2015-01-05 07:48:59

Yataka moyo kweli kweli!


Ushemasi ni daraja la huduma kwa Neno la Mungu linalomwilishwa katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ni daraja la huduma katika maisha ya kiroho; ni chemchemi ya matumaini mapya kwa watu waliokata tamaa, wale waliopotea na wote waliokufa kiimani. RealAudioMP3

Ni huduma inayojikita katika unyenyekevu, imani, matumaini na mapendo. Hili ndilo daraja ninalojiandaa ili kulipokea hapo tarehe 6 Januari 2015 pamoja na ndugu yangu Justus Okibo, kutoka Jimbo Katoliki la Kisii, Kenya.

Naitwa Frateri Aristid Shayo. Nilizaliwa katika jimbo la Moshi parokia ya Lowerere. Mimi ni mtoto wa pili kati ya watoto 9 wa Mzee Michael Shayo na Rosalia Makombo. Tangu utoto wangu, nimelelewa katika maadili na desturi za Kikatoliki. Kila siku asubuhi na jioni ilikuwa ni sheria kusali pamoja katika familia yetu, kwa kutambua kwamba, familia ni shule ya sala, utakatifu na chimbuko la miito mbali mbali.

Mama daima alikuwa anatuhimiza kusali kwa njia ya ushiriki mkamilifu na wala hakupenda kuwaona watoto wake wakichapa usingizi wakat iwa sala, ikizingatiwa kwamba, wakati fulani Rombo kuna baridi! Sala ya kwanza kabisa kujifunza katika utoto wangu ilikuwa sala ya kubariki chakula na kushukuru ambayo nilifundishwa na mama yangu.

Historia fupi ya wito wangu!
Katika utoto wangu, nilitamani sana kutumikia misa. Kwa kifupi ni kwamba nilikuwa navutiwa sana na kutoa huduma pale Altareni hasa kushika chetezo. Kwa kweli sikuwa naelewa ni kwa nini hasa nilivutiwa hivyo ila nilitamani kufanya hivyo muda na wakati wowote. Suala la kufukuzia chetezo, na ule moshi wa ubani vilikuwa vinanipa raha ya ajabu. Nilitamani sana siku moja na mimi nifanye kama anavyofanya Padre Altareni. Hii ilinifanya nitamani kuingia seminarini. Nilipomaliza shule ya msingi niliomba kujiunga na Seminari ndogo ya Maua inayoongozwa na Wakapuchini iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi lakini kwa bahati mbaya sikuweza kuchaguliwa.

Hii ilinifanya nikate tamaa kabisa.
Niliamua kutokupoteza muda na kuendelea na masomo ya sekondari, nilisoma kidato cha kwanza hadi cha nne katika sekondari ya kutwa ya Tarakea kule Rombo, Kilimanjaro. Muda wote nikiwa shuleni hapo nilikuwa najishughulisha na shughuli za TYCS lakini wazo la kujiunga na seminari halikuwepo tena moyoni. Baada ya kidato cha nne, nilijiunga na kidato cha tano katika sekondari ya Galanos kule mkoani Tanga. Hapa ndipo palikuwa kitovu cha kugundua tena wito wangu.

Kama kawaida nilijishughulisha sana na shughuli za kanisa shuleni pale hasa katika chama cha wanafunzi wakatoliki Tanzania (TYCS).
Mara kwa mara Padre Titus Mdoe ambaye kwa sasa Askofu Msaidizi wa jimbo kuu la Dar es Salaam alikuwa anatutembelea. Akiwa kama mlezi wa vijana jimboni Tanga alitulea kwa namna ya kipekee katika imani katoliki. Zaidi sana Padre Firmati Tarimo ambaye kwa sasa ni mkuu wa Warosmini kanda ya Afrika alikuwa anatutembelea pia pale shuleni.
Siku ya siku mashirika matano ya kitawa na kimisionari yalifanya semina ya kukuza miito katika makao makuu ya Warosmini Mwambani Tanga.

Walikuwemo Warosmini wenyewe, Wayesuit, Mamisionari wa Afrika, Wadomenikani na ”Christian Brothers”. Tulienda mwambani kuwasikiliza kuanzia Ijumaa jioni hadi Jumapili. Kwa kweli hapo ndipo nilipogundua tena wito wangu. Kuanzia siku hiyo nilifanya maamuzi ya kuwaza tena kuhusu maisha ya kipadre. Niseme tu kwamba, nilivutiwa sana na karama ya Mwenye heri Antonio Rosmini ambayo ni Mapendo yasiyo na kikomo kwa Mungu na kwa Jirani.

Nilijiunga na Shirika mwaka 2004, malezi ya kwanza nilifanyia Lushoto, baadaye, nikasoma Falsafa Nairobi, Kenya. Kwa sasa nipo hapa Roma nasoma Teologia mwaka wa tatu katika chuo kikuu cha Kipapa cha Lateran. Tarehe 6 Januari 2015 Siku ya Tokeo la Bwana, au Epifania ya Bwana itakuwa siku ya muhimu sana katika historia ya maisha na wito wangu.

Siku hii nitapewa daraja la Ushemasi hapa Roma na Askofu Mkuu mstaafu Alessandro Plotti wa Jimbo kuu la Pisa, Italia. Nazidi kuomba neema za Mungu ili nipewapo daraja hili la ushemasi nipende zaidi kuhudumia watu wa Mungu kwa Neno na Matendo ya huruma na sio kuhudumiwa.

Namshukuru sana Mwenyezi Mungu, kwa kunipa nguvu hadi nikaweza kudumu katika safari hii. Nawashukuru wazazi wangu kwa kunilea katika maisha ya kikatoliki.
Nawashukuru walimu wangu wote pamoja Warosmini wote kwa kunipokea na kunilea katika Shirika hili la Mapendo.


ARISTID MICHAEL SHAYO, (I.C).








All the contents on this site are copyrighted ©.