Jubilee ya miaka 450 tangu kuundwa kwa mji wa San Sebastiano Rio de Janeiro, Brazil,
kumbu kumbu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2013 na miaka 50 tanu
Mwenyeheri Papa Paulo VI alipowasha taa kwenye Sanamu ya Kristo Mfalme, iliyotundikwa
kwenye kilele cha Mji wa Rio de Janeiro ni matukio ambayo yamegusa sakafu ya moyo
wa Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa wananchi wa Brazil, wanaoadhimisha
kumbu kumbu ya matukio haya muhimu katika historia yaliyozinduliwa katika mkesha wa
Mwaka Mpya 2015.
Baba Mtakatifu anasema miaka 450 si haba! Hii ni historia
ya watu wenye ujasiri na furaha na kamwe hawakuacha kutikiswa na magumu ya maisha,
bali wameendelea kuonesha ushuhuda wa imani tendaji kwa Kristo na Kanisa lake, kama
alivyofanya Mtakatifu Sebastiani, Mlinzi wao. Hii ni historia inayojikita katika imani
na matumaini kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kuendelea kuonesha uchaji, huku wakitumainia
huruma yake.
Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kubahatika kuwa na mji wenye maajabu
yanayowashangaza wengi, lakini pia kuna umaskini unaotia giza uzuri na maajabu ya
mji huu, kutokana na ukosefu wa usawa kijamii; kuna uhalifu wa kutisha, ukosefu wa
haki pamoja na kundi kubwa la watu ambao wanatamaduni maalum; yote haya yasiwafanye
watu kupoteza matumaini, kwani Mwenyezi Mungu yupo pamoja nao na kwamba, Yesu Mkombozi
hawezi kamwe kufumbia macho mateso na mahangaiko ya watu wake.
Mikono yake
wazi, inawachangamotisha waamini na watu wenye mapenzi mema kuvuka vikwazo vya kinzani,
ili kujenga mji unaosimikwa katika umoja, mshikamano, haki na amani! Watu wajenge
utamaduni wa kujadiliana, ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwani kila
mwananchi analo jambo ambalo anaweza kuchangia katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni
wa haki na udugu. Watu wanaweza kujifunza kujenga moyo wa ukarimu na mshikamano kutoka
kwa watu wa kawaida kabisa. Brazil bado ina mchango mkubwa katika ustawi na maendeleo
ya ulimwengu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Kardinali Oran
Tempesta kwa kumpatia nafasi ya kutoa ujumbe kwa wananchi wa Brazil wakati huu wanapoadhimisha
Jubilee ya miaka 450 tangu kuanzishwa kwa mji wa Rio de Janeiro. Anawatakia wote heri
na baraka kwa Mwaka Mpya wa 2015, anawaomba kumsindikiza kwa sala na sadaka zao katika
maisha na utume wake.