2015-01-06 15:44:47

Kwa unyenyekevu, na tuulize, wapi mkombozi wa dunia alipolala- Papa


(Vatican) Mtoto Yesu alizaliwa mjini Bethlehemu na Bikira Maria, si tu, kwa watu wa Israeli, na kuwasilishwa na wachungaji wa Bethlehemu, lakini pia kwa ajili ya binadamu wote, na tena aliwasilishwa na watu wenye hekima na busara kutoka Mashariki.

Papa Francisko ameeleza mapema Jumanne hii , wakati akiongoza Ibada ya misa kwa ajili ya maadhimisho ya Sikukuu ya Epifania. Katika sikukuu hii Papa ametoa mwaliko kwa waamini wote, kuisherehekea Sikukuu ya Epifania, kama ilivyokuwa kwa watalaam wa nyota wenye hekima na busara, kufunga safari ya kwenda kumtafuta Masiya kwa ishara ya nyota walioona. Kufunga safari ya kiroho na kwenda kutafuta mahali alipolala mtoto Mkombozi wa Dunia.Amesema huo ndiyo mwaliko wa Mama Kanisa leo hii, kutafakari na kuomba neema ya kutambua maana ya tukio hili katika safari ya wokovu, ulioletwa na mtoto Yesu.

Homilia ya Papa ililenga katika masomo ya sikukuu hii, ambamo mnaelezwa juu ya wanajimu wa Mashariki, watu wenye hekima na busara kutoka Mashariki, akiwataja kuwa watu wa kwanza katika historia ya ukombozi wa Yesu, kufunga safari na kuandamana kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Isaya 60: 1-6). Papa anasema , maandamano ambayo tangu wakati huo, yameendelea kuwepo na kila kizazi kipya na lika husikia ujumbe wa nyota na kutafuta kumwona Mtoto, anaye onyesha huruma ya Mungu. Na kwamba kila kizazi kinapaswa kuangaziwa na nyota ile , na kushika njia na kwenda kumtafuta mahali alipo.

Homilia ya Papa, iliendelea kutafakari ujumbe wa Sikukuu hii, kwa kuwatazama watu wenye hekima, wahenga, watalaam na watazamaji wa nyota, katika mtazamo wa mazingira ya utamaduni wa kidini, ambamo nyota inaonekana kuwa na umuhimu na uwezo, juu ya mambo ya wanadamu. Na kwamba, Watu hao wenye busara wanawakilisha wanaume na mwanamke hata wa leo hii, wanaomtafuta Mungu katika dini za dunia na falsafa: jitihada zisizokuwa na mwisho.

Watu wenye busara ambao huonyesha njia, katika mapito ya safari ya maisha, kuutafuta ukweli wa mwanga, kama wimbo wa tokeo la Bwana unavyosema: "Lumen requirunt lumine"; kwa kufuata mwanga, waliouona mwanga. Walitoka nje na kwenda kumtafuta Mungu . Na kwa ishara ya Nyota , walizingatia ujumbe wake na kuanza safari ndefu. Papa amebainisha kwamba, ni Roho Mtakatifu ambaye aliwaita na kuwahimiza kwenda nje, na wakati wa safari pia waliweza kukutana binafsi na Mungu wa kweli.

Hata hivyo , Papa anaonya kwamba, safari hii ya kumtafuta Mungu alipo, inaweza kuwa si nyepesi kama tunavyoweza fikiri. Kama ilivyokuwa kwa wanajimu, pia hata leo hii kwa wanaomtafuta Mungu wa kweli, imejaa changamoto, matatizo na vipingamizi. Ni safari inayohitaji maongozi ya Roho Mtakatifu na si kutegemea akili za kibinadamu. Majusi walipofika Yerusalemu, walikwenda kwa nyumba ya Mfalme ambamo walifikiri ndiko kazaliwa Mfalme na kumbe wanakutana na majaribu ya Mfalme Herode.

Wakati huo wa majaribu , majusi waliipoteza nyota iliyokuwa mbele yao na kutumbukia katika majaribu ya shetani , udanganyifu wa Herode. Mfalme Herode hakuwa na nia ya kumwabudu mtoto lakini kumwangamiza. Herode alikuwa ni mtu mwenye nguvu ambaye hakuvumilia upinzani. Kichinichini, pia alimwona Mungu pia kuwa mpinzani, kwa hakika mpinzani wa hatari zaidi ya yote. Katika ukumbi wa Herode watu wenye hekima na uzoefu walipambana na kati wa upofu, lakini hawakukata tamaa. Papa ameshukuru uvuvio wa Roho Mtakatifu, ambaye huzungumza kwa njia ya unabii wa Maandiko Matakatifu, aliyewaonyesha kwamba, Masihi, atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi.

Papa aliendelea kutoa shukurani kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, yaliyowawezesha kutambua kwamba vigezo vya Mungu ni tofauti kabisa na vile vya binadamu. Kwamba Mungu hajionyeshi kama Mungu wa mabavu, lakini huzungumza kwa lugha ya unyenyekevu na upendo wake. Watu wenye hekima hivyo, wanauona uongofu wa kweli katika imani. Majusi hivyo, wanakuwa mfano wa kweli wa kubadilika katika imani. Wao waliamini zaidi katika wema wa Mungu kuliko katika ufahari dhahiri wa madaraka.

Kwa ufafanuzi huo, Papa alitoa mwaliko kwa watu wote pia leo, kujiuliza, wapi siri hii ya Mungu imefichika? Ni wapi wanaweza kumwona mtoto Yesu akiwa amelala horini? Papa alieleza kwa kuzitazama hali halisi za maisha ya kijamii leo hii, akitaja uwepo wa vita, madhulumu na manyanyaso kwa watoto, mateso mbalimbali ya maisha njaa, usafirishaji wa silaha, usafirishaji wa watu ... Anasema, katika mambo hayo yote, mna wake kwa waume , watu maskini wanapambanishwa na hali hizi. Humo ndimo mna mtoto Yesu aliyelala horini. (cf. Mt 25: 40,45).

Hori alimolazwa mtoto linatuonyesha sisi njia mbalimbali za kupata kumwona, ikiwa tofauti na mawazo ya dunia hii. Ni njia ya fumbo la Mungu mwenyewe, katika utukufu wa siri yake horini, katika mji wa Bethlehemu, na juu ya msalaba huko Kalvario, hali wanazoziishi ndugu zetu wateswa wake kwa waume.


Papa alikamilisha homilia yake juu ya Majusi wenye hekima katika fumbo hili, watu waliopata kufunuliwa siri ya fumbo hili, wakivuka upeo wa kibinadamu, katika uongofu wao. Na hivyo alimtaka kila mmoja aliyekuwa akimsikiliza, ajihoji mwenyewe, iwapo ameianza safari ya kwenda kuMtafuta mahali alipolala Mtoto Yesu, ili akamsujudie . Papa ametoa mwaliko wa kuomba majaliwa ya Bwana, katika kuipita njia ya safari hii ya maisha, ili kuweza kuwa na mabadiliko ya kweli, kupata hekima na busara katika kutoa maamuzi ya kimaisha. Aliongeza, tuombe ulinzi wa Bwana, ili atuweke huru dhidi ya majaribu wakati tunapopoteza mwelekeo wa maisha adilifu, nyota ya kutuongoza. Na daima mioyo yetu na isikome kuuliza swali, " iko wapi nyota? Na hasa wakati wowote wa kupambana na udanganyifu wa dunia hii, wakati nyota inapotoweka mbele yetu.
Papa aliomba, Mungu na atusaidie daima kugundua upya maana ya fumbo hili la wokovu, na si katika hali za mashaka mashaka, lakini kwa ishara inaonyesha mahali mtoto mchanga aliye vikwa nguo za kitoto, alipolazwa horini" (Lk 2:12), na kwa unyenyekevu kumwuliza mama, Mama yetu Maria, wapi tunaweza mwona Mtoto Yesu. Kupata ujasiri wa kukombolewa kutoka ndoto zetu, zenye kutia gizagiza taa yetu ya maisha. Kutafuta kwa ujasiri na katika unyenyekevu wa imani, njia ya kukutana na Mwanga, kama ilivyokuwa kwa Watakatifu Majusi, watu wenye busara. Amina.










All the contents on this site are copyrighted ©.