2015-01-05 10:22:26

Mseminari wa zamani!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo na kwa mara nyingine tena Heri kwa Mwaka Mpya 2015! Tunawatakia wasikilizaji wote wa Radio Vatican heri na Baraka katika mwaka huu na nyakati zote. Kumbuka: Muda ni zawadi kutoka kwa Mungu, mwito kwa kila mmoja wetu kuutumia muda vizuri kwa ajili ya maendeleo binafsi na kwa manufaa ya wengi. RealAudioMP3

Basi, karibu tuendelee kupapasa hati za mtaguso Mkuu wa pili wa Vatikani, kutokamo tuendelee kuhekimishwa katika yale yenye kutujenga katika maisha yetu ya kumwendea Mungu. Baada ya kuitazama ile hati iliyohusu daraja ya Mapadre katika Kanisa katika kipindi kilichopita, leo kwa mantiki tuitazame hati inayohusu malezi ya Waseminari; ijulikanayo kwa lugha ya kikatini kwa jina la OPTATAM TOTIUS, maana yake kuchagua yaliyo bora.

Mintafaru malezi ya Waseminari, Mtaguso umegusa maeneo mbalimbali ya malezi kwa majandokasisi wetu wanapokuwepo Seminarini na pia wanapokuwepo katika mazingira ya nje. Mfumo wa malezi umeratibiwa kwa hekima kubwa, ili kuweza kuwapata mapadre walioiva vizuri kuweza kuifaa jamii ya watu wa nyakati zetu. Mfumo huo wa malezi ya kiroho na kitaaluma uliowekwa, unalengo la kumuunda mseminari katika ukomavu mkamilifu, ili kuweza kumpata padre aliyekomaa kimwili, kiroho, kiakili, kifikra, kijamii, kisaikolojia na kiutendaji. Ni kwa mtazamo huo tunaona kwamba, malezi ya Kipadre ni ya kina na yanachukua muda mrefu wa kutosha.

Mama Kanisa amepanga mfumo huo wa malezi kwa uzito mkubwa, akijua fika uzito na umuhimu wa huduma ya Kipadre katika Kanisa. Mama Kanisa anataka wale walioitwa katika huduma takatifu ya altare, waandaliwe vema, ili kweli waweze kumudu kazi ya kuzinena siri za Kristo, kufafanua mafumbo ya Mungu kwa watu na kuadhimisha sakramenti za Kanisa kwa ajili ya wokovu wa watu.

Katika hati hii, jumuiya nzima ya waamini imejukumishwa swala la malezi ya vijana na ustawi wa miito hasa kwa njia ya sala. Njia ya kawaida ya kuotesha mbegu za miito ni seminari ndogo. Na kwa nyakati zetu hizi, milango ya miito inachipua sana pia kupitia katika sekondari zisizo za mlengo wa ki-jandokasisi. Iwe ni seminarini, au nje ya seminari, jambo la msingi kabisa ni malezi bora, ili pale vijana wetu wenye kuitikia wito wanapoenda katika majiundo makini katika seminari kuu, malezi hayo ya seminari kuu yawe ni ukuta unaojengwa katika msingi wa malezi bora ya kiimani na kitaaluma waliyoyapata tangu awali.

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, umetoa mwangwi mkubwa wa uwajibikaji wa malezi hayo kwa sisi wakristo wote. Ni jukumu letu kuchochea, kuibua, kukuza na kutunza mbegu ya wito ndani ya vijana wetu na kuwasindikiza hatua kwa hatua hadi wafikie altare takatifu ya Bwana. Tunaambiwa sisi Wakristo tutatekeleza wajibu huo vema kwa kuishi maisha bora ya Kikristo. Tunakubaliana kwamba, sisi kama waamini tunahitaji wachungaji, na wachungaji hao ni watoto wetu, wanatoka kwetu sisi wenyewe. Hivyo ni wajibu wetu kuwaandaa vizuri, kushirikiana na taratibu zilizowekwa na Kanisa ili tupate wahudumu bora wa altare.

Mpendwa Mwana Kanisa la Nyumbani, Mtaguso unatuambia kwamba ‘familia zetu zikiongozwa na roho ya imani, upendo na uchaji wa Mungu, hapo hufanywa kama ndio seminari ya kwanza kabisa’. Tazama, leo, tunaambiwa kuwa familia zetu ndio seminari za msingi. Mwito kwa familia kujibidisha kweli kufundisha watoto dini na maadili na kuwekea mkazo maendeleo ya kitaaluma kuanzia katika shule za msingi, ili wakifika ngazi ya seminari, wasioone masomo ni magumu na hivyo kuhisi kuwa upadre ni mgumu.

Mtaguso pia unagusa juu ya uwajibikaji wa Parokia katika malezi ya waseminari. Tunaelekezwa kwamba, parokia zilete uhai, na vijana wenyewe washiriki katika malezi yao. Katika mikutano mbalimbali, mada zihusuzo wito mtakatifu zifundishwe kwa vijana, ili waweze kutambua wito huo na kuufuata kwa hiari. Na mapadre na maaskofu wetu nao wameelekezwa kuonesha juhudi zao za kitume katika kuiendeleza miito mitakatifu, na kujibidisha kuivutia mioyo ya vijana waume kupenda maisha ya upadre. Hadi hapo tunaona jinsi ambavyo sote katika Kanisa tunawajibika katika suala hili muhimu.

Mpendwa msikilizaji, tukubaliane kwamba, mtu anayejitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu, anatoa sadaka ya nafsi yake kamilifu. Ndiyo maana kuna vigezo vya kiimani, kiakili, kimwili na kijamii, kuhakikisha kuwa huyu mtu anafaa kwa ajili ya huduma takatifu. Imetokea bahati mbaya sana katika nyakati fulani, badala ya kuwatia moyo vijana wetu wasonge mbele katika njia yao ya kumtumikia Mungu, tukawakatisha tamaa kwa sababu tu za ubinafsi wetu.

Watoto wetu wakionekana wana akili nyingi, ni sisi wazazi na wanandugu na watu wengine wasiomtakia Mungu mema, tunawashawishi kwamba, kwa akili nzuri uliyo nayo hupaswi kwenda Seminari kuu, nenda chuo kikuu usome uajiriwe. Kwa sababu ya tabia hizo, tutaona kwamba katika seminari ndogo tunakuwa na waseminari wengi, lakini baada ya malezi ya seminari ndogo na za kati, vijana wanapukutika kwa sababu tele za kupoteza mwelekeo.

Ni nani aliyesema Upadre hauhitaji watu wenye akili nzuri? Ni nani alisema wanaokuwa mapadre ni wale walioshindwa maisha? Dhana hizo potovu kutoka kwetu sisi wenyewe ambao tuna wajibu wa kuwalea vema waseminari wetu, ndio zimewafanya baadhi ya vijana wazuri waliokuwa na wito haswa wakakata tamaa, na Kanisa linaendelea kukosa wachungaji. Kwa kufanya hivyo tunalitakia nini Kanisa letu?

Pamoja na maelekezo ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vaticani mintarafu malezi ya waseminari wetu, sisi nasi, kwa kuzingatia hali halisi ya nyakati zetu, tunaomba tutoe rai kwako mpendwa msikilizaji. Nyakati zile Kanisa la Missioni lilikuwa linategemezwa kwa kiasi kikubwa sana na Kanisa la Ulaya. Wafadhili waliweza kulipia masomo ya waseminari na malipo ya waalimu wao pia. Leo ndugu mpendwa upepo umebadilika! Imani Ulaya imepoa, watu wamepungua kabisa makanisani na wafadhili hakuna tena.

Ni jukumu langu mimi na wewe, kumsaidia Askofu wetu kuwasomesha Waseminari hadi wafikie daraja Takatifu. Tunaamini kwa dhati kwamba tukitaka tunaweza. Parokia nzima haitashindwa kulipa karo ya mseminari mmoja katika Seminari Kuu kwa miaka yote anayosoma huko.

Pia tunapeleka mwito kwa watu binafsi, au familia au jumuiya ndogondogo, jisadakeni kwa dhati ili kuweza kumfadhili kiuchumi mseminari mmoja mmoja kupitia mikono ya Askofu hadi afikie daraja takatifu. Hakika, tuwe wafadhili wa sala na ada. Wakati mwingine waseminari wetu wanaishi katika maisha duni na ya kukatisha tamaa hadi inakuwa aibu kuwa mseminari, na hatimaye hufikia hatua ya kupoteza wito, kwa sababu sisi Wanaparokia kuonekana kwamba hatuwajali, hatuwatunzi vizuri, hatuna ukaribu wa ukarimu kwao, ni kuwasemasema tu na kuwatishatisha na kuwazulia majanga ambayo yanawakwamisha katika safari yao. Tuwajenge, tuwatie moyo, wasije wakakata tamaa.

Wakati mwingine tunasali tu, kumwombea mseminari wetu afikie upadre. Hilo ni sawa lakini peke yake halitoshi!! Sala pekeyake hazilipi ada wala kununua madaftari na sabuni. Tuwafadhilie mahitaji yao ya kila siku. Tuamke wapendwa, wakati ndio huu wa kutupilia mbali blanketi zito lenye ndoto za ufadhili wa Ulaya. Wewe na mimi ndio wafadhili wenyewe. Tuitikie wito huu wa Mtaguso Mkuu, ili tumpatie Mama Kanisa Wahudumu wa Altare Takatifu, kwa ajili ya utakatifu wa ulimwengu na wokovu wa roho zetu.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB (Mseminari wa zamani).








All the contents on this site are copyrighted ©.