2015-01-01 11:55:24

Bikira Maria ni Mama wa Mungu, Kanisa na Watu wote!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe Mosi, Januari 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa k Takatifu kwa ajili Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, sanjari na maadhimisho ya Siku ya 48 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2015, inayoongozwa na kauli mbiu "Si tena watumwa, bali ndugu".

Baba Mtakatifu mwanzoni mwa Mwaka Mpya wa 2015 ametafakari kwa kina kuhusu baraka ya Bikira Maria inayotajwa na Elizabeth, kama sehemu ya mwendelezo wa baraka ya kikuhani, ambayo ilikuwa inatolewa kwa Waisraeli, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwabariki, kuwalinda, kuwaangazia nuru na kuwainulia uso wake na hatimaye, awakirimie amani. Bikira Maria ni utimilfu wa baraka hizi, aliyependelewa na Mwenyezi Mungu kiasi hata cha kumwangazia uso wake na kumjalia Mwana wa pekee, ambaye kila mwanadamu anaweza kumtafakari.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wanaweza kumsifu na kumtukuza Yesu Kristo kama walivyofanya wachungaji waliporudi kutoka Bethlehemu huku wakishangilia baada ya kumwona Mtoto na Mama yake; hija ambayo imekamilika pale Mlimani Kalvari; mahusiano yanayojionesha kwa namna ya pekee kati ya mtoto na mama yake. Mwili wa Yesu Kristo uliotungwa mimba tumboni mwa Bikira Maria ni chanzo cha ukombozi wa mwanadamu, ndiyo maana Bikira Maria anaitwa Mama wa Mkombozi, aliyethubutu kushiriki maisha na utume wake, hadi pale Mlimani Kalvari.

Umoja na mshikamano huu kati ya Bikira Maria na Yesu unafumbatwa katika undani ya moyo wake, katika imani na kurutubishwa kwa njia mang'amuzi ya kimama, ndiyo maana Bikira Maria anajulikana kuwa ni Mama mwenye imani thabiti, aliyetoa nafasi ya kwanza moyoni mwake kwa uwepo wa Mungu na mipango yake; ni mwamini mwenye uwezo wa kukubali kupokea zawadi ya Mwana pekee, tukio linaloonesha utimilifu wa nyakati, Mwenyezi Mungu alipoingia katika historia ya wokovu, ndiyo maana, mtu hawezi kumfahamu vyema Yesu, pasi na kumfahamu Bikira Maria.

Baba Mtakatifu anasema huwezi kumtenganisha Kristo na Kanisa lake na kwamba, mtu hawezi kufahamu ukombozi ulioletwa na Yesu bila kutambua Umama wa Kanisa; huwezi kumpenda na kumsikiliza Kristo, bila kulipenda na kulisikiliza Kanisa kwani Kanisa na Kristo ni chanda na pete kama anavyosema Mwenyeheri Paulo VI.

Kanisa ni Familia kubwa ya Mungu inayowapeleka watu kwa Kristo, kwani imani ya Kikristo inajikita katika mahusiano na Yesu Kristo na wala si jambo la kufikirika. Yesu Kristo aliteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu na yuko hai kati ya watu wake, ndiye yule Mwana Kondoo wa Mungu ambaye Kanisa linaendelea kumtangaza na kumwadhimisha kwa njia ya Sakramenti, chemchemi ya neema na baraka; hii ni kazi na utume unaofafanua umama wa Kanisa, kwa kumlinda Mtoto Yesu na kumpeleka kwa wengine kwa furaha na ukarimu.

Yesu Kristo ni nguzo thabiti ya maisha na utume wa Kanisa; bila Kanisa, Yesu atabakia kuwa ni wazo la kufikirika, hali ya kujisikia au kanuni maadili tu! Mahusiano ya waamini na Kristo yanajikita katika uhalisia wa maisha anasema Baba Mtakatifu Francisko! Yesu ni baraka kwa kila mtu na kwa binadamu wote, utume ambao Watu wa Mungu wanatumwa kuutekeleza kwa kutoa baraka ambayo imemwilishwa katika Kristo.

Bikira Maria ni mfuasi amini wa Yesu, kielelezo cha Kanisa linalosafiri, Mama anayefungua njia kwa ajili ya umama wa Kanisa; anaenzi utume wa Kanisa unaoelekezwa kwa wengi; ushuhuda na umama wa Bikira Maria umeendelea kuambatana na Kanisa tangu mwanzo anasema Baba Mtakatifu Francisko. Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa, ni Mama wa wote, aikirimie familia ya binadamu baraka na kwa namna ya peke mwanzoni kabisa mwa mwaka mpya, Kanisa linaposali kwa ajili ya kuombea amani duniani kwa kuongozwa na kauli mbiu "si tena watumwa, bali ndugu".

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria ili aweze kuombea ili amani ipatikane katika mioyo ya watu, katika familia na amani kati ya mataifa. Watu wote wanahamasishwa kuwa huru na kuendelea kuwa ni watoto, kila mtu mintarafu wajibu na dhamana yake, aweze kupambana kufa na kupona dhidi ya mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu anawaalika watu kutoka katika jamaa, tamaduni na dini kuunganisha nguvu dhidi ya utumwa, kwa kutambua kwamba, wote ni ndugu kwa njia ya Yesu aliyejifanya kuwa Mtumishi wa wote! Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza Mababa wa Kanisa waliothubutu katika mkutano wa Efeso kutangaza kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu, "Theotokos" bila woga licha ya vistisho vilivyokuwa vinawazunguka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.