2014-12-31 10:21:59

Viongozi wa Kanisa waliouwawa kikatili kwa Mwaka 2014


Shirika la Habari za Kimissionari, Fides, katika taarifa yake, linaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2014, viongozi 26 wa Kanisa wameuwawa sehemu mbali mbali za dunia, sawa na ongezeko la viongozi watatu, ikilinganishwa na takwimu za mwaka 2013. Amerika imemwaga damu ya viongozi wengi wa Kanisa kwa mwaka 2014.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, yaani kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2013, kuna viongozi wa Kanisa 230 waliouwawa kikatili na kati yao kuna Maaskofu watatu. Hawa ni viongozi waliopoteza maisha yao huku wakiwatangazia Watu wa Mungu Injili ya Furaha, Imani na Matumaini. Ni watu waliojisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kuna viongozi wa Kanisa waliofariki dunia huko Sierra Leone na Liberia wakati wakiwahudumia wagonjwa wa Ebola. Ni watu waliokumbana na kifo uso kwa uso, lakini bila kukata tamaa kwa ajili ya huduma kwa maskini. Viongozi wa 26 wa Kanisa waliopoteza maisha, kati yao kuna mapadre 17, watawa 7, mseminaristi mmoja na mlei pia ni mmoja. Viongozi 14 wameuwawa Barani Amerika, viongozi 7 wamepoteza maisha Barani Afrika; Asia ni wawili, Oceania nako ni viongozi wawili na Ulaya Padre mmoja ameuwawa kikatili.

Hawa wote ni mashuhuda wa huduma ya upendo kwa Mungu na jirani, waliyoitekeleza kwa moyo mnyenyekevu. Taarifa zinaonesha kwamba, wengi wa viongozi hawa wa Kanisa wameuwawa kutokana na matukio ya wizi na ujambazi wa kutumia silaha; kielelezo makini cha kumong'onyoka kwa tunu msingi za kimaadili na utu wema; ni hali ya watu kukata tamaa kutokana na umaskini wa hali na mali na hivyo matukio kama haya yanakuwa ni njia ya mkato kwa ajili ya kutafuta maisha. Ni matukio ambayo wakati mwingine yanaonesha ukosefu wa maridhiano ya kitamaduni na kiimani kati ya watu.

Fides inaonesha pia taarifa za kutia moyo kwamba, baadhi ya wahusika katika mauaji ya viongozi wa Kanisa wametiwa mbaroni na haki imetendeka. Huko Argentina, baada ya miaka thelathini na minane kupita tangu Askofu Enrique Angelelli alipouwawa, hivi karibuni wahusika wamehukumiwa na wameanza kutumikia kifungo chao. Wahusika wa mauaji ya Askofu Luigi Locati, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Isiolo, Kenya aliyeuwawa kikatiliki kunako mwaka 2005 wamekamatwa na kupatikana na hatia na tayari wanatumikia adhabu yao gerezani.

Hata hivyo, Mama Kanisa bado anaendelea kusubiri kwa imani na matumaini kuona baadhi ya viongozi wa Kanisa waliotekwa nyara tangu mwaka 2012 huko Kivu, DRC ambao hadi sasa hawajulikani walipo, wanaachiliwa huru, ikiwa bado wako hai. Kanisa bado linangoja kwa hamu kusikia hatima ya Padre Paolo Dall'Oglio aliyetekwa nyara huko Syria kunako mwaka 2013 bila ya kumsahau Padre Alexis Prem Kumar aliyetekwa nyara huko Herat, nchini Afghanstan.

Orodha hii ya majina ya viongozi wa Kanisa waliouwawa, inapaswa kuboreshwa kwa kuongezea majina ya vongozi wa Kanisa ambao pengine hawatakumbukwa wala kutajwa, lakini bado wanateseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.