Baba Mtakatifu Francisko katika Siku kuu ya Tokeo la Bwana, au Epifania ya Bwana,
inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 6 Januari, anatarajiwa kuadhimisha Ibada
ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuanzia saa 4:00
za asubuhi kwa saa za Ulaya.
Hii ni Siku
kuu ambayo Yesu, Mwana wa Mungu alipenda kujifunua kwa mataifa, akawa ni kivutio kikubwa
cha wataalam wa nyota kutoka Mashariki wanaojulikana kama Mamajusi kutoka Mashariki
ya Mbali. Wataalam hawa wa nyota kadiri ya Mapokeo ya Kanisa wanaitwa: Gaspar, maana
yake, mtu mwenye heshima au mwalimu; Melchior jina linalomaanisha: Mfalme wangu ni
mwanga na Balthazar maana yake Mungu ayalinde maisha yako! Hii ni Siku kuu yenye utajiri
mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa waamini kuwa kweli ni chumvi
ya dunia na mwanga wa mataifa.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa
ya Kiswahili ya Radio Vatican.