2015-01-02 12:07:33

Wakristo wametikiswa sana huko Mashariki ya Kati, lakini wamebaki "ngangari"


Padre Pierbattista Pizzaballa, Mlinzi mkuu wa Maeneo Matakatifu katika Nchi Takatifu anasema, Wakristo huko Mashariki ya Kati wametikiswa na kujeruhiwa vibaya sana kutokana na misimamo mikali ya kiimani, lakini bado wameendelea kuwa imara na thabiti katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kufanyika huko Mashariki ya Kati vinahatarisha amani, mshikamano na mfungamano wa Jumuiya ya Kimataifa kwa misingi ya kidini.

Vita na mauaji yanayoendelea huko Mashariki ya Kati vina malengo mbali mbali yanayofumbatwa na baadhi ya nchi kutoka Ulaya na kwamba, madhulumu ya kidini dhidi ya Wakristo ni mwendelezo huu, ambao baadhi ya viongozi wakuu wa dini ya Kiislam wameshindwa kukemea wala kulaani, hadi pale ambapo, Chuo kikuu cha Kiislam cha Al Azhar, kilichoko Cairo, Misri kiliposikika kikilaani mauaji ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, kiasi cha watu wengi kushikwa na bumbuwazi!

Baba Mtakatifu Francisko hazungumzii kuhusu vita na machafuko ya kisiasa huko Mashariki ya Kati, jambo ambalo anaendelea kulipatia kipaumbele cha kwanza ni majadiliano ya kidini yanayojikita katika ukweli, haki na mafao ya wengi; kama suluhu ya watu kujenga na kuimarisha amani ya kudumu. Madhulumu na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati zimewaimarisha zaidi badala ya kuogopa, sasa wanaweza kukabiliana na fumbo la kifo kwa macho makavu.

Hii ni changamoto kubwa huko Mashariki ya Kati kuhakikisha kwamba, masuala ya kisiasa kamwe, hayachanganywi na mambo ya kidini, yanayoibua misimamo mikali ya kiimani, kwani watu wamechoshwa na vita, wanataka kuona haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu vinatawala. Licha ya magumu yote haya, bado kuna cheche za matumaini kati ya watu wanaotaka kuona mchakato wa majadiliano ya kidini, kisiasa na kijamii yanaendelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.