Rushwa, ufisadi na mmong'onyoko wa maadili ni majanga ya kitaifa!
Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana katika ujumbe wake kwa ajili ya Maadhimisho ya Noeli
na Mwaka Mpya 2015, linasema, rushwa na ufisadi wa mali ya umma; biashara na matumizi
haramu ya dawa za kulevya sanjari na kuporomoka kwa kanuni na tunu msingi za kimaadili
na utu wema; ni mambo ambayo yanatishia amani, usalama, umoja na mshikamano wa kitaifa
nchini Ghana.
Haya ni mambo ambayo yanawagusa wananchi wengi na kwamba, si
rahisi mtu kujitutumua kwamba, kamwe hausiki na “majanga haya ya kitaifa”. Maaskofu
wanakiri kwamba, hata baadhi ya viongozi wa Kanisa wametikiswa na majanga haya katika
maisha na utume wao. Kwa hakika wanasema Maaskofu, bila “majanga haya ya kitaifa”
Ghana ingekuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.
Baraza la Maaskofu Katoliki
Ghana linasema kwamba, kuna haja kwa wananchi wote wa Ghana katika ujumla wao kusimama
kidete kupinga kwa nguvu zote tabia ya kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili
na utu wema; kwa kusimama kidete ili kushuhudia tunu msingi za maisha ya kiroho na
kiutu kila mwamini kadiri ya imani yake.
Leo hii nchini Ghana, ulevi wa kupindukia,
biashara ya ngono, utoaji wa mimba, utumiaji haramu wa dawa za kulevya, rushwa na
ufisadi ni mambo ya kawaida kabisa, kiasi kwamba, mwananchi anayekwenda kinyume cha
mwlekeo huu wa kijamii, anaonekana kuwa ni kituko! Dhamiri za watu zinaanza kuharibika
kiasi kwamba, watu wanashindwa kuona ubaya wa dhambi na badala yake, fedha imewekwa
mbele kwa mambo mengi!
Yote ni mambo ambayo yanaendelea kubomoa misingi ya
ustawi na maendeleo ya wananchi wa Ghana! Hapa kuna haja ya kubadilisha mwelekeo kwa
kujikita katika kanuni maadili na utu wema, kila mtu akijitahidi kuwa kweli ni shuhuda
wa imani yake. Maaskofu wanawahamasishwa wananchi kujenga na kuimarisha utamaduni
wa msamaha, ukweli na upatanisho badala ya kuendekeza tabia ya kutaka kulipizana kisasi!
Baraza
la Maaskofu linapenda kuwaonya Mapadre na Watawa kusimama kidete katika misingi ya
Kiinjili, utu na maadili mema na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu kwa kuthamini
na kupenda mno fedha na mali; mambo ambayo yanaweza kuwaletea hatari katika utekelezaji
wa majukumu yao katika maisha na utume wa Kanisa. Wasipokuwa makini wanaweza kujikuta
“wakila kwenye nyumba za wajane na maskini” wanaowaendea kutafuta suluhu ya matatizo
na changamoto za maisha.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S Idhaa ya Kiswahili
ya Radio Vatican.