2015-01-02 10:34:46

Ebo! Mvi si dalili za hekima!


Hekima ni mradi wa uzee utokanao na mang’amuzi marefu ya maisha. Wazee wanayo hekima, hivi maneno yao yamejaa busara. Neno la busara katika mazungumzo ya wazee linatokana na hekima waliyo nayo. Kwa hiyo ni ngumu kuutenganisha uzee, hekima na neno wanalozungumza, ndiyo maana tunasema: “Penye wazee haliharibiki neno.”

Neno kwa lugha ya kilatini huitwa verbum, na kwa kigiriki ni logos. Ukifuatilia kidhati logos maana yake ni mradi, kusudi, nia, malengo, sayansi, elimu au hekima. Kisarufi ya kilatini na kihebrania, neno hili Hekima lipo katika hali ya kike na kwa kigiriki ni Sofia, ndiyo maana jina hili wanapewa wanawake tu.

Hekima ya Mungu unaiona katika Neno lake umbaji. Hekima yake iko daima na Mungu mwenyewe na ni ngumu kumtenganisha Mungu na hekima na Neno lake umbaji. Angalia jinsi hekima inavyotamba: “Mungu alipozithibitisha mbingu nalikuwepo. Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu;…Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.” (Methali 8:27-32).

Mwinjili Yohane, hatumii msamiati wa hekima, bali anatumia neno la kigiriki Logos, ili aweze kuwasilisha picha hiyo ya mradi wa hekima iliyojimwilisha na kuwa mtu, Yesu wa Nazareti. “Neno alitwaa mwili akakaa kwetu”. Kwa hiyo kilele cha hekima ya Mungu iliyojimwilisha ndiyo Neno au logos ile iliyojifanya kuwa mmoja kama sisi. Hebu tuone matendo mengi yanayoweza kufanyika na hekima ya Mungu iliyojimwilisha: “Kila kitu kilifanyika kwa njia yake.” Baada ya kuumba ulimwengu, akaona kila kitu ni chema.

Aidha, ukiupembua kwa dhati mradi huo wa uumbaji, utamkuta binadamu peke yake ndiye anayeweza kuelewa kwa sababu anaweza kujipambanua na kujipembua. Binadamu anapoupembua ulimwengu kwa jicho la kisayansi peke yake, hapo anafika kwenye kufahamu sheria za kimaumbile zinazomwezesha kuutumia huo ulimwengu. Lakini pia, ni binadamu peke yake anayetaka kuufahamu ulimwengu zaidi, kuutumia ipasavyo na kuupatia maana.

Mathalani, maisha yanatufundisha bila sisi wenyewe kujua hasa tunapopambana na magumu, magonjwa, utata fulani, tunapodanganywa na kujikuta katika matatizo tunakimbilia kuitumia hekima na kuhoji: “hebu tumia busara kidogo, Je, unaona kuna maana yoyote ya mambo uliyoyatenda?” Bila ya kujihoji hivyo, yaani mwanzo (kuzaliwa), mateso yetu na kufa, na kila kitu vinakosa maana (hekima) kwa vile havina mwumbaji wake ambaye ni hekima.

“Hekima hiyo ilikuwa ni uzima, na uzima ulikuwa ni mwanga wa binadamu.” Katika kigiriki kuna maneno mawili yanayomaanisha uzima: Kuna neno bios (baiolojia) lenye maana ya uzima, uhai unaoweza kufa na neno jingine ni zoe, lenye pia maana ya uzima na uhai usio na mwisho. Katika Agano jipya neno hilo zoe linametajwa mara 135. Nusu ya idadi hiyo iko katika injili ya Yohane. Neno hilo ambalo lilikuwa toka mwanzo, ambalo ni hekima ndilo linalofasiriwa kuwa ni Zoe.

Yohane anasema, uzima wa kibaolojia (bios) una kikomo lakini zoe ni uzima usio kikomo, na uzima huo ndiyo mwanga kwa wanadamu. Tora ilikuwa ni mwanga uliowaongoza wayahudi, “Neno lako ni mwanga katika njia zangu” au “Katika mwanga wako tunaona mwanga”. Tora hiyo lakini, ilikuwa ni sheria za Mungu zilizoandikwa.

Yesu kumbe ni Tora ya Agano jipya ambayo siyo kitabu tena kilichoandikwa, bali ni Mwana wa Mungu aliye hekima, Neno, aliye nafsi hai yenye uzima. Na Uzima huo ndiyo Mwanga aliotoa Mungu baba kwa watoto wake binadamu. Mwanga huo hauko nje yetu, bali ndani mwetu. Sheria na kitabu vinamwongoza mtu toka nje, bali uzima (hekima), mwanga upo ndani ya binadamu.

Ni binadamu peke yake anao uwezo wa kutambua kuwa Neno au Hekima hiyo ni mwanga unaoangaza maisha yake. Aidha, ni binadamu peke yake anao uwezo wa kuunganisha na kugundua ukweli upi unaendana na kutosheleza mahitaji anayoyatarajia. Binadamu daima anachakalika kutafuta mradi, au ukweli, na hekima aliyopewa ya utambuzi haiwezi kamwe kutulia kama hafaulu kulinganisha mwanga au hekima hiyo na neno, mradi au uzima. Ama kweli“Hekima inawalipa wenye haki ujira wa kazi”.

Ingawaje mwanga huo daima unapata vikwazo, yaani unakinzana na giza, lakini mwisho mwishoni, “Giza halitaweza kuushinda”. Mwanga au hekima hiyo ilipoingia ulimwenguni na kuwa mwili, haukuweza kutambulikana. “Mwanga huo ulifanywa kwa ajili ya ulimwengu, lakini ulimwengu huo haukuutambua”. Hapa haimaanishi kwamba akili ya kisayansi haikumtambua alipofika la hasha, alionekana na alitambuliwa.

Lakini hapa kutambua kunamaanisha “kuikiri” kwamba hekima hiyo inaendana na utu wa binadamu, na inayo hadhi na ubinadamu wetu, yaani kukiri alama za uwepo wake, katika tamaduni mbalimbali, katika desturi za watu mbalimbali hata kama alama hizo zinavurugwa na giza na uovu mbalimbali.

Kwa hiyo hekima maana yake ni kuipokea na kuikiri Hekima ya Neno la iliyojifanya mtu na kuiishi. Zawadi anayotuahidia ni hii kwamba tukiitambua Hekima yake na kuishuhudia itatufanya tuwe watoto wake. “Wale walioipokea wakafanywa kuwa watoto wa Mungu. Naye atafanya makao yake kwetu. Ndipo litakapotimia neno lile kuu kwamba “Neno likafanyika mwili na kujenga hema yake kwetu.” Au Neno la Mungu akatwaa mwili, akakaa kwetu”.

Ndiyo maana ya Noeli kwamba Hekima imejifanya mwili, neno limechukua kila aina ya udhaifu wa binadamu, limejikita moja kwa moja kwa kila hali ya maisha ya binadamu hadi kifo. Lengo la ukweli huo ni kutaka kutuonesha kuwa hilo ndilo lengo kuu la hekima ya Mungu toka mwanzo, yaani “kujenga hema yake kwetu” kama ilivyokuwa katika Kutoka. Mungu alikaa pamoja na watu ake daima katika hema ya wayahudi safarini, utumwani na popote. Kwamba Mungu hawezi kukaa bila ya kuwa na watu wake.

Kwa hiyo mradi wa Mungu katika kujimiwilisha kwa Neno ni kupiga Hema na kukaa nasi daima katika maisha yetu. “Hema ya Mungu ipo nasi na itabaki nasi daima. Hivyo hakutakuwa tena maovu, uchungu, kifo. Katika fumbo la Noeli tunaalikwa kuutafakari mradi huo wa Mungu. Mwanzo wake yaani pale alipopiga Hema la kwanza pale Betlehemu pangoni, na kuendelea kuyafanya maisha yetu kuwa Hema yake, na hatimaye kutufikisha kwenye Hema Takatifu isiyoweza kubomolewa kamwe.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.