Umoja wa wanavyuo wa Kanisa Katoliki (Tanzania Movement Of Catholic Students – TMCS),
wamesema wanakubaliana na mafundisho ya Kanisa katika uzazi salama kwa kutumia njia
za asili badala ya kukumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za uzuiaji
na utoaji mimba, mambo ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu
na chanzo cha kutoweka kwa amani na utulivu. Vijana wanapaswa kujengewa uwezo wa kusimama
kidete kutangaza Injili ya Familia kwa kujikita katika maadili na utu wema!
Mratibu
wa TMCS Mathias Kabyemela, alitoa kauli hiyo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu mafunzo
ya siku tatu wa wanachama 210 wa TMCS waliokuwa wamekutanika hivi karibuni katika
ukumbi wa St. Claver nje kidogo ya mji wa Dodoma. Kabyemela alisema umoja wao unaamini
na utaendelea kuamini kuwa njia za asili ndizo zinazofaa kwa vijana wa Kitanzania
katika kupanga uzazi kuliko kutumia njia za kisasa ikiwemo sindano za kuzuia mimba.
Alisema
Umoja wao ambao unaunganisha vyuo vya kati na vyuo vikuu 103 nchini Tanzania, umekuwa
ukifanya kazi ya kutoa elimu kwa vijana wasomi ambao nao hutumia nafasi zao kutoa
elimu kwa vijana wenzao mara warudipo vijijini na katika makazi yao. “Huu kwetu ni
mkutano wa sita ingawa TMCS inatimiza miaka 30 sasa, lakini bado tunaunga mkono msimamo
wa Kanisa katika suala zima la kupanga uzazi tukijua kuwa kutumia kalenda ndyo njia
sahihi zaidi kuliko vitu vingine,” alisema Kabyemela.
Kuhusu umoja huo alisema
umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuwaunganisha vijana wa Tanzania na nje ambao
wanafanya kazi ya kuinjilisha kwa ushirikiano mkubwa. Nchini Tanzania alisema wameganya
uongozi wa umoja huo katika kanda 14 ambazo wanaziita ni majimbo na maeneo hayo yana
uongozi kwa kila chuo kwa ajili ya uwakilisha jambo linalofanya huduma yoa kuwa nyepesi
zaidi.
Akitoa mada katika warsha hiyo, Padri Aman Nyoni, aliwataka vijana kujitambua
na kutumia nafasi walizonazo kuwaelimisha wenzao ambao hawakubahatika kupata elimu
ya kutosha kuhusiana na Injili ya Uhai, ili waweze kusimama kidete, kulinda, kutetea
na kuendeleza Injili ya Uhai kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao adili na manyofu yanayosimikwa
katika dhamiri nyofu, Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa.
Padre Nyoni alisema
suala la usiri ndilo ambalo linawapelekea wasichana wengi wengi kujikuta wakitumbukia
katika ujauzito kwani wanakuwa hawana elimu ya kutosha kuhusu maisha na maumbile yao.
Naye
mlezi wa Umoja huo kwa kanda ya Tabora ambaye pia alikuwa akikaimu nafasi ya ulezi
taifa katika mkutano huo Padri Josephat Mande, alitaja lengo la mikutano hiyo ni kuwafunda
vijana katika Uinjilishaji katika nyakati hizi za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo
ya teknolojia, ili vijana waweze kuwa macho na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu,
kwani huko watakiona cha mtema kuni!