Kanisa linahitaji "majembe" yaliyoandaliwa barabara!
Mababa wa awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrka walikazia kwa namna ya pekee
umuhimu wa majiundo makini ya Waseminari katika masuala ya kitaalimungu na maisha
ya kiroho; bila kusahau mambo msingi ya makuzi ya kiakili na kiutu ya kila Mseminari.
Mapadre wa baadaye hawana budi kukuza uelewa sahihi wa utamaduni wao bila ya kufungwa
na ukabila au mahali anapotoka mtu.
Ni watu wanaopaswa
kukita maisha yao katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili, ili kuimarisha majitoleo
na sadaka yao kwa Kristo na Kanisa lake. Lazima wajenge na kudumisha uaminifu kwa
Kristo na Kanisa lake kwa njia ya maisha bora ya sala, tafakari ya Neno la Mungu,
Sakramenti za Kanisa, daima wakijitahidi kuwa kweli ni watu wa Mungu wanaotafuta kuishi
katika misingi ya haki, imani, upendo, udumifu na utaratibu. Waseminari hawana budi
kukazia maisha ya kijumuiya, ili kupata majiundo makini yanayozingatia maisha ya mtu
mzima: kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita
katika barua yake kwa Waseminari alikumbusha kwamba, maisha Seminarini ni muda wa
matayarisho kwa maisha na wito wa Kipadre; ni muda wa kujifunza, kufanya maamuzi,
malezi pamoja na makuzi ya kiutu na kiroho, ili hatimaye, waweze kukomaa katika maamuzi
ya maisha yao ya baadaye kama Mapadre. Waseminari wanatakiwa wasiogope kufanya maamuzi
magumu kwa kukumbatia maisha na wito wa Kipadre kwani kuna watu wengi wanawasindikiza
kwa njia ya sala na sadaka zao
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika
ujumbe wake kwa Waseminari kutoka Ufaransa waliokuwa wanafanya hija yao ya maisha
ya kiroho kwenye madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, aliwataka kujikita katika udugu,
sala; maisha na utume wa Kanisa.
Hivi karibuni, Padre Reginald Mrosso, Mkuu
wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu alizundua rasmi Mwaka wa Pili wa
Malezi kwa Majandokasisi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Parokiani
Chibumagwa, Jimbo Katoliki Singida, kwa kuwataka Waseminari hawa kudumisha umoja,
udugu na upendo na kwamba, Familia ya Mungu inawajibika kukuza na kulea miito mitakatifu,
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Waseminari hawa wameanza
mwaka huu wakati Shirika la linajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Jubilee ya Miaka
200 tangu Mtakatifu Gaspar Del Bufalo alipoanzisha Shirika la Wamissionari wa Damu
Azizi ya Yesu. Shirika pia nchini Tanzania liko katika kipindi cha mpito, kuelekea
katika ukomavu kwa kuwa ni Kanda kamili inayojitegemea, changamoto ya kukazia majiundo
makini, ili kweli Shirika liweze kupata majembe ya nguvu katika mchakato wa Uinjilishaji
wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Padre Mrosso amewataka
Waseminari hao kuanza kujizoesha kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari
kujitoa bila ya kujibakiza katika kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha; huku
wakiwa kweli ni vyombo vya haki, amani, furaha na matumaini kwa walimwengu waliojikatia
tamaa kutokana na kumezwa mno na malimwengu. Mwaka huu, Mafrateri walioanza mwaka
wa pili wa malezi ni wanane; hawa ni wale waliohitimu masomo yao ya Falsafa na wako
chini ya uongozi wa Padre Gregory Mkhotya, C.PP.S. Mkuu wa nyumba ya Malezi ya Mtakatifu
Francisko Xsaveri, iliyoko Parokia ya Chibumagwa, Jimbo Katoliki la Singida.