Simameni kidete kupambana na mifumo yote ya utumwa!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, katika Maadhimisho ya
Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 48 ya kuombea amani duniani,
kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican tarehe Mosi, Januari 2015 amemwelezea
Bikira Maria kuwa ni mwanamke mnyenyekevu aliyekubali Neno wa Mungu kutungwa mimba
tumboni mwake, kiasi kwamba, si rahisi kuweza kutenganisha Bikira Maria na Yesu!
Bikira
Maria amemkiria Yesu Mwana wa Mungu ubinadamu wake, kiasi hata cha kuzaliwa chini
ya sheria, ili aweze kumkomboa mwanadamu kwa njia ya sheria, inayomweka mtu huru na
kuzaliwa tena kama mwana mpendwa wa Mungu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake
na kwa njia ya Ubatizo, aweze kufanyika kuwa ni mtoto mteule wa Mungu; tukio linalowaunganisha
Wakristo kuwa viumbe hai katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.
Siku
ya kwanza ya Mwaka, iwe ni fursa ya kukumbuka ile Siku ya Ubatizo, pale waamini walipozaliwa
upya kwa maji na Roho Mtakatifu, kwa njia ya Mama Kanisa na Bikira Maria ni mfano
kamili wa umama huu. Ubatizo unawaunganisha na Mungu na hivyo kupokea upendo, upole
na huruma kutoka kwa Mwenyezi Mungu, chemchemi ya amani ya kweli inayowafanya huru
na wala si watumwa, bali ndugu, kauli mbiu ya ujumbe wa Siku ya Kuombea Amani Duniani
kwa Mwaka 2015.
Watu wote wanahamasishwa kupambana na mifumo mbali mbali ya
utumwa, ili kujenga na kudumisha udugu, kila mtu kadiri ya dhamana na madaraka aliyo
nayo!
Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko amewatakia
wote amani, furaha na baraka tele kwa Mwaka Mpya. Amewapongeza kwa namna ya pekee
watoto kutoka Ujerumani, Austria na Uswiss ambao wametembea nyumba hadi nyumba kwa
ajili ya kutafuta fedha ya kusaidia kugharimia miradi kwa ajili ya watoto wanaoishi
katika mazingira magumu.
Baba Mtakatifu anawashukuru wote walioshiriki katika
maandamano ya kuombea amani kitaifa, nchini Italia, yaliyofanyika Jimboni Vicenza,
Kaskazini mwa Italia, ili kuombea amani duniani kote, utume ambao umetekelezwa na
majimbo mbali mbali duniani. Baba Mtakatifu amewakumbuka pia wahanga wa vita kuu za
dunia na kwamba, anatumaini kuwa hakutakuwepo tena na vita na badala yake, amani na
udugu vitaweza kutawala kati ya watu.