2015-01-03 10:27:10

Tumieni njia za mawasiliano ya jamii katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya!


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa mwaka kwa kutaka Kanisa Barani Asia kuimarisha zaidi tasaufi ya mawasiliano ya jamii pamoja na kujikita zaidi katika mchakato wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. RealAudioMP3

Maaskofu wanatambua na kuthamini mchango unatolewa na vyombo vya mawasiliano ya jamii katika Uinjilishaji Mpya na kwamba, Kanisa halina budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa kutangaza Injili ya Kristo kwa ari na moyo mkuu. Mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa Barani Asia hayana budi kuzingatia kanuni maadili na tamaduni za wananchi wa Bara la Asia, kwa kutambua kwamba, hivi ni vyombo vinavyopaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na utamadunisho, ili kweli Injili iweze kuota mizizi katika maisha na vipaumbele vya watu; kwa kusafisha na kuboresha pale ambapo tamaduni hizi zinasigana na Habari Njema ya Wokovu.

Njia za mawasiliano ya kijamii ziwe ni madaraja yanayowaunganisha watu ili kukoleza majadiliano na maelewano, ili kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Maaskofu wanatambua mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii na changamoto zilizopo kwa vyombo vya habari Barani Asia kwa kusema kwamba, kuna haja ya kuwa na mbinu mkakati mpya wa mawasiliano kwa kusoma alama za nyakati, ili kukabiliana na mabadilio haya, vinginevyo, Kanisa linaweza kujikuta limepitwa na wakati katika mawasiliano ya kijamii.

Maaskofu wanasema, jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linawafunda Wakristo wanaojihusisha na vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili waweze kutekeleza kikamilifu dhamana na utume wao, kwa kuzingatia weledi na taaluma; ukweli na uwazi sanjari na kanuni maadili; kwa kukuza udugu, mshikamano wa upendo katika shughuli za kichungaji pamoja na kuwa na huruma.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia linataka kuwepo na Jukwa la Mawasiliano litakalounganisha Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, ili kushirikishana rasilimali fedha na watu; uzoefu na mang’amuzi pamoja na habari katika ulimwengu wa mawasiliano.

Maaskofu wanasema kuna haja ya kufanya maboresho makubwa katika taasisi za mawasiliano zinazomilikiwa na kuendeshwa na Mama Kanisa Barani Asia, kwa kukazia majiundo makini katika mikakati ya shughuli za kichungaji, ili kweli Fumbo la Umwilisho kama anavyosema Mtakatifu Yohane Paulo II, liwe ni kielelezo cha juu kabisa cha ufunuo wa Mungu kwa mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.