2015-01-05 10:36:51

Nendeni Jangwani kwa ajili ya Mwaka 2015


Katika Maandiko Matakatifu tunasoma yafuatayo: "Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani, akakaa huko siku arobaini akijaribiwa na shetani" (Marko 1:12-13).Yesu anaenda Jangwani na kukaa huko kwa muda wa siku arobaini. Lengo la kwenda jangwani si kujaribiwa ila kujiandaa kwa kazi iliyokuwapo mbele yake, kazi ya kumkomboa mwanadamu. Yesu alikwenda kutafakari kazi yake yote na yale yatakayompata katika kazi hiyo. Yesu alikwenda kutengeneza dira ya utekelezaji wa kazi ya ukombozi.
Nasi tunapoanza Mwaka Mpya 2015 tunahitaji kuingia katika 'jangwani' la kiroho na kimaisha ili kujitengenezea dira ya utekelezaji kwa mwaka mzima. Tujiwekee malengo binafsi, malengo ya familia, Jumuiya, kanda, kigango, parokia, jimbo na mahali pa kazi. Ni kipindi cha kujiwekea malengo ya kiroho, kiuchumi na kijamii. Mathalani. Mfano :
KIROHO: Jipangie mwaka huu unataka kufika wapi? Panga mambo yako ya kukua kiroho;tafakari ya Neno la Mungu; sala binafsi, sala za familia, ushiriki wako katika Jumuiya, kanda, kigango, parokia na kijimbo. Panga kushiriki mafungo ya kiroho, semina za kiroho, hija na matendo ya huruma. Ushiriki wako katika vipindi vya Kwaresma, Pasaka, Majilio na Krismas n.k.
KIUCHUMI: Tengeneza dira ya kiuchumi mwanzoni mwa mwaka kwa kupanga unataka kufika wapi kiuchumi mwaka huu. Usiache suala la uchumi likuendeshe bali wewe ulitawale kwa kufuata utakachojipangia mwanzoni mwa mwaka. Utajikuta unafanya mambo mengi kwa mpangilio hadi unafurahia maisha. Panga bajeti ya mwaka mzima; mapato na matumizi yako yaandike ili yakuongoze.
Bajeti yako iwe shirikishi ili itekelezeke, isiwe siri yako. Shiriki au ongoza kupanga bajeti ya mwaka ya familia, jumuiya, parokia, jimbo na mahali pa kazi. Iheshimu bajeti hiyo. Bajeti yako ianze na matumizi ili ikuongoze kupanga mapato. Kama mapato ni madogo kulingana na matumizi; fanya ubunifu, fikiria fursa mpya na zifanyie kazi, pia punguza matumizi yasiyo ya lazima, kadi za michango isiyo ya lazima, vikao visivyo na tija vitakavyokugharimu n.k. Wakati mwingine ni heri ya lawama kuliko fedheha!
Panga zaka yako, sadaka, majitoleo, michango ya Jumuiya, mavuno ya parokia, mavuno ya jimbo n.k usikurupuke kila siku na kwenda kutoa 'makombo' hayana nafasi mbele ya Mungu ni sawa na kujiletea 'laana' maishani mwako.
Mambo mengine muhimu ya kupanga katika dira ya mwaka huu ni pamoja na kushiriki matukio muhimu ya kijamii. Ni mwaka wa kura za maoni ya kupata katiba ya nchi yetu, usithubutu kupanga kutokushiriki, huo ni wajibu wa kila raia wa Tanzania.
Kushiriki uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais. Ili tupate viongozi wazuri, wachamungu, waadilifu na wakweli, jitokeze ili uchaguliwe na/au uchague kiongozi atakayetufaa kuiongoza jamii na nchi yetu.
Mwaka wa Familia utafungwa rasmi mwaka huu, Je, umeambulia nini kiimani? Umejiwekea mikakati gani ya kutengeneza mapungufu yaliyo ndani ya familia yako? Shiriki vyema semina za mwaka wa familia. Huu pia ni Mwaka wa Watawa Duniani, Je, unashiriki namna gani katika kuhamasisha, kukuza na kulea miito mitakatifu ndani ya Kanisa?
Huu ni mwaka wa uchaguzi wa viongozi wa Kanisa - walei kuanzia ngazi ya Jumuiya ndogondogo hadi Taifa. Jitokeze uchaguliwe na uchague viongozi hao. Shiriki kikamilifu kwani kanisa linakuhitaji.
Yote hayo yanatuhitaji kwenda 'jangwani' ili kujipanga. Tumshirikishe Mungu kupitia sala na mafungo. Tumkabidhi Mungu malengo yetu ya mwaka 2015. Tujitathmini mara kwa mara juu ya utekelezaji wa malengo hayo. Tuache kuishi kwa mazoea, mwaka 2015 tuwe wahalisia, tusibahatishe! Tuepuke mikwaruzano, tuongeze furaha na ufanisi. Tuwe 'Kristu' katika maisha yetu ya kila siku ili kuisaidia jamii. Tuache kulalamika lalamika, tuchukue hatua.
Wapendwa, Heri ya Mwaka Mpya 2015!
Na Antipasi Shinyambala!
Dar es Salaam, Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.