mkombozi wa wote. Na hivyo watu wote wameitwa kuilisha daima imani na tumaini hili, kwa kila binadamu na wokovu wake , na hasa kwa wale wanaoonekana kuwa mbali na Bwana, au tuseme kuwa mbali na upendo wake wenye huruma na aminifu.

Papa aliendelea kuwazungumzia majusi wa Mashariki walivyofanya safari yao , akisema hii ni safari ya kiroho, safari ya kukutana na Kristo. Alikumbusha wao walikuwa makini na dalili zote zilizo onyesha uwepo wa mfalme aliyezaliwa, Masiya ; na hawakuchoka wala kukatishwa tamaa na matatizo yaliyojitokeza katika utafiti wao. Kwa ujasiri walitoka na kwenda kukutana na Bwana. Safari hii ya Majusi, ni safari ya Kila Mkristo.

Papa anasema, kama Majusi, pia kila Mkristo, anatakiwa kutoka na kwenda kumtafuta Mungu, ikiwa na maana ya kutembea, kwa kutazama nyota angani, kuona ishara inayoonekana ya nyota, Mungu asiyeonekana lakini ambaye anazungumza ndani ya mioyo yetu. Papa ameitaja ishara hii ya nyota , yenye uwezo wa kumwongoza mtu yeyote kwa Yesu, kuwa ni Neno la Mungu: mwanga unaoongoza njia yetu, wenye kuwasilisha imani yetu na kuifanya upya. Ni neno la Mungu lenye kuleta upya ndani ya mioyo yetu na jamii zetu.

Papa alieleza na kuhimiza , kutosahau kusoma na kutafakari kila siku Neno la Mungu, na kulimwilisha na kutembea nalo, kama moto wenye kutia joto mwilini, tunaotakiwa kubebana nao ndani mwetu kila siku, kwa ajili ya kuangazia hatua zetu, na hata wale ambao wanatembea kando yetu, ambao pengine labda wanajitahidi kutafuta njia yao kwa Kristo.


Papa pia katika siku kuu hii ya Epifania, alipeleka mawazo yake pia kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki Wakatoliki na Waotodosi , ambao wengi wao, wanaadhimisha Siku Kuu ya Noeli , Alhamisi hii tarehe 7 Januari kwa mujibu wa Kalenda yao. Na pia alikumbusha kwamba, leo pia dunia inaadhimisha Siku ya Dunia ya Utoto wa Kitume. Ni sherehe ya watoto, ambamo hufurahia zawadi ya imani na kuomba mwanga wa Yesu, uweze kuwafikia watoto wote wa dunia. Kwa ajili hii, Papa amewahimiza walimu wote , kupandikiza roho ya kimisionari kwa wadogo hawa, ili kuweze kuzaliwa kati yao, mashahidi wa upendo wa Mungu na watangazaji wa upendo wake.

Mwisho Papa, alimgeukia Mama Bikira Maria na kuomba ulinzi wake kwa kanisa la ulimwengu, na ili Injili ya Kristo iweze kuzamishwa , na kuwa mwanga kwa mataifa yote.








All the contents on this site are copyrighted ©.