2015-01-03 10:18:34

Silaha za kinyuklia bado zinatishia amani na utulivu!


Silaha za kinyuklia ni tatizo la kimataifa linalohitaji kudhibitiwa kwa kuzingatiwa kanuni maadili, kutokana na ukweli kwamba, maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayafanya mataifa kutegemeana, kumbe hata matumaini yao kwa siku za usoni, yanajikita katika kanuni maadili ya kimataifa. RealAudioMP3

Ni jukumu la Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inadhibiti utengenezaji na matumizi ya silaha za kinyuklia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi kijacho na ulimwengu katika ujumla wake. Madhara ya matumizi ya silaha za kinyuklia linaweza kuwa ni janga la kimataifa na watu wengi wataathirika.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, wakati akichangia kwenye mkutano uliokuwa unajadili kuhusu silaha za kinyukilia, uliokuwa unafanyika mjini Vienna, nchini Austria. Ujumbe wa Vatican unakiri kabisa kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kudhibiti utengenezaji, ulimbikizaji pamoja na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani.

Pamoja na mafanikio haya, bado kuna haja ya kuhakikisha kwamba mazungumzo kuhusu uthibiti wa silaha za kinyuklia yanaendelezwa kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Mahusiano kati ya nchi zinazotengeneza na kumiliki silaha za kinyuklia si mazuri sana na wala hayatoi matumaini ya kuweza kupata suluhu ya kudumu!

Jumuiya ya Kimataifa bado inakabiliwa na changamoto kubwa za athari za mabadiliko ya tabianchi, wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi, vita na kinzani za kisiasa; umaskini pamoja na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; changamoto ambazo kimsingi zinahitaji mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa. Inasikitisha kuona kwamba, bado kuna nchi ambazo zinaendelea kutumia kiasi kikubwa cha bajeti yake kwa ajili ya kununulia silaha, pamoja na kuwekeza katika maboresho ya utengenezaji wa silaha za kinyuklia, hali ambayo inaacha changamoto kubwa kwa ajili ya usalama wa Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu mkuu Silvano Maria Tomasi anasema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kusimama kidete kupinga utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia na badala yake, Jumuiya ya Kimataifa ijikite zaidi katika mchakato wa mfungamano, ushirikiano na mshikamano, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Mtakatifu Yohane XXIII kunako mwaka 1963 aliandika Waraka juu ya Amani Duniani, Pacem in terries, unaowataka wakuu wa Mataifa kujikita katika mchakato utakaosaidia kudumisha misingi ya amani duniani kwa kujikita katika maendeleo ya watu, kwani amani ni jina jipya la maendeleo endelevu, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi kwa kuzingatia: haki, upendo, ukweli na uhuru.

Na Padre Richard A. Mjigwa,
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.