Tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Tokeo la Bwana!
Kutokana na sababu za kichungaji, majimbo mengi Barani Afrika yanaadhimisha Siku kuu
ya Tokeo la Bwana, Jumapili tarehe 4 Januari 2015 badala ya tarehe 6 Januari kadiri
ya Kalenda la Liturujia ya Kanisa. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea
tafakari ya Neno la Mungu, Siku kuu ya Epifania ya Bwana.
Ninakuleteeni
kwa furaha ujumbe wa Neno la Mungu tunapoadhimisha Sherehe ya Epifania, yaani Tokeo
la Bwana, ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo terehe 6 Januari katika kipindi
cha Noeli.
Ni sherehe ambayo Mfalme Masiha anajitambulisha wazi kwa ulimwengu.
Ni kwa njia ya nyota, Mamajusi wanaweza kufika mahali alipokuwa na wakaweza kumsujudia
na kumpatia zawadi zao. Kumbe Yesu Kristu Masiha ni nyota inayoangaza na kuongoza
maisha yetu mpaka mwisho wa nyakati hadi kufika mbinguni. Ni nyota inayoongoza historia
ya maisha yetu, historia ya ulimwengu wetu.
Katika somo la kwanza tunaona jambo
la ajabu na zuri likitokea. Nabii Isaya yuko katika ndoto anaona Yerusalemu iliyokuwa
imeharibiwa kwa sababu ya vita na mapigano mbalimbali miaka 600 hivi kabla ya Kristu
sasa inakuwa chanzo cha nuru, na utukufu wa Mungu unaonekana juu yake. Mataifa wakiwakilishwa
na Mamajusi wanaijia nuru hiyo.
Nabii Isaya anaimba akisema “inua macho yako
Yerusalemu utazame pande zote za dunia, wote wanakusanyana; wanakujia wewe” Ni wimbo
wa sifa kwa Yerusalemu, ni kielelezo cha kuzaliwa Masiha na kwamba atakuwa nuru angavu
kwa ulimwengu na mataifa yote watakusanyika kumsujudia na kumtolea zawadi. Habari
na uaguzi huu tunauona vema katika Injili ambapo tunawaona Mamajusi wakitokea pande
zote za dunia kwa ajili ya kuja na kumsujudia Bwana aliyezaliwa na zaidi sana aliye
nyota ya mataifa, nyota ya milele. Kwenye jumuiya zetu kunapotokea tatizo tunaweza
kulitazama kama nabii Isaya? Tutafakari.
Katika somo la pili Mtume Paulo anapowaandikia
Waefeso anawaambia juu ya kufunuliwa siri za Mungu kwa njia ya Mitume. Anasema ni
kwa njia ya Manabii na Mitume na si wanadamu katika vizazi vingine Mungu amefunua
siri yake. Hata hivyo pamoja na kupewa siri hiyo bado mataifa mengine wanashiriki
pamoja nasi ahadi ya Bwana ya kurithi ufalme wake. Hivi Neno la Mungu linatualika
kutambua kuwa sisi sote tuliobatizwa na kupokea mataji matakatifu tumeshirikishwa
katika ukoo wa kikuhani kwa ajili wokovu wetu na wokovu wa ulimwengu.
Katika
Injili tunapata kuona ujumbe wa Neno la Mungu kwa njia ya Mamajusi, wamefika kwa mfalme
Herode na wanamwuliza yuko wapi mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake mashariki
nasi tumekuja kumsujudia. Herode anashangaa kwa kufadhaika na anauliza habari kwa
wakuu wa makuhani na waandishi Kristu azaliwa wapi? Wanamjibu Betlehemu.
Anawaagiza
Mamajusi wakati wakishamwona wamletee habari ili naye akamsujudie! Mamajusi hawa wanaongozwa
na nyota mpaka pale alipo mtoto na hawatarudi kwa Herode kwa sababu Herode anayo nia
ya kutaka kumwua Mwana wa Mungu. Ona kiburi cha mwanadamu badala ya kufurahia kuingia
kwa maisha mapya kwa njia ya mtoto Yesu.
Mamajusi wako katika msingi uleule
wa nabii Isaya anaposema Yerusalemu ikiangaza watu wote watakuja na kumiminika katika
mji. Kumbe Mamajusi wakitimiza ule uaguzi wa nabii Isaya, wanaleta manemane, dhahabu
na uvumba. Mamajusi ni kiwakilishi cha watu wote wanaokubali kuongozwa na ujumbe wa
amani, ujumbe wa Yesu Kristu Masiha yaani nyota, nuru ya ulimwengu. Ni alama ya Kanisa
lililo jumuiya ya watu wenye chimbuko moja yaani Mungu, lakini lugha, tamaduni, umri,
kabila, mashirika na mamlaka tofauti. Watu hawa wote wako mbele ya nyota angavu ndiye
Mkombozi aliyezaliwa.
Mpendwa, unaalikwa basi leo na Neno la Mungu kujiweka
chini ya maongozi ya Nyota angavu, nyota ya milele ndani ya Kanisa familia ya Mungu.
Ninakutakieni heri na baraka za Mungu, ukazidi kuongozwa na Kristu mwenyewe, daima
ukampe hazina stahili kama Mamajusi kwa sifa na utukufu wa Mungu na pia kwa wokovu
wako.
Heri na baraka kwa wale walio na majina ya Epifania na majina ya Mamajusi
yaani Gaspar, Melkiori na Barthazari. Mkakomae katika kusujudu na kumtolea Mungu vipaji
vyenu kama kielelezo cha kuongozwa naye katika maisha yenu. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.