2014-12-31 10:32:12

Vijana ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni mkusanyiko wa Makanisa ya Kikristo yapatayo 349 yanayowaunganisha Wakristo millioni 560 kutoka katika nchi zaidi ya mia moja duniani. Ni Makanisa yanayomkiri Yesu Kristo kuwa ni Mungu na Mwokozi kadiri ya Maandiko Matakatifu na kwa pamoja wanataka kulipatia Fumbo la Utakatifu Mtakatifu: utukufu, sifa na heshima.

Baraza la Makanisa linaendelea kujibidisha katika mchakato wa kutafuta umoja kamili miongoni mwa wafuasi wa Kristo, kwa kuungama na kuadhimisha Mafumbo ya maisha na utume wa Kanisa kwa pamoja, ili walimwengu waweze kumwamini Yesu Kristo! Kwa sasa Baraza la Makanisa linajikita katika hija ya haki na amani kama kielelezo cha ushuhuda wa umoja na mshikamano kati ya Wakristo na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawaridhia.

Kwa njia ya Sala na huduma makini kwa binadamu, Baraza la Makanisa linapenda kumshuhudia Kristo, kwa kumwilisha Heri za Mlimani katika huduma zake, kwani watu wengi wana kiu ya haki na amani; zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa pamoja wanaweza kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, kusali na kudumisha misingi ya haki na amani, ili kweli zawadi ya amani inayotolewa na Mwenyezi Mungu iweze kutua na kujikita katika mioyo ya watu duniani.

Hizi ni salam na matashi mema kutoka kwa Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni alizowaandikia vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè wanaokusanyika mjini Prague, Jamhuri ya Watu wa Czech, kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana wa Bara la Ulaya.

Baraza la Makanisa linaendelea kuhamasisha umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani kwa kutambua kwamba, watu wote wanahitajiana na kutegemeana kwa hali na mali. Kumbe kuna haja ya kushirikiana katika kutafuta, kulinda na kudumisha misingi ya amani kwa wote, lakini zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawakumbusha vijana kwamba, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa; wawe ni madaraja na wajenzi wa misingi ya haki, amani na mshikamano kati ya watu; wawe ni wadau katika mchakato wa kuhamasisha imani, mapendo, usawa; haki msingi za binadamu pamoja na haki jamii. Baraza la Makanisa linaendelea kusali, ili ufalme wa Mungu uweze kujengeka kati ya Watu wa Mataifa.

Ulimwengu mamboleo unawahitaji mashuhuda wa imani wanaomwilisha imani hii katika maisha, dunia inawahitaji vijana wenye imani thabiti, tayari kujisadaka ili kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa katika ulimwengu wa utandawazi ambamo, watu wengi wanamezwa na malimwengu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawapongeza vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè ambao kuanzia tarehe 29 hadi tarehe 2 Januari 2015 wanakusanyika mjini Prague, nchini Czech.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.All the contents on this site are copyrighted ©.