Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inakuletea salam za Mwaka Mpya 2015 kutoka kwa
Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, kwa watanzania, alizozitoa hapo tarehe 31 Desemba
2014.
Ndugu zangu; Watanzania Wenzangu; Kama ilivyo ada imefikia siku
ya kuuaga mwaka mmoja na kuukaribisha mwaka mwingine. Leo tunauaga mwaka 2014 na kuukaribisha
mwaka mpya wa 2015. Tunamshukuru Muumba wetu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima
na kutuwezesha kuifikia siku ya leo. Kwa ndugu na jamaa zetu ambao hawakujaliwa kuiona
siku ya leo tuzidi kuwaombea mapumziko mema. Nasi tumuombe Mwenyezi Mungu, mwingi
wa rehema atujaalie umri mrefu, afya njema na mafanikio tele kwa kila tuliombalo katika
mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ndugu wananchi; Hizi ni salamu zangu za mwisho
za mwaka mpya kutoa nikiwa Rais wa nchi yetu. Mwakani salamu kama hizi zitatolewa
na Rais wetu mpya. Mimi wakati huo nitakuwa raia wa kawaida kijijini kwangu Msoga
nikifuatilia kwenye TV na radio hotuba ya Rais wa Awamu ya Tano ya uongozi wa nchi
yetu akitoa salamu zake za kwanza za mwaka mpya, itakuwa siku ya furaha na faraja
kubwa kwangu.
Hali ya Usalama Ndugu Wananchi; Tunaumaliza mwaka
2014 kwa salama na amani. Mipaka yetu iko salama na hakuna tishio lolote la kiusalama
kutoka ndani au nje ya nchi yetu. Uhusiano wetu na nchi jirani na nyinginezo duniani
ni mzuri. Hakuna nchi iliyo adui au tunayoitilia shaka kuwa na njama za kuhatarisha
usalama wa Tanzania. Nawapongeza wanadiplomasia wetu pamoja na viongozi na watendaji
wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya nchi yetu kuwa salama.
Uhalifu
Unapungua Ndugu Wananchi; Taarifa za Polisi zinaonyesha kuwa, mwaka 2014
vitendo vya uhalifu vimepungua ikilinganishwa na mwaka 2013. Mwaka huu, matukio ya
uhalifu yaliyoripotiwa Polisi yalikuwa 64,088 ikilinganishwa na matukio 66,906 katika
mwaka 2013. Haya ni matokeo ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi wakishirikiana
na vyombo vingine vya usalama pamoja na raia wema. Naomba ushirikiano huu uendelee
mwaka ujao na miaka ijayo ili tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi.
Ajali
za Barabarani Ndugu Wananchi; Nimefarijika kusikia pia kuwa matukio ya ajali
za barabarani nchini nayo yanaendelea kupungua. Mwaka huu kumetokea ajali 14,048zilizosababisha
vifo vya watu 3,534 na wengine 16,166 kujeruhiwa. Mwaka 2013 kulitokea ajali 22,383zilizosababisha
vifo 3,746 na majeruhi 19,433. Hivyo mwaka huu kulikuwa na ajali 8,335, vifo 212 na
majeruhi 3,267pungufu kuliko mwaka jana. Huu ni mwelekeo mzuri na wa kutia moyo ingawa
bado ni nyingi mno. Naomba yale tuliyoyafanya yaliyotuwezesha kupata unafuu huu mwaka
huu yaendelezwe maradufu mwaka 2015 na miaka ijayo.
Ugaidi Ndugu
Wananchi; Mwaka huu tumefanikiwa kutambua mtandao wa viongozi na washirika wao
wanaotuhumiwa kupanga na kufanya mashambulizi ya kigaidi kwa kutumia mabomu na kumwagia
watu tindikali Tanzania Bara na Zanzibar. Watu 112 wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo
vya ugaidi wametiwa nguvuni. Tayari watuhumiwa 87 kati yao wameshafikishwa mahakamani
na waliosalia watafikishwa wakati wo wote. Uchunguzi unaendelea ili kuwatambua wahusika
wengine ambao hawajakamatwa.
Ndugu wananchi; Kwa niaba ya Watanzania wenzangu
wote, natoa pongezi nyingi kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kazi nzuri waliyofanya
ya kutambua mtandao wa ugaidi nchini na kuchukua hatua thabiti za kuudhibiti. Hali
kadhalika nawashukuru raia wema waliotoa taarifa zilizowezesha haya kufanyika. Hatupaswi
kubweteka wala kudhani kuwa mambo yamekwisha. Lazima tuendelee kuchukua tahadhari
muda wote kwani hatujui adui anapanga kufanya hujuma gani, lini na wapi.
Dawa
za Kulevya Ndugu Wananchi; Tumeendelea kupata mafanikio ya kutia moyo katika
vita dhidi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini. Mwaka huu watuhumiwa
935 wakiwemo vigogo wa biashara hii haramu duniani wamekamatwa. Jumla ya kesi 19 zimefunguliwa
Mahakamani. Aidha, kiasi cha kilo 400 za heroine, kilo 45za cocaine na kilo 81,318
za bangi zimekamatwa. Narudia kutoa pongezi nyingi kwa Kikosi Kazi Maalum cha Kukabiliana
na dawa za kulevya nchini kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana. Matunda ya kazi
yao tunayaona. Naomba juhudi ziongezwe maradufu mwaka ujao na miaka ijayo. Serikali
itaendelea kuwaunga mkono.
Ndugu wananchi; Kama nilivyoahidi mwaka jana,
Muswada wa Sheria ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya umeshasomwa kwa mara
ya kwanza katika Mkutano wa Novemba, 2014 wa Bunge letu tukufu. Pamoja na kupendekeza
kuongeza adhabu kwa makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, Muswada huo pia unapendekeza
kuanzisha chombo kipya chenye nguvu cha kuzuia na kupambana na dawa za kulevya. Muswada
huu ukipitishwa na kuwa Sheria tutakuwa tumeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya biashara
na matumizi ya dawa za kulevya nchini.
Ujangili wa Wanyamapori Ndugu
Wananchi; Katika mwaka tunaomaliza leo mapambano dhidi ya ujangili na biashara
haramu ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori yameimarishwa. Kwa ujumla kasi ya ujangili
imeendelea kupungua. Katika mwaka 2014 ndovu114 waliuawa ikilinganishwa na ndovu219
waliouawa mwaka 2013 au ndovu 473 mwaka 2012. Aidha, majangili 1,354 wamekamatwa na
pembe za ndovu 542 na silaha mbalimbali 184 nazo zilikamatwa. Naamini uamuzi wa kuifanya
Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa Wakala yaani Tanzania
Wildlife Agency (TAWA) kutaongeza nguvu ya kuhifadhi wanyama pori na mapambano dhidi
ya ujangili.
Natoa pongezi nyingi kwa askari wa wanyamapori, Jeshi la Polisi
na vyombo vingine vya Serikali na raia wema kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya na
mafanikio yanayoendelea kupatikana. Juhudi za kupambana na ujangili na biashara haramu
ya bidhaa zinazotokana na wanyama pori zitaendelezwa kwa nguvu zaidi mwaka ujao 2015
na miaka inayofuatia. Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati marafiki zetu
wa maendeleo wanaotuunga mkono kwa hali na mali katika mapambano haya. Naomba waendelee
kutusaidia.
Hali ya Uchumi Jumla Ndugu wananchi; Mwaka 2014 ulikuwa
mzuri kwa uchumi wa taifa. Uzalishaji katika sekta nyingi ulikuwa ni mzuri. Ndiyo
maana tunategemea kuwa tutafikia au hata kuvuka lengo tulilojiwekea la pato la taifa
kukua kwa asilimia 7.4 mwaka huu. Mwaka 2013 pato la taifa lilikua kwa asilimia 7.3.
Mfumuko wa bei uliendelea kushuka na kufikia asilimia 5.8 Novemba, 2014 ukilinganisha
na Januari 2014 ulipokuwa asilimia 6.0. Hali nzuri ya upatikanaji wa chakula nchini
imesaidia sana kufanya mfumuko wa bei kuendelea kushuka. Ni matumaini yangu kuwa mfumuko
wa bei utaendelea kushuka na kufikia asilimia 5 ifikapo Juni, 2015.
Mauzo
Nje Ndugu Wananchi; Mauzo nje yameendelea kuongezeka. Katika kipindi kilichoishia
Oktoba 31, 2014, Tanzania iliuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya dola za Marekani
milioni 8,503.9 ukilinganisha na mauzo ya dola milioni 8,332.5 katika kipindi kama
hicho mwaka 2013. Mapato yetu yangekuwa makubwa zaidi kama bei za kahawa, chai, korosho
na pamba zisingeanguka au bei ya dhahabu nayo isingepada.
Akiba ya Fedha
za Kigeni Ndugu Wananchi; Akiba yetu ya fedha za kigeni ilikuwa Dola za
Marekani milioni 4,251.8 kwa kipindi kilichoishia Novemba 30, 2014. Kiasi hicho kinatuwezesha
kuagiza bidhaa toka nje kwa miezi 4.1.Hii ni chini ya lengo letu la kuwa na akiba
ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa kwa miezi minne na nusu. Hata hivyo, sina wasiwasi
kabisa kwamba tofauti hii ndogo tutaweza kuiziba mwaka 2015.
Mapato ya
Serikali Ndugu Wananchi; Makusanyo ya mapato ya Serikali kwa mwezi, kati
ya Julai hadi Novemba, 2014 yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 3,555.5 kipindi kama
hicho mwaka 2013 hadi shilingi bilioni 3,924.1 mwaka huu. Hata hivyo, makusanyo hayo
yalikuwa asilimia 90 ya lengo tulilojiwekea la kukusanya shilingi bilioni 4,459.7.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mapato, zipo sababu mbalimbali zilizosababisha lengo lisifikiwe
katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2014/2015. Hatua zipasazo zinaendelea kuchukuliwa
kurekebisha mambo hayo ili katika nusu ya pili ya mwaka huu wa fedha makusanyo yafikie
lengo na ikiwezekana yazidi ili kufidia pengo la nusu ya kwanza.
Takwimu
Mpya za Pato la Taifa Ndugu wananchi, Ni utaratibu wa kawaida wa nchi zote
duniani kuwa na mwaka unaotumika kuwa kizio (base year) cha kukokotoa takwimu za Pato
la Taifa. Ni utaratibu wa kawaida pia kwa kila baada ya muda fulani mwaka wa kizio
hubadilishwa. Lengo ni kuboresha takwimu husika. Katika marekebisho hayo pia huingizwa
thamani ya bidhaa na huduma mpya katika pato la taifa na kuziondoa zilizotoweka ili
kutoa picha halisi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Katika miaka ya hivi
karibuni nchi za Ghana (mwaka 2010), Nigeria (mwaka 2013) na Kenya (mwaka 2014) wamefanya
marekebisho ya takwimu zao za pato la taifa. Na sisi Tanzania tumefanya hivyo mwaka
huu (2014). Hii ni mara ya tano kwa nchi yetu kurekebisha takwimu za pato la taifa.
Mara nne zilizopita ilikuwa mwaka 1966, 1976, 1992 na 2001.
Ndugu wananchi; Ofisi
ya Taifa ya Takwimu imekamilisha marekebisho ya takwimu za pato la taifa na kukokotoa
takwimu mpya kwa kutumia mwaka 2007 kama mwaka wa kizio. Kutokana na marekebisho yaliyofanyika,
pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 70 kwa kutumia bei za mwaka 2007.
Ukitumia bei za mwaka 2001, pato la taifa kwa mwaka 2013 ni shilingi trilioni 53.17.
Kuongezeka kwa pato la taifa kumeongeza pia pato la wastani la kila Mtanzania kutoka
shilingi 1,186,200 (sawa na US$ 742) kwa bei za mwaka 2001 hadi shilingi 1,560,050
(sawa na US$ 977) kwa bei za mwaka 2007.
Kilimo na Chakula Ndugu
Wananchi; Mwaka 2014 ulikuwa mzuri sana kwa uzalishaji wa mazao ya chakula nchini.
Uzalishaji ulikuwa tani milioni 16.02 ukilinganisha na uzalishaji wa tani milioni
14.38mwaka wa jana 2013. Hili ni ongezeko la tani milioni 1.64. Kwa mujibu wa mahitaji
yetu ya chakula nchini kuna ziada ya tani milioni 3.25. Katika ziada hiyo, mahindi
yanachangia tani milioni 1.55, mchele tani 794,000 na kiasi kinachobakia kinachangiwa
na mazao mengine ya chakula.
Ndugu wananchi; Kuna jambo moja muhimu kuhusu
ununuzi wa nafaka ambalo ningependa kulifafanua. Naomba ieleweke kuwa Wakala wa Taifa
wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) sio mnunuzi wa mahindi yote, mpunga wote na mtama wote
unaozalishwa na wakulima nchini. Wakala hununua sehemu ndogo tu ya nafaka ya ziada
iliyozalishwa na hununua kwa ajili ya kuweka akiba ya taifa ya chakula cha kutumika
wakati wa dharura ya watu kupata tatizo la njaa. Aidha, Wakala hununua kiasi kinacholingana
na uwezo wa maghala yake kuhifadhi. Kwa sasa uwezo wa maghala yetu ni kuhifadhi tani
246,000 ingawaje tunaendelea kujenga maghala mengine mpaka tufikie uwezo wa kuhifadhi
tani 400,000 ifikapo 2015. Hivyo basi kwa Wakala kununua tani 292,415.41 mwaka huu
ina maana kwamba kiasi cha karibu tani 50,000 zinahifadhiwa nje ya maghala kwa kutumia
maturubai. Huu siyo utaratibu mzuri na haifai kuendelea nao kwani kuna hatari ya nafaka
hiyo kuharibika na kuzua mgogoro mkubwa siku moja.
Ndugu wananchi; Baada
ya NFRA kununua tani 292,415.41 kuna takribani tanimilioni 2.96 za nafaka ya ziada
ambayo iliyobaki mikononi mwa wakulima. Mategemeo yetu ni kuwa wafanyabiashara wetu
watanunua nafaka hiyo kwa ajili ya kuuza mijini na kwingineko inakohitajika. Bahati
mbaya mwaka huu kama ilivyokuwa mwaka wa jana, wafanyabiashara wetu hawakuweza kununua
nafaka yote ya ziada ambayo Serikali haikuweza kununua kupitia Wakala wa Taifa wa
Hifadhi ya Chakula. Hali hii imezua tatizo ambalo Serikali kwa kushirikiana na wafanyabiashara
nchini hatuna budi kulitafutia majawabu. Tunalazimika kutafuta masoko mengine ndani
na hata nje ya nchi ya kuuza mahindi, mpunga na mtama wa ziada. Nimeagiza Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kukaa chini na kushirikiana
na wafanyabiashara kulitafutia ufumbuzi suala hili lenye maslahi makubwa kwa wakulima
na nchi yetu kwa jumla.
Ndugu Wananchi; Katika mazingira haya, ninapopata
taarifa ya kuwepo watu wanaotaka kuuza mahindi nje ya nchi lakini wanawekewa vikwazo
na maafisa wa Serikali inanishangaza na kunisikitisha. Nawataka wale wote wanaofanya
hivyo waache mara moja na badala yake wawasaidie wafanyabiashara hao kufanikisha azma
yao. Hali kadhalika, tuwashawishi watu wengine nao wajitokeze kufanya biashara hiyo.
Jambo muhimu ninalopenda kulisisitiza ni kwamba pawepo na utaratibu mzuri ili biashara
hiyo ifanywe kwa kutumia njia halali na zilizo wazi. Kutumia njia za panya hakukubaliki
na wala hakuna sababu ya kufanya hivyo.
Miradi ya Kimkakati Ndugu
wananchi; Katika mwaka 2014 utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kwa mujibu
wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 – 2015/16) umeendelea vizuri. Tunayo
matumaini makubwa kwamba katika mwaka 2015 miradi mingi itakamilika.
Tuanze
na Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam.
Mradi huu unategemewa kukamilika Januari, 2015. Utakapokamilika utatuwezesha kutimiza
lengo letu la kuzalisha MW 2,780 za umeme ifikapo 2016. Mipango ya kupata ardhi ya
ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asili kuwa ya kumiminika (LNG) ili iweze kusafirishwa
kwenda kwenye masoko, inakwenda vizuri.
Ndugu Wananchi; Utekelezaji wa
mradi mkubwa wa kimkakati wa kusambaza umeme vijijini umeendelea vizuri na tumepata
mafanikio makubwa yasiyokuwa na mfano wake katika historia ya nchi yetu. Hadi kufikia
Novemba, 2014, jumla ya vijiji 3,836 vimepatiwa umeme na vingine 1,500 vinategemewa
kupatiwa umeme ifikapo Juni, 2015. Hivyo basi, vijiji 5,336 kati ya vijiji 12,423
vya Tanzania Bara vitakuwa vimepatiwa umeme. Hii ni sawa na asilimia 43 ya vijiji
vyote nchini vitavyokuwa vimepata umeme. Hivi sasa wananchi milioni 17.3 nchi nzima
sawa asilimia 36 wamefikiwa na huduma ya umeme ikilinganishwa na watu milioni 8.1
sawa na asilimia 18.4 waliokuwa wamefikiwa na huduma hiyo mwaka 2012. Mwaka 2015 tunatarajia
watu milioni 18.2 sawa na asilimia 38 watafikiwa na umeme. Kwa upande wa vijijini
mwaka 2012 watu milioni 2.3 sawa na asilimia 7 walikuwa na umeme. Ifikapo Juni 2015,
idadi hiyo itaongezeka na kuwa milioni 7.4 sawa na asilimia 21. Haya ni mafanikio
makubwa kwa wananchi wengi vijijini na mijini kupata umeme katika kipindi kifupi kiasi
hiki. Ni mageuzi ya aina yake yatokayotoa mchango muhimu katika kuinua hali za maisha
ya Watanzania. Ndugu Wananchi;
Tunaanza kuiona nuru ya matumaini kwamba
siku si nyingi kutoka sasa, makaa ya mawe ya Mchuchuma na madini ya chuma ya Liganga
yataweza kutumika kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wa Ludewa. Maandalizi yote muhimu
yamekamilika kwa ajili ya Januari, 2015 kuanza ujenzi wa mgodi wa makaa ya mawe kule
Mchuchuma, mtambo wa kufua umeme, ujenzi wa mgodi wa chuma kisichoyeyushwa pale Liganga
na ujenzi wa kiwanda cha kuyeyusha chuma.
Natoa pongezi maalum kwa Shirika
la Maendeleo la Taifa (NDC) na wabia wenzao, Kampuni ya Sichuan Hongda ya China kwa
hatua iliyofikiwa. Inakadiriwa kuwa miradi hii ikikamilika itatoa ajira 33,000 za
moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja.
Ndugu Wananchi; Mradi mwingine
mkubwa wa kimkakati ni ule wa kujenga Eneo Maalumu la Kiuchumi (Special Economic Zone)
la Mbegani, Bagamoyo. Kwa mujibu wa mpango kazi wa wabia wa mradi huo yaani Mamlaka
ya Kuendeleza Maeneo huru ya Uwekezaji (EPZA), Kampuni ya China Merchants Holdings
International na Mfuko wa Uhifadhi wa Akiba ya Mali za Serikali ya Oman (Oman State
General Reserve Fund), ujenzi wa bandari na miundombinu mingine itakayowezesha viwanda
kujengwa imepangwa kuanza Julai 2015.
Miundombinu ya Usafiri na Uchukuzi Ndugu
Wananchi; Katika mwaka huu wa 2014 kazi ya kujenga barabara za lami na kuimarisha
barabara za udongo ili ziweze kupitika wakati wote ziliendelea kote nchini. Huu nao
ni mradi mkubwa wa kimkakati. Barabara za lami 19 zenye urefu wa kilometa1,459 zimekamilika
kujengwa mwaka huu katika Mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Kagera, Dar es Salaam, Dodoma,
Tanga, Morogoro, Arusha, Tabora na Shinyanga. Ujenzi unaendelea kwa barabara nyingine
24 katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Kilimanjaro, Rukwa, Simiyu, Katavi, Tabora,
Mwanza, Dar es Salaam, Kagera na Pwani ambazo wakati wo wote mwaka 2015 zitakamilika.
Maandalizi ya kuanza ujenzi wa barabara nyingine nane yanaendelea vizuri sehemu mbalimbali
nchini.
Kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara, tumeendelea kufanya kazi ya
ujenzi na ukarabati wa barabara za udongo kote nchini. Mwaka huu Mfuko huo umetengewa
shilingi bilioni 751.7 ukilinganisha nashilingi bilioni 504.4 mwaka jana. Aidha, mwaka
huu tumeweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la Mto Kilombero. Matumini yetu ni
kuwa ujenzi wa daraja hilo na Daraja la Kigamboni utakamilika mwaka 2015. Ujenzi wa
Daraja la Malagarasi ulishakamilika mwaka jana, kinachosubiriwa ni sherehe ya uzinduzi.
Kwa upande wa jiji la Dar es Salaam, tunategemea kukamilisha ujenzi wa Awamu
ya Kwanza ya barabara za mabasi yaendayo kasi. Ni matarajio yetu pia kwamba mabasi
yataanza kusafirisha abiria katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2015. Halikadhalika,
tunategemea katika mwaka 2015 ujenzi utaanza wa barabara zinazozunguka jiji la Dar
es Salaam (ring roads), barabara ya Mwenge - Morocco na ile ipitayo juu ya nyingine
(flyovers) eneo la TAZARA. Vile vile, daraja jipya la Salenda litaanza kujengwa. Aidha,
kivuko cha abiria 300 cha MV Dar es Salaam kitaanza kusafirisha abiria kati ya Dar
es Salaam Kaskazini na Ferry mapema mwakani. Hatua zote hizi zinalenga kupunguza msongamano
wa magari katika jiji la Dar es Salaam.
Usafiri wa Anga na Reli Ndugu
wananchi; Jitihada za kuboresha huduma ya usafiri katika Reli ya Kati zimeendelea
kwa mafanikio. Mwaka huu vichwa vinane vya treni vimekarabatiwa, mabehewa mapya 22
ya abiria na mabehewa 274ya mzigo yamenunuliwa. Mabehewa hayo yameanza kuwasili nchini
kati ya Novemba na Desemba mwaka huu. Kati ya Januari na Mei, 2015 tunatarajia kupokea
vichwa vipya vya treni 13. Uboreshaji huu wa huduma za treni unakwenda sambamba na
ukarabati wa reli yenyewe, ujenzi wa madaraja na kuimarisha maeneo yaliyo korofi katika
reli hiyo.
Kuhusu ujenzi wa reli iliyo pana zaidi (standard guage), yenye
uwezo wa kubeba mabehewa mengi na kuwezesha treni kwenda kwa mwendo wa kasi zaidi,
juhudi za kutafuta fedha za ujenzi au wabia wa kushirikiana nasi kujenga zinaendelea.
Wakati huo huo, tunaendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi kwa matatizo ya reli ya
TAZARA ili mambo yaende vizuri. Tutashirikiana kwa karibu na wabia wenzetu wa Zambia.
Bahati nzuri Serikali ya China iko tayari kuunga mkono juhudi zetu za kufufua reli
ya TAZARA.
Usafiri wa Anga Ndugu Wananchi; Sekta ya usafiri wa
anga imeendelea kukua katika mwaka 2014. Idadi ya abiria wanaowasili na kutoka katika
viwanja vyetu vya ndege nchini imeongezeka kutoka abiria milioni 2.5 mwaka 2013 hadi
abiria milioni 3.5 kufikia Septemba, 2014. Safari za ndege kati ya Tanzania na nchi
za nje zimeongezeka kutoka 274Januari, 2013 hadi 295 kufikia Septemba, 2014. Hili
ni ongezeko la asilimia 8. Safari za ndege ndani ya nchi nazo zimeongezeka kutoka
safari 230,458mwaka 2013 hadi safari 241,922 mwaka 2014. Hii ni sawa na ongezeko la
asilimia 39. Maongezeko haya ni kielelezo na ushahidi kuwa shughuli za utalii na biashara
nchini zimeendelea kukua. Ndugu Wananchi; Ujenzi wa Jengo la 3 (Terminal 3)
la Abiria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere unaendelea vizuri.
Jengo hilo litakapokamilika mwakani, litakuwa na uwezo wa kuhudumia wastani wa abiria
milioni 8 kwa mwaka. Aidha, ukarabati wa Jengo la 2 (Terminal 2) utafanyika ili liweze
kutoa huduma iliyo bora zaidi. Sambamba na ujenzi huo, Wakala wa Viwanja vya Ndege
wameendelea kukarabati na kuboresha viwanja vya ndege vya KIA, Mwanza, Songwe, Bukoba,
Tabora na Kigoma. Tunatarajia ukarabati wa viwanja vya ndege vya Shinyanga na Sumbawanga
kuanza mapema mwaka 2015.
Elimu Ndugu wananchi; Tumeendelea kupiga
hatua za kuridhisha katika kuboresha elimu nchini. Tumefanikiwa kupunguza tatizo la
upungufu wa maabara, vitabu na walimu wa shule za msingi na sekondari. Mwaka huu tumeajiri
walimu 36,339 kati ya 81,562 wanaohitajika. Tumebakiwa na upungufu wa walimu 45,223
yaani 26,946 wa shule za msingi na 18,277 wa shule za sekondari hususan wa masomo
ya sayansi. Hivi sasa hatuna tatizo la walimu wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari.
Mwaka
huu tumeanza mpango maalumu wa kutoa mafunzo ya Diploma ya Ualimu kwa masomo ya sayansi
na hisabati katika Chuo Kikuu cha Dodoma ambapo jumla ya wanafunzi 5,602 wa masomo
hayo wamedahiliwa. Mpango huu utatuwezesha kupunguza pengo kubwa tulilonalo la walimu
wa sayansi katika muda mfupi zaidi.
Ujenzi wa Maabara Ndugu wananchi; Ujenzi
wa maabara za Fizikia, Kemia na Baiolojia katika shule za sekondari za Kata 3,463
umekwenda vizuri kiasi. Kwa idadi hiyo ya shule inatakiwa zijengwe maabara 10,389
ilipofika Novemba, 2014. Taarifa kutoka TAMISEMI zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba
29, 2014, maabara 4,207 sawa na asilimia 40.5 zilikuwa zimekamilika, maabara 5,688
sawa na asilimia 54.8 zilikuwa katika hatua mbalimbali za ukamilishwaji, na maabara
494 sawa na asilimia 4. zilikuwa katika hatua za awali za ujenzi.
Ndugu Wananchi; Natoa
pongezi nyingi kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti na Wakurugenzi Watendaji
wa Halmashauri za Wilaya na Miji nchini pamoja na wananchi, kwa jitihada kubwa iliyofanyika.
Kwa kutambua jitihada hizo, nimeongeza miezi sita zaidi kwa wale ambao hawajakamilisha
ujenzi wa maabara hizo wafanye hivyo. Sikusudii kuongeza tena muda baada ya hapo.
Naomba watumie kipindi hicho kitumike kutafuta vifaa vya maabara. Serikali itasaidia
upatikanaji wa watunza maabara (laboratory technicians) ambao tumeanza programu kubwa
ya mafunzo yao na mahitaji mengine ya maabara.
Ununuzi wa Vitabu Ndugu
Wananchi; Tumeendelea kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu na vifaa vya kufundishia
katika shule za msingi na sekondari. Tumekuwa tunanunua vitabu kwa kutumia Bajeti
ya Serikali na misaada kutoka kwa marafiki zetu wa maendeleo. Kwa mfano, Serikali
ya Marekani imetupatia vitabumilioni 2.5 vya masomo ya sayansi na hisabati kwa shule
za sekondari. Ongezeko hili la vitabu linashusha uwiano uliopo sasa wa kitabu kimoja
kwa wanafunzi wanne na kufikia kitabu kimojakwa wanafunzi wawili. Lengo letu ni kila
mtoto kuwa na kitabu chake kwa kila somo ifikapo mwaka 2016.
Sera Mpya ya
Elimu na Mafunzo Ndugu wananchi; Mafanikio mengine tuliyopata mwaka huu
ni kukamilika kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Hii ni hatua muhimu sana
katika maendeleo ya elimu nchini hakuna badala yake. Sera mpya inalenga kuinua ubora
wa elimu na mafunzo na kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha Watanzania wengi
zaidi kupata fursa za elimu iliyo bora na inayolinga na wakati tulionao. Jambo jipya
sana na la kihistoria katika Sera mpya ya Elimu ni dhamira ya Serikali ya kuondoa
ada katika elimu ya sekondari kuanzia mwaka 2016. Mpaka sasa hatuna ada kwenye shule
za msingi, sasa wakati umefika kufanya hivyo pia kwa elimu ya sekondari. Kwa mujibu
wa maelezo hayo ya Sera, nimekwishatoa maagizo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Fedha na Tume ya Mipango
kuanza kutafakari namna jambo hilo litakavyotekelezwa.
Afya Ndugu
Wananchi; Katika mwaka 2014 jitihada za kuboresha huduma ya afya kwa Watanzania
ziliendelea. Tulipambana kwa mafanikio na mlipuko wa homa ya dengue iliyowapata watu
1,039 na kusababisha vifo vya watu 3 kati yao. Kwa upande wa maradhi ya ebola tumejiandaa
vya kutosha kutambua watu wenye maradhi hayo wanapoingia nchini kupitia viwanja vya
ndege vya kimataifa na vituo vyote vya mpakani. Aidha, tumejipanga vyema kuwahudumia
wagonjwa wa maradhi hayo iwapo watatokea.
Mwaka huu pia, Madaktari wetu watano
wamekwenda Liberia kusaidiana na ndugu zetu wa huko katika kukabiliana na ugonjwa
wa ebola. Madaktari wetu hao wako salama na wanaendelea vizuri kutoa huduma. Madaktari
hao watakaporejea nchini watakuwa hazina kubwa ya taifa katika kupanga mipango ya
kukabiliana na ugonjwa huu hatari. Hali kadhalika, watakuwa viongozi wa wengine katika
kutibu wagonjwa wa maradhi ya ebola iwapo watatokea nchini.
Ndugu Wananchi; Katika
kipindi cha Januari hadi Desemba, 2014, tumeweza kuajiri watumishi wa sekta ya afya
8,345 ambao kati yao kuna madaktari 244, madaktari bingwa 75, wauguzi 2,555 na wataalamu
wa kada nyingine za afya 5,471. Mwaka huu pia tumefanikiwa kuongeza udahili wa wanafunzi
kutoka wanafunzi 7,956 katika mwaka 2012/2013 hadi wanafunzi 9,730. Kwa ongezeko hilo,
sasa tumefikia asilimia 97 ya lengo letu la kudahili wanafunzi 10,000ifikapo mwaka
2017.
Jitihada zetu za kuongeza fursa za mafunzo kwa Madaktari, Wauguzi na
wataalamu wengine wa afya zina muelekeo mzuri. Ujenzi wa hospitali ya kufundishia
pale Mloganzila unaendelea vizuri na hospitali ya kufundishia ya Chuo Kikuu cha Dodoma
umekamilika. Ni matarajio yangu kuwa wakati wo wote mwakani ujenzi wa kampasi mpya
ya Chuo Kikuu cha Muhimbili pale Mloganzila utaanza. Ujenzi huo ukikamilika Chuo kikuu
cha Muhimbili kitaweza kudahili wanafunzi 12,000 kutoka wanafunzi 2,500 wa sasa jambo
ambalo litafanya upungufu wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wa Afya kupata jawabu
la uhakika. Tumeendelea kufanya mambo mengine ikiwemo ujenzi wa jengo la tiba za ubongo
na mishipa ambalo limekamilika pale Muhimbili, sasa tunahangaikia kupata vifaa.
Maji Ndugu
Wananchi; Katika mwaka huu wa 2014 tumeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya
kuwapatia wananchi maji safi na salama mijini na vijijini. Kwa ajili hiyo miradi 498
ya maji vijijini imekamilika na miradi 740 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Miradi mingine378 ipo katika maandalizi ya ujenzi kuanza. Ni matarajio yetu kwamba
katika mwaka ujao wa 2015, miradi mingine 731itatekelezwa na vituo 25,790 vya kuchota
maji vitajengwa. Miradi hii ikikamilika tutaweza kuwafikia asilimia 71 ya wananchi
wanaopata maji safi na salama vijijini kutoka asilimia 58 ya sasa. Kwa ajili hiyo,
tutakuwa tumevuka lengo tulilojiwekea la kuwapatia watu maji asilimia 65 ya Watanzania
waishio vijijini ifikapo 2015. Ombi langu kwa ndugu zetu wa Hazina waiangalie sekta
hii ya maji kwa ukaribu zaidi na wawapatie fedha kwa wakati.
Ndugu Wananchi; Utekelezaji
wa mradi wa kuipatia maji miji ya Mwanga – Same – Mkomazi pamoja na miji na vijiji
vyote vya njiani, utaanza Februari, 2015. Fedha zimekwishapatikana na Mkandarasi wa
Awamu ya Kwanza ameshapatikana. Makandarasi wa Awamu ya Pili na Tatu watapatikana
muda si mrefu kutoka sasa. Hii pia itahusu kupata Mkandarasi wa mradi wa maji wa mji
wa Orkesment.
Ndugu Wananchi; Mwaka huu miradi ya kuipatia maji miji kadhaa
nchini ilikamilika na tatizo la upungufu wa maji litakuwa limepatiwa ufumbuzi. Ipo
miji kadhaa ambayo miradi imefikia hatua ya juu na kwamba wakati wowote mwakani itakamilika.
Jiji la Dar es Salaam lipo katika kundi hili. Kazi ya upanuzi wa miradi ya maji ya
Ruvu Juu na Ruvu Chini kwa msaada wa Serikali ya Marekani na mkopo kutoka Serikali
ya India imefikia hatua nzuri. Inatarajiwa kukamilika katika nusu ya kwanza ya mwaka
2015. Mwaka ujao pia visima virefu vya Kimbiji na Kipera vitachimbwa na Bwawa la Kidunda
litaanza kujengwa.
Serikali ya India pia imekubali kutupatia mkopo wa Dola
za Marekani milioni 268.2 kwa ajili ya kugharamia mradi wa kuipatia maji miji ya Tabora,
Nzega na Igunga kutoka Ziwa Victoria. Uwezekano wa kujumuisha miji ya Sikonge na Urambo
katika mradi huo utaangaliwa.
Bunge na Mahakama Ndugu Wananchi; Katika
mwaka 2014, mihimili ya Bunge na Mahakama iliendelea kutekeleza vyema majukumu yao.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeweza kuendesha shughuli zake kama ilivyopangwa
pamoja na kulazimika kugawana Ukumbi ule wa Bunge na Bunge Maalum la Katiba. Bunge
limefanya mikutano mitatu, Miswada 17 ya Sheria ilisomwa kwa mara ya kwanza, Sheria
tano na maazimio saba yalipitishwa. Maswali ya msingi 569 na ya nyongeza 1,541yaliulizwa
na kujibiwa. Aidha, sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow nalo lilijadiliwa na kutolewa
maazimio. Tumeshaanza kuchukua hatua kuhusu maazimio hayo na bado tunaendelea.
Napenda
kuitumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wabunge wetu kwa kutekeleza vizuri wajibu
wao wa Kutunga Sheria na kusimamia Serikali. Nawasihi waendelee na msimamo huo mwema
na chanya kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi; Kwa
upande wa Mahakama napenda kutambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa ya kupunguza mrundikano
wa mashauri katika Mahakama za ngazi zote. Wahenga wamesema “mcheza kwao hutunzwa”.
Hatuna budi kutoa pongezi maalum kwa Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman kwa
uongozi wake mahiri. Chini ya uongozi wake Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa
Mahakama Kuu na Mahakimu Wakazi na Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wamejiwekea malengo
ya kusikiliza na kutoa hukumu kwa mashauri yasiyopungua 200 kwa mwaka kila mmoja wao.
Habari njema na ya kuleta faraja ni kwamba utekelezaji unaendelea vizuri. Mashauri
870 yalisikilizwa na kuamuliwa kwenye Mahakama ya Rufani, mashauri 11,334kwenye Mahakama
Kuu, mashauri 8,715 kwenye Mahakama ya Mahakimu Wakazi na Mashauri 25,683 katika Mahakama
za Wilaya. Aidha, mkakati wa kupeleka timu ya Majaji wa Mahakama Kuu kwa wakati mmoja
kwenye maeneo yenye mashauri mengi kama ilivyofanyika Kigoma, Shinyanga na Tabora
umesaidia sana kupunguza mrundikano wa mashauri ya siku nyingi. Haijawahi kutokea
mashauri mengi kiasi hicho kusikilizwa na kumalizwa katika historia ya Mahakama nchini.
Ndugu
Wananchi; Mkakati huu mpya umeleta matumaini mapya kwamba tatizo la kuchelewesha
kwa mashauri ambalo lilidhaniwa kuwa ni tatizo sugu sasa limeanza kupatiwa ufumbuzi.
Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote natoa shukrani na pongezi nyingi kwa Jaji Mkuu,
Majaji wa Rufani, Jaji Kiongozi, Majaji wa Mahakama Kuu na Mahakimu wa ngazi zote
kwa kazi nzuri waifanyayo.
Hali kadhalika, nampongeza Mtendaji Mkuu wa Mahakama
na watendaji wote wa Mahakama kwa kazi nzuri waifanyayo ya kuwawezesha Majaji na Mahakimu
kutimiza ipasavyo majukumu yao. Hakika utendaji Mahakamani umebadilika na kuwa bora
zaidi. Mimi naahidi kuendelea kusaidia Mahakama kwa kuwahimiza ndugu zetu wa Hazina
kutoa kwa wakati pesa zilizotengwa katika bajeti.
Mapambano Dhidi ya Rushwa Ndugu
Wananchi; Mapambano dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yameendelea
bila ya ajizi. Katika mwaka huu wa 2014 TAKUKURU wamepokea taarifa 237 na wamekamilisha
uchunguzi wa mashauri 545. Watuhumiwa waliofikishwa Mahakamani ni 428. Mashauri yaliyomalizika
ni 205, kati ya hayo 125 watuhumiwa waliachiliwa na 80walipatikana na hatia na kuhukumiwa.
Mwaka huu wa 2014 mali na fedha taslimu zenye thamani ya shilingi bilioni 38.96 zimeokolewa.
Katika kuimarisha Taasisi hiyo kiutendaji, maafisa wapya 394 wameajiriwa.
Sherehe
za Miaka 50 ya Muungano Ndugu Wananchi; Mwaka huu wa 2014 tuliadhimisha
miaka 50 ya Muungano wa nchi zetu mbili yaani Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri
ya Tanganyika kwa heshima inayostahili. Maadhimisho yalifikia kilele tarehe 26 Aprili,
2014 na zilifanyika sherehe nchini kote na sherehe hizo zilifana sana. Ni ukweli usiopingika
kuwa kwa Muungano wetu kuweza kudumu kwa nusu karne ukiwa bado imara na unazidi kustawi
ni mafanikio makubwa. Matumaini kwa siku za usoni ni mazuri. Naamini Muungano wetu
utaimarika zaidi iwapo Katiba Inayopendekezwa itapitishwa kwani yale mambo yenye kuleta
matatizo hivi sasa yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.
Miaka 50 ya JWTZ Ndugu
Wananchi; Wakati nchi inasherehekea miaka 50 ya Muungano, baadhi ya vyombo na taasisi
muhimu kitaifa zilifanya hivyo hivyo. Miongoni mwa walioadhimisha nusu karne ya kuundwa
kwake ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kama mjuavyo JWTZ ilizaliwa tarehe
1 Septemba, 1964. Jeshi letu liliadhimisha siku yao hiyo kwa kufanya zoezi kubwa la
kivita lililoanza Kibaha mkoani Pwani na kumalizikia Monduli Mkoani Arusha.
Nilibahatika
kushuhudia siku ya mwisho ya zoezi hilo. Nilifurahishwa sana na kiwango cha utayari
kivita cha Jeshi letu. Wanajeshi wetu walionesha weledi wa hali ya juu, umahiri mkubwa,
ujasiri, ukakamavu na uvumilivu wa aina yake wakati wa kutekeleza majukumu yao katika
mazingira magumu ya uwanja wa medani za vita. Niliwapongeza siku ile na narudia tena
leo kuwapongeza. Niliyoyaona yamenihakikishia mimi na Watanzania wote kuwa Jeshi letu
la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania liko imara kulinda mipaka ya nchi yetu na kuhakikisha
usalama wa taifa letu na watu wake. Jeshi letu bado ni lile tunalolijua sisi sote,
lakini limezidi lile lililomng’oa mvamizi Dikteta Iddi Amin wa Uganda, tena limezidi
kwa mbali.
Mchakato wa Katiba Mpya Ndugu Wananchi; Mwaka huu
pia tumeshuhudia kukamilika kwa zoezi muhimu la kuandika Katiba Inayopendekezwa. Kama
tujuavyo sote, mchakato uliozaa Katiba Inayopendekezwa ulikuwa na changamoto nyingi
ndani na nje ya Bunge Maalum la Katiba. Pamoja na hayo, Bunge hilo lilikamilisha kazi
yake kwa salama siku mbili kabla ya tarehe 4 Oktoba, 2014 ambayo ndiyo ilikuwa siku
ya mwisho. Mimi na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein tulikabidhiwa
nakala za Katiba Inayopendekezwa tarehe 8 Oktoba, 2014. Nimeshatimiza wajibu wangu
wa kuchapisha katika Gazeti la Serikali na kutangaza siku ya kupiga kura ya maoni
kuwa tarehe 30 Aprili, 2015. Nimeshatoa maagizo kwa Tume ya Uchaguzi kufanya matayarisho
husika ya kuwezesha Kura ya Maoni kufanyika.
Ndugu Wananchi; Moja ya mambo
muhimu ambayo Tume ya Uchaguzi inafanya kwa sasa ni kuandikisha wapiga kura katika
Daftari la Mpiga Kura. Tume imeamua kutumia mfumo mpya wa Biometric Voters Register.
Uandikishaji wa majaribio umefanyika katika baadhi ya Kata katika Majimbo ya Mlele,
Kawe na Kilombero. Matatizo yaliyojitokeza yatasaidia kuboresha mfumo huo kabla ya
uandikishaji wa watu wote wenye sifa stahiki kuanza.
Ndugu Wananchi; Napenda
kutumia nafasi hii kuwafahamisha Watanzania wenzangu wote kuwa mfumo mpya unatengeneza
Daftari Jipya la Mpiga Kura ingawaje lugha inayotumika ni uboreshaji wa Daftari la
sasa. Uboreshaji huu wa Daftari la Mpiga Kura ni tofauti na ule tuliouzoea ambapo
walikuwa wanaandikishwa wapiga kura wapya na wale waliopoteza vitambulisho vyao. Safari
hii wanaandikishwa wote wapya na wa zamani na wote watapata vitambulisho vipya. Hivyo
basi, sisi wenye vitambulisho vya kupiga kura vya zamani tusifanye ajizi, tujitokeze
kujiandikisha wakati ukifika.
Jambo la pili ni kwamba, Daftari la Mpiga Kura
linalotayarishwa siyo kwa ajili ya Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa peke yake,
daftari hilo hilo litatumika pia kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Hivyo basi,
kujiandikisha ni jambo muhimu sana. Usipofanya hivyo siyo tu utajinyima fursa ya kushiriki
kuamua kuhusu Katiba Inayopendekezwa bali pia utakosa fursa ya kuchagua Rais wako,
Mbunge wako na Diwani wako. Katu usikubali yakukose hayo.
Uchaguzi wa Serikali
za Mitaa Ndugu Wananchi; Kama mjuavyo tarehe 14 Desemba, 2014 na 20 Desemba,
2014 ulifanyika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi wa vitongoji, vijiji
na mitaa. Uchaguzi umekwisha na viongozi wamekwishapatikana. Sasa ni wajibu wa viongozi
hao kufanya kazi waliyoiomba. Kwa walioendesha uchaguzi ni wakati mzuri wa kufanya
tathmini ili wapate mafunzo yatokanayo na uchaguzi huo. Kwa TAMISEMI na Wakurugenzi
Watendaji wa Halmashauri, lengo liwe ni kuona namna ya kuimarisha mazuri na kusahihisha
makosa na matatizo yaliyojitokeza. Kwa walinzi wa amani watambue matatizo ya kiusalama
yaliyotokea na kuona namna ya kutengeneza mikakati ya kuzuia matatizo ya namna hiyo
yasijitokeze tena. Hatma ya yote, shabaha yetu ni kutaka kufanya vizuri zaidi katika
chaguzi zijazo za Serikali za Mitaa na kufanya vizuri zaidi katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.
Jumuiya ya Afrika Mashariki Ndugu Wananchi; Mwaka
huu Tanzania imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni zamu
yetu kwa mujibu wa mzunguko wa uongozi wa Jumuiya yetu kati ya nchi wanachama. Ni
dhamana kubwa na kwamba wenzetu wa Afrika Mashariki wanatutegemea tuwaongoze katika
kutekeleza malengo na madhumuni ya Jumuiya kama yalivyoainishwa katika Mkataba ulioanzisha
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hali kadhalika, tunategemewa kuongoza katika utekelezaji
wa maamuzi mbalimbali ya vikao vya Jumuiya. Hii inahusu maamuzi yaliyokwishafanywa
kabla yetu ambayo utekelezaji wake unaendelea na uamuzi mpya utakaofanywa katika kipindi
cha uongozi wetu.
Kwa niaba ya Watanzania wote napenda kuwashukuru ndugu zetu
wa Burundi, Kenya, Rwanda na Uganda kwa kutuamini. Napenda kuahidi kuwa hatutawaangusha.
Sisi Watanzania tutafanya kila tuwezalo kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa
manufaa ya Jumuiya yenyewe, nchi zetu na wananchi wa Afrika Mashariki. Tutajitahidi
kuwa wabunifu kwa nia ya kuona utangamano unakua na kustawi kwa kasi na kuzaa matunda
ya maendeleo tunayoyatarajia sote. Matunda tuliyoyatarajia tulipoamua kuanzisha Jumuiya
hii na matunda tuliyoyapata tulipoamua kwa hiari yetu kujiunga nayo kuwa wanachama.
SADC, AU NA UN Ndugu Wananchi; Kuhusu Jumuiya ya Maendeleo ya
Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa, tunaahidi kuendelea
kuwa wanachama waaminifu na kushiriki kwa ukamilifu katika utekelezaji wa shughuli
mbalimbali za mashirika haya ya kikanda na kimataifa. Kwa upande wa SADC tutaendelea
kushiriki katika utekelezaji wa mikakati na mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii
na ile ya kisiasa na kiusalama kama ilivyoainishwa katika RISDP (Regional Indicative
Strategic Development Plan) na SIPO (SADC Strategic Indicative Plan for the Organ).
Kwa ajili hiyo Tanzania, itaendelea kutoa mchango wake katika kukuza utangamano wa
kiuchumi katika SADC na kusaidia kuimarisha uhusiano mwema na usalama miongoni mwa
nchi wanachama wa SADC. Hii ni pamoja na kusaidia katika kutatua migogoro ya kisiasa
na kusalama kati ya nchi wanachama.
Kwa upande wa Umoja wa Afrika tutaendelea
kutekeleza maamuzi ya vikao na taasisi mbalimbali za Umoja huo. Daima tutakuwa wanachama
waaminifu wa Umoja wa Afrika na kuchangia katika uimarishaji wake. Kuhusu Umoja wa
Mataifa tutaendelea kutimiza wajibu wetu kama wanachama wa Umoja huo wa kimataifa
ulio adhimu na muhimu kwetu na dunia nzima. Tutaendelea kushiriki katika shughuli
za ulinzi wa amani chini ya Umoja wa Mataifa. Hivi sasa tunao wanajeshi wetu katika
majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo, Sudan na Lebanon. Tuko tayari wakati wote kuchangia zaidi iwapo Umoja wa
Mataifa watatutaka tufanye hivyo.
Hitimisho Ndugu Wananchi; Namaliza
hotuba yangu hii ndefu kwa kuwashukuru Watanzania wote kwa kuiunga mkono Serikali
yetu na kwa mchango wenu uliowezesha nchi yetu kupata mafanikio haya makubwa tunayojivunia
katika mwaka 2014. Tumeweza kuvuka mitihani na nyakati zenye majaribu mengi. Umoja
wetu na mshikamano wetu ndivyo vilivyotuwezesha kufika hapa. Tunauanza mwaka 2015
kwa matumaini makubwa. Mwaka 2015 unatupa fursa kubwa ya kuendelea kuliimarisha zaidi
taifa letu. Mwaka ujao ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo huenda ukawa na changamoto
na majaribu magumu zaidi kuliko mwaka huu. Uelewa wetu, umoja wetu, mshikamano wetu
na moyo wetu wa uzalendo ndivyo vitakavyotuvusha kama ilivyokuwa kwa miaka ya nyuma.
Mimi nina imani kubwa kwa uwezo na utayari wa Watanzania wenzangu kuidumisha sifa
nzuri ya nchi yetu ya umoja na mshikamano wa watu wake uliozaa amani na utulivu. Tumeweza
mwaka huu na miaka ya nyuma, tutaweza tena mwakani na miaka ijayo. Inawezekana, Timiza
Wajibu Wako! Nawatakia heri ya mwaka mpya. Mungu Ibariki Afrika! Mungu Ibariki
Tanzania! Asanteni kwa kunisikiliza.