2015-01-06 09:35:18

Familia ni madhabahu ya upendo na Injili ya Uhai


Askofu mkuu Carlos Osoro Sierra wa Jimbo kuu la Madrid, Hispania, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu sanjari na maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba 2015, anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujifunga kibwebwe katika ujenzi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu kwa sasa na kwa siku za usoni!

Tunu msingi za maisha ya kifamilia hazina budi kuimarishwa kwa kutambua kwamba, familia ni kiini cha maisha ya mwanadamu na jamii katika ujumla wake. Familia kwa sasa inakumbana na changamoto kali katika maisha na utume wake. Lakini, hakuna haja ya wanafamilia kukata tamaa, bali wasonge mbele kwa kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu; inayomsaidia mwanadamu kutafakari uzuri na utakatifu wa familia; unaopaswa kuendelezwa na kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya.

Familia ni mahali ambapo, tunu msingi za maisha ya: kiroho, kiutu, kimaadili na kijamii zinarithishwa kwa utaratibu mzuri, kwani familia ni shule makini ya ubinadamu. Ni katika familia ya Kikristo, waamini wanatambua umuhimu wa kujenga na kudumisha upendo, ukarimu na wajibu msingi wa kuendelea kutangaza Injili ya Uhai, kwa kumpokea na kumtunza mtoto tangu pale anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake; ili binadamu aendelee kuwa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi.

Askofu mkuu Sierra anasema ni katika familia inayowajibika kikamilifu, wanafamilia wanaweza kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kusaidiana sanjari na kujenga mfungamano wa udugu, ukoo na jamii katika ujumla wake. Kwa kawaida ndani ya familia kila mtu anapaswa kujisikia kuwa "nyumbani" na hakuna mtu anayepaswa kutengwa au kubaguliwa kwa sababu yoyote ile, kwani familia ni kisima cha upendo, kila mtu anaweza kujichotea kadiri ya mahitaji yake pamoja na kuwasaidia wadhaifu zaidi, ili kuendelea kumtukuza Mwenyezi Mungu, anayemshirikisha mwanadamu katika kazi ya uumbaji na malezi kwa watoto ambao kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Ndani ya familia, watu wanajifunza na kurithishana karama msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili; mambo msingi katika maisha. Kutokana na mwelekeo huu, Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ni kioo cha familia za Kikristo na mfano wa kuigwa na watu wote wenye mapenzi mema.

Askofu Sierra anasema, familia inayojikita katika umoja, upendo na udumifu mambo yanayofumbatwa katika Sakramenti ya Ndoa Takatifu; kwa kujitajirisha kwa tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma; pamoja na kuendelea kuboresha maisha yake ya kiroho kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho; familia ya namna hii inatekeleza kweli dhamana na utume wake na kwa jinsi hii, inaweza kuwa ni Injili ya Familia inayotangazwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha!

Askofu mkuu Carlos Osoro Sierra wa Jimbo kuu la Madrid, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiangalia Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kwa jicho la imani na matumaini pasi na kukata tamaa hata pale wanapokabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.









All the contents on this site are copyrighted ©.