2015-01-05 08:33:01

Uongozi ni huduma wala si ujiko!


Waamini wa Kanisa Katoliki pamoja na watu wenye mapenzi mema nchini Nigeria wanadhamana ya kuhakikisha kwamba, kwa njia ya ushiriki na ushuhuda wao katika maisha ya kisiasa, kijamii na kiuchumi, wanayatakatifuza malimwengu kwa kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, kwa maneno na matendo yao. Kwa njia hii waamini wanaweza kuyatakatifuza malimwengu na Nigeria, ikawa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kuliko hali ilivyo kwa sasa, ambako siasa imegeuzwa kuwa ni mchezo mchafu unaoendelea kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia, kutokana na uchu wa mali na madaraka!

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Alfred Martins wa Jimbo kuu la Lagos, Nigeria wakati wa Kongamano la Wakatoliki Kijamii, lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Bwana, tupatie viongozi kadiri ya moyo wako”. Kongamano hili limefanyika mwanzoni kabisa mwa Mwaka 2015, mwaka ambao Nigeria inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu, ambao kwa sasa kimebaki kuwa ni kitendawili kutokana na kinzani na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kutokea nchini humo.

Askofu mkuu Martins anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wenye sifa, uwezo na vigezo vya kuwania nafasi mbali mbali za uongozi kujitokeza, lakini kwa kutambua kwamba, uongozi ni huduma na wala si kwa ajili ya kujitafutia umaarufu wala utajiri; mambo ambayo yamekuwa ni chanzo kikuu cha kuvunjika kwa misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Kuna haja pia ya kufanya maboresho makubwa katika mchakato wa kuwapata viongozi wa kisiasa wanaowania madaraka nchini Nigeria, ili kweli wawe ni watu safi, wapenda haki na amani; Wachamungu na wapenda maendeleo ya watu wao! Mchakato wa kuwapata viongozi wa kisiasa uongozwe na demokrasia ya kweli na kamwe udini, ukabila na umajimbo visipewe nafasi kwani ni hatari kwa mfungamano wa kitaifa.

Chaguzi nyingi zimekuwa ni chanzo cha majanga, rushwa, vita na kinzani, kumbe, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, mambo haya yanabaki kuwa ni historia iliyopitwa na wakati. Watu wasitumie dini zao kama chambo cha kuombea kura! Kanisa linafundisha kwamba, uongozi ni huduma inayopania kulinda na kudumisha: utu, heshima na mafao ya wengi.

Viongozi wanaochaguliwa wahakikishe kwamba, kweli wanakuwa ni vikolezo vya maendeleo endelevu ya watu, kwa kuwahakikishia kwamba, wanapata: makazi safi na bora; chakula na maji safi na salama; huduma bora za elimu na afya; usalama wa maisha na mali zao pamoja na huduma muhimu zinazopania kuharakisha maendeleo ya watu.

Uongozi si daraja la kujitafutia umaarufu wala mali! Waamini wawaombee viongozi watakaochaguliwa waweze kuwa na karama za Roho Mtakatifu, ili kuleta mabadiliko nchini Nigeria, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, washiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 si kwa kujikita katika ubinafsi, wala kwa kutafuta ujiko wala mali, bali kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya wananchi wote wa Nigeria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.