2015-01-05 11:55:00

Jengo jingine limeporomoka Jijini Nairobi!


Taarifa kutoka Jeshi la Polisi nchini Kenya zinasema kwamba, watu wawili wamepoteza maisha na wengine thelathini na wanane kujeruhiwa vibaya baada ya Jengo lenye ghorofa nane lililokuwa linatumika kama makazi ya watu kuporomoka, Jijini Nairobi, jumapili tarehe 4 Januari 2015.

Taarifa zinasema kwamba, bado kuna idadi kubwa ya wakazi waliokuwa wanaishi kwenye jengo hili hawafahamiki mahali waliko na kwamba, juhudi za Kikosi cha Uokoaji zinaendelea kuwatafuta watu ambao wanahofiwa kwamba, wamefunikwa kwa kifusi cha jengo hili. Taarifa zinasema kwamba, ujenzi wa jengo hili haukuzingatia muda, kiasi kwamba, ulifanywa kwa haraka sana, ili kukidhi mahitaji ya makazi ya watu ambayo kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Jiji la Nairobi.

Itakumbukwa kwamba, Mwezi Desemba 2014, watu wanane walifariki dunia baada ya Jengo kuporomoka katika eneo la Kaloleni, nje kidogo ya Jiji la Nairobi. Kutokana na uhaba mkubwa wa makazi ya watu, baadhi ya wajenzi na wamiliki wa majengo wanakiuka sheria kwa makusudi, ili kupunguza gharama za ujenzi na hatimaye, kupata faida kubwa lakini kwa gharama ya maisha ya watu wasiokuwa na hatia!







All the contents on this site are copyrighted ©.