2015-01-03 12:05:02

Msifumbuie macho utumwa na nyanyaso dhidi ya binadamu!


Rais Giorgio Napolitano wa Italia, katika maadhimisho ya Siku ya 48 ya Kuombea Amani Duniani, iliyofanyika hapo tarehe Mosi Januari 2015, amemwandikia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa shukrani, kwa kugusa mifumo mbali mbali inayojitokeza katika utumwa mamboleo, jambo ambalo wakati mwingine linafumbiwa macho; lakini ni matendo yanayo nyanyasa: uhuru, utu na heshima ya binadamu.

Rais Napolitano anasema, changamoto zilizotolewa na Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu "Si tena kama watumwa, bali ndugu", zinapaswa kufanyiwa kazi kama ajenda za masuala na mikakati ya kisiasa kitaifa na kimataifa. Anasema, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo inayoendelea kujionesha katika sura ya dunia inapaswa kushughulikiwa kikamilifu na serikali pamoja na taasisi zinazohusika, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika haki, utu na heshima ya binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kujifunga kibwebwe katika kupambana na uhalifu wa kimataifa, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, unaowatumbukizwa wasichana na wanawake wengi katika biashara ya ukahaba; kazi za suluba bila kusahau madhara yanayosababishwa na rushwa na ufisadi wa mali ya umma.

Rais Napolitano anaungana na Baba Mtakatifu Francisko kuwashukuru watawa na mashirika mbali mbali ya kiraia yanayoendelea kusimama kidete kupinga biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo pamoja na kuwasaidia wahanga wa vitendo hivi ambavyo kimsingi ni uhalifu wa kibinadamu. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, utandawazi unajengeka katika misingi ya haki, mshikamano na udugu pamoja na kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mikakati ya kiuchumi na kisiasa itakayoweza kupunguza pengo kati ya maskini na "akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi"!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.